HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 29, 2019

Serikali yaombwa iache kuwatisha watetezi wa haki za binadamu

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Hebron Mwakagenda (katikati) akitoa tamko kwa waandishi wa habari,  la mkutano wa azaki kuhusu kupanua nafasi za kiraia.


Na Janeth Jovin

ASASI za kiraia zaidi ya 40 imeiomba Serikali iache kuwatisha watetezi wa haki za binadamu badala yake iwalinde na kuwasaidia ili waweze kufanya kazi zao kwa amani na salama pia ilinde hazi za kijamii ba kisiasa.

Hayo yamebainishwa jijini Jana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Hebron Mwakagenda wakati akitoa tamko kwa waandishi wa habari,  la mkutano wa azaki kuhusu kupanua nafasi za kiraia.

Alisema watetezi wa haki za binadamu nchini wanaokabiliwa na changamoto nyingi wakati wa kutekeleza majukumu yao hivyo wanaomba serikali iache kuwatisha watu hao na ihakikishe inalinda haki za kijamii na kisiasa.

"Tumeshuhudia mara kadhaa kukamatwa na kushtakiwa kwa watetezi wa haki za binadamu, unyanyasaji wa waandishi wa habari na kuwekwa vizuizi vingi juu ya uendeshaji wa  Asasi za Kiraia (AZAKI).

Kwa kuongezea, Asasi za Kiraia zimezuiliwa kwa kiasi kikubwa kushiriki katika michakato ya uchaguzi wa ndani licha ya kuomba kuruhusiwa kufanya hivyo," alisema Mwakagenda.

Alisema vitendo hivyo havikubaliki kwa kuzingatia ahadi zilizotolewa na Serikali kuheshimu na kulinda haki za raia ambazo zimewekwa katika katiba na mikataba ya kimataifa ambayo nchi imeridhia.

Aidha alisema Serikali pia inapaswa kuondoa vizuizi vilivyowekwa na sheria juu ya utendaji kazi wa asasi za kiraia na kuanzisha mifumo inayowezesha zaidi.

"Asasi za Kiraia, Watetezi wa Haki za Binadamu, Taasisi za Dini, Wanaharakati na Vyombo vya Habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar tulikutana katika warsha iliyofanyika jijini Arusha kwa lengo la kujadili  'Nafasi za kiraia na jukumu la Asasi za Kiraia Katika Kuchagiza Maendeleo ya Nchi yetu'.

Katika mkutano huo Washiriki wote walitambua uhusiano mkubwa uliopo kati ya nafasi za kiraia (Civic Space) na maendeleo endelevu na yenye usawa na hivyo kutambua jukumu walilonalo la kuchangia kupanua na kukuza nafasi za kiraia ili kuleta maendeleo ya nchi," alisema.

Alisema warsha hiyo ilikua na malengo ya kuweka fursa ya asasi za Kiraia kutathmini kwa pamoja mwenendo wa nafasi za asasi hizo nchini na mahali pengine kujifunza na kubadilishana uzoefu.

"Pia tulikuwa na lengo la kuandaa mfumo mzuri kuhusu mambo ambayo Asasi za Kiraia zinaweza kufanya peke yake  au kwa pamoja ili kutatua changamoto  na kupanua nafasi za kiraia  ili kuleta maendeleo ya nchi," alisema.

Alisema katika warsha hiyo, waliona kuwa nafasi za kiraia zinapungua haraka sana hali ambayo inaleta wasiwasi kwa maendeleo ya nchi, uanzishwaji wa sheria na maagizo ya makatazo pamoja na vitisho vya baadhi ya viongozi wa Serikali juu ya watetezi wa haki za binadamu.

Naye Wakili na Ofisa Utetezi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Leopold Mosha alisema wanaiomba Serikali kubadilisha sheria za mitandao ambazo kwa kiasi kikubwa zinawakandamiza watetezi wa haki za binadamu.

No comments:

Post a Comment

Pages