HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 29, 2019

Kilimo chashusha thamani ya misitu

Mkurugenzi Mkuu wa TFCG, Charles Meshack.
Na Suleiman Msuya, Morogoro

UWEKEZAJI kwenye sekta ya kilimo nchini ni moja ya sababu ya kushuka kwa thamani ya rasilimali misitu katika vijiji.

Hayo yameanishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack (pichani), wakati akizungumza kwenye mkutano Mkuu wa 19 wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi Misitu Tanzania (Mjumita) uliofanyika mkoani Morogoro.

Alisema kwa siku za karibuni jamii imejikita kwenye uwekezaji wa kilimo hali ambayo inachangia upotevu wa misitu ya asili.

Meshack alisema mara nyingi Serikali imeendelea kuruhusu mashamba kutolewa kwenye misitu ya vijiji bila kujali thamani ya misitu hiyo na kusababisha  ekari laki 469 kupotea kila mwaka.

Alisema ipo haja ya wadau wa misitu kuendelea kuonesha thamani ya mazao ya misitu kwa jamii  ikiwemo vijiji kunufaika na kuachana na dhana ya kutegemea kilimo katika masuala ya maendeleo.

"Misitu ina thamani kubwa sana iwapo mnyororo wa mazao yake utatumiwa vizuri na hilo litafanikiwa iwapo Serikali itatambua fursa zilizopo," alisema.

Aidha alisema nguvu za wadau katika kufanya Usimamizi Shirikishi na uhifadhi wa Misitu (USM) zimeendelea kuonekana licha ya Serikali kuwa na uwekezaji mdogo katika usimamizi huo.

Meshack alisema wakati umefika kwa  mfumo wa usimamizi misitu unaotekelezwa na Mjumita kuendelezwa nchi nzima ili kutetea misitu ya asili iliyobaki ambayo huenda ikapotea ndani ya miaka 40.

Mkurugenzi huyo  aliishauri Mjumita kuendelea kutenga misitu hiyo ili kumilikiwa na wananchi wenyewe na kuendelea kunufaisha jamii.

Awali Ofisa Misitu Mkoa wa Morogoro Josephat Chuwa, alisema misitu iliyopo haijapewa thamani inayolingana nayo jambo ambalo linapaswa kuangaliwa upya.

Chuwa alitolea mfano Misitu ya Tao la Mashariki ambayo imekuwa ikichukua nafasi kubwa katika kuinua uchumi wa nchi lakini usimaizi wake sio wa kuridhisha.

Alisema misitu hiyo inachangia upatikanaji wa maji kwa asilimia 25 ya wakazi wanaoishi kwenye maeneo hayo, asilimia 60 ya nishati ya umeme na asilimia 75 maji yanayoenda jijini Dar es Salaam kwa matumizi ya kawaida na  viwanda.

Alisema ni vema jamii ikafahamu umuhimu wa utunzaji wa misitu na kuona kwamba hakuna misitu hakuna huduma hizo muhimu kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

Pages