Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia Wahitimu wa Chuo cha IFM, kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam Novemba 29, 2019.
Na Mwandishi Wetu
“Natambua kwamba baadhi ya wahitimu wamepata mkopo kutoka
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, hivyo natumia fursa hii kuwakumbusha
wale wote mlionufaika na mkopo wa Serikali katika kutimiza ndoto zenu za kupata
elimu ya juu, mkumbuke kurejesha mikopo,” amesema.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 29, 2019) wakati akizungumza kwenye mahafali
ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila
anayenufaika na mkopo asaidie wengine walio nyuma yake ili nao waweze kufaidika
na utaratibu huo wa kukopa na kulipa. Alisisitiza kwamba bila
kufanya hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa Serikali itashindwa kuwajengea uwezo
wananchi wake wa kupata fursa zinazojitokeza za elimu katika ngazi
mbalimbali.
“Ikumbukwe kuwa, maendeleo ya Taifa lolote yanategemea
uwekezaji katika rasilimali watu. Hivyo nitoe rai kuwa wote mliokopeshwa na
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu mfanye hima kulipa,” alisema
Majaliwa
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wahadhiri na wanachuo wa vyuo
vikuu na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam wachangamkie fursa ya
kupata nyumba na vyumba vya kupangisha katika miradi ya ujenzi wa nyumba ya
NSSF, NHC na Watumishi Housing zilizopo Kigamboni.
Amesema
amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF atenge maghorofa ambayo yatakaliwa na wahadhiri na
wanafuzi wa vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu tena waache kuwatoza bei kubwa
na badala yake wapange bei mpya za kupangisha ambazo wanachuo watazimudu.
Ili
kufanikisha utekelezaji wa jambo hilo, Waziri Mkuu amesema
amewashauri viongozi wa taasisi za elimu ya juu za mkoa wa Dar es Salaam wafanye
mawasiliano na Watendaji Wakuu wa NSSF, NHC na Watumishi Housing ili
wafikie makubaliano ya namna ya kupangisha au kununua nyumba hizo.
Akizungumzia
suala la kuboresha usafiri kwa wanafunzi na watu wakaoishi kwenye nyumba
hizo, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari amekwishatoa maelekezo kwa
viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Kigamboni na
Temeke wakutane na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) ili wapange
safari za mabasi ya abiria kutoka Tuangoma, Mtoni Kijichi hadi eneo la Ferry
Kigamboni.
Mheshimiwa
Majaliwa amewasihi wahadhiri na wanachuo wachangamkie fursa hiyo ili waweze kupata
nyumba bora za kupanga au kununua ili kuepuka adha ambayo imewakabili kwa muda
mrefu ya kupanga au kuishi katika nyumba duni.
Akiwaasa wahitimu wa Mahafali hayo, Mheshimiwa
Majaliwa alisema: “Mnao wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mnatumia vizuri
elimu mliyoipata chuoni ili kuchochea maendeleo ya kweli ya nchi
yetu. Hivyo basi, huko mnakoenda iwe ni kwenye Halmashauri, Mikoa, Wizara, taasisi
za umma na hata sekta binafsi, mkawe chachu ya mafanikio.”
“Aidha, mtakapokuwa huko kwenye maeneo mbalimbali ya kazi,
hakikisheni mnajitanabaisha kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.
Tunawatarajia muwe mfano kwa kuwa waadilifu, waaminifu na wachapa kazi,”
alisema Mheshimiwa Majaliwa.
Aliwasihi
wahitimu hao kuwa watakapoingia kwenye utumishi wa umma au kwingineko
wakazingatie maadili na kujiepusha na tabia ya kujitafutia utajiri wa
harakaharaka. “Kafanyeni Kazi kwa uzalendo wa hali ya juu,” aliongeza
Mheshimiwa Majaliwa.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza
katika mahafali hayo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango alisema
ili Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kiweze kuwa chachu ya mabadiliko makubwa
ya kiuchumi yanayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, ni lazima uongozi wa chuo
hicho utekeleze sera ya elimu kwa vitendo na kuwa wabunifu katika kupitia upya
mitaala, ufundishaji na kufanya tafiti.
Waziri Mpango
amelitaka Baraza la Uongozi wa Chuo cha IFM na wanataaluma waendelee kuwa
wabunifu zaidi ili kuhakikisha kwamba fani zinazofundishwa Chuoni hapo
zinaendana na wakati huku wakizingatia mahitaji ya nchi na wananchi wake pamoja
na mabadiliko ya haraka ya kitekinolojia yanayoendelea ulimwenguni.
Jumla ya
wahitimu 2,775 wametunukiwa tuzo mbalimbali na wanafunzi 20 wa Shahada ya
Usimamizi wa Fedha wamepongezwa.
No comments:
Post a Comment