November 27, 2019

TASAF yaing'arisha Longido kielimu

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Juma Mhina.

Na Irene Mark

"TUMEPIGA hatua kubwa kitaaluma ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita, kiwilaya, kimkoa na hata kitaifa tunaongoa... Kwa taarifa yenu mshindi wa insha ya SADC anetoka kwetu na mshindi wa insha ya Afrika Mashariki pia ametoka hapa Longido."

Hizo ni kauli za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Juma Mhina, aliyekuwa akizungumzia Maendeleo ya elimu kwenye wilaya hiyo na mchango wa Mfuko wa Maedeleo ya Jamii (TASAF).

Mhina anasema maendeleo ya elimu na mafanikio ya sekta hiyo yametokana na mfumo bora waliojiwekea watendaji na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wananchi wenyewe.

Anasema mwaka 2016 shule ya mwisho kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba iliyoka wilayani Longido hivyo ni wilaya iliyofanya vibaya kitaifa kwa shule za sekondari.

"Aibu hiyo ilikuwa mwingi kwetu tukaamua kupambana na kipekee TASAF wametushika mkono parefu sana leo hii matokeo bora tunayaona.

"...Kwenye matokeo ya darasa mwaka wa 2019 sisi Longido kwa maana ya ufaulu tuongoza ki mkoa na kitaifa tumeingia kwenye shule 10 bora za msingi za Serikali.

"Shule ya kwanza na ya pili mkoa zimetoka Wilaya ya Longido, haya ni matokeo chanya kwa miaka mitatu hatua hii ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na wenzetu TASAF kwenye elimu, miundombinu, afya na uchumi wa kaya moja moja," anatamba Mhina ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Mkurugenzi huyo anasema TASAF ilipeleka Sh. Bilioni 1.6 zilizotumika kwenye miradi ya ajira ikiwemo shule ya msingi ya mfano iliyogharimu Sh. Milioni 290.

Kwa mujibu wa Mhina, shule hiyo itakayoanza Januari mwaka 2020 itawasaidia watoto zaidi ya 150 kutoka vijiji vya Ilchang'it Sapukin na Alaililai vyenye wafugaji zaidi ambao kwao elimu sio jambo muhimu.

"Naamini hii ni shule ya mfano wa shule bora vijijini hapa Arusha na kwenye mikoa mingine, itasisimua zaidi sekta ya elimu kwa maana ya kuongeza idadi ya wanafunzi na ubora kwenye ufaulu," anasisitiza.

Kuhusu ujenzi wa shule hiyo ya mfano iliyopo kwenye Kata ya Gelai Lumbwa, Mhina anasema ndoto za  watoto wa kijiji na kata hiyo kupata elimu bora karibu  na makazi yao zimetimia huku akibainisha kwamba kuna madarasa sita, matundu 15 ya vyoo, uzio wa kisasa na nyumba mbili za walimu zinazobeba familia nne.

"Hii shule itawapunguzia mwendo wanafunzi maana iliwalazimu kutembea mpaka kilometa 18 hadi 20 kwenda shule na kurudi nyumbani Na mkumbuke kuwa watoto hawa wanakuwa kwenye hatari ya kuvamiwa na wanyama wa porini nimewaambia awali hii wilaya imezungukwa na hifadhi za wanyama kwa hiyo kupishan na tembo, chui ni kawaida.

"...Unajua TASAF licha ya ujenzi wa shule hii ya kisasa pia imemjenga Mzazi wa huyu mwanafunzi kuondoa changamoto ya sare na chakula pia inampa mzazi uhakika wa matibabu mtoto akiugua.

"Mzazi huyu anaingizwa kwenye vikundi vya ujasiriamali na ajira za muda hivyo sida ndogondogo hakuna hapo mtoto atasoma kwa amani na atafau vizuri," alisisitiza Mhina.

Wilaya ya Longido ina ukubwa wa mita za mraba 7782 na wakazi 140,000 kwenye vijiji 49.

No comments:

Post a Comment

Pages