November 27, 2019

PROF. NDALICHAKO: TUMIENI HATA POSHO ZA WATUMISHI KUKAMILISHA UJENZI VETA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA Ndolage mkoani Kagera. (Picha na Alodia Dominick).
 

Na Alodia Dominick, Muleba

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema  haridhishwi na kasi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA Ndolage, kilichopo Kata ya Kamachumu Kijiji cha Bushagara mkoani Kagera.

Prof. Ndalichako ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa chuo hicho uliofanyika Novemba 27, 2019, amesema ujenzi uliofanyika chuoni hapo haukuwa na thamani ya fedha iliyotolewa na wizara yake.

 "Haiwezekani Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA, thamani ya fedha hizo haionekani. Licha ya changamoto zilizotajwa chuoni hapa, Serikali haitatoa fedha zozote mpaka ujenzi huo ukamilishwe na VETA kabla ya Juni mwakani", amesema Prof. Ndalichako.

Amemtaka  Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Taifa, Peter Maduki, kutumia hata posho za watumishi wa Veta ikiwezekana ili kukamilisha ujenzi wa chuo hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Pankrasi Bujuro, amesema chuo hicho ni miongoni mwa vyuo 10 nchini vilivyopata fedha ya Serikali kiasi cha Sh. Bilioni 4, ambapo chuo hicho kilipata Sh. Milioni 281.5 kutoka serikalini kwa ajili ya ujenzi huo.

Amebainisha kuwa katika fedha hiyo, kuunganisha umeme ilitumika Sh. Milioni 12.2, fedha za ujenzi Sh. Milioni 177.5, Samani na vifaa vya kufundishia Sh. Milioni 70.1 na ramani na ulinzi Sh. 380,000 na Sh. Milioni 21.6 zimebaki kwa ajiri ya kuendeshea mafunzo.

Bujuro ametaja majengo yaliyojengwa kuwa ni pamoja na jengo la utawala, karakana ya uashi, vyoo vya watu wenye ulemavu wa viungo matundu mawili na jengo moja lenye vyumba vinne kwa ajiri ya karakana za uchomeleaji na uungaji vyuma, uhazili, ushonaji na chumba cha darasa.

Ameongeza kwamba, chuo hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 80 kwa mwaka, kila darasa wanafunzi 20 kwa masomo ya muda mrefu yaani miaka 2 na wanafunzi 300 kwa kozi za muda mfupi na chuo kitaanza kutoa mafunzo Januari mwakani.

Madhumuni ya awali ya ujenzi huo yalikuwa ni kujengaa sekondari, kwa hiyo kwa nguvu ya wananchi vilijengwa vyumba vinne mpaka usawa wa linta, ambavyo thamani yake ni Sh. Milioni 28, lakini kutokana na kuwepo kwa sekondari nyingine Kata ya Kamachumu, waliamua kubadili mawazo kutoka kuwa ujenzi wa sekondari kwenda chuo cha ufundi stadi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Generali Marco Gaguti, amewataka wananchi kuwa wasimamizi wa miradi mbalimbali inayojengwa katika maeneo yao ili kuhakikisha kila senti inayotolewa inatumika kama ilivyopangwa, kwani fedha za miradi hiyo zinatokana na kodi za wananchi ambazo ni fedha za umma.

No comments:

Post a Comment

Pages