Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum Arusha, Joyce Mukya, Bungeni jijini
Dodoma, Novemba 13, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema zoezi la usambazaji wa huduma ya nishati
ya umeme linaloendelea kufanyika nchini hususan kwenye maeneo ya vijiji
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni endelevu.
”Mheshimiwa
Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya
Mtanzania inawaka umeme ifikapo 2021. Kazi hiyo inaendelea vizuri kwa
usimamizi wa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.”
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 14, 2019) katika kipindi cha
maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la
Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza.
Mbunge
huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu vijiji ambavyo bado
vitakuwa havijaunganishiwa umeme hadi 2021 ambao ni muda wa ukomo wa
miradi ya REA.
Waziri
Mkuu amesema hakuna kijiji kitakachokosa kuunganishiwa huduma hiyo na
ili kuhakikisha inawafikia wananchi wote gharama za kuunganisha umeme
vijijini zimepunguzwa na sasa ni sh 27,000 tu.
Amesema
mbali na kupunguzwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme, pia Serikali
imefuta gharama za bidhaa nyingine za kupeleka umeme kwenye maeneo yao
ikiwemo nguzo na nyaya.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira kwenye
sekta za afya, elimu na kilimo na hivi sasa inatarajia kutoa vibali 16,
000 vya ajira za walimu na kisha itatoa vya watumishi wa afya.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo,
Rashid Shangazi, ambaye alihoji, nini mkakati wa Serikali wa
kuhakikisha wanapatikana watumishi wa kutosha kuwahudumia Watanzania.
Amesema
mkakati wa kujenga miundombinu ya kutolea huduma mbalimbali nchini
unakwenda sambamba na kuajiri wataalamu watakao wahudumia wananchi
katika maeneo husika.
”Serikali
imeanza kutoa vibali vya ajira katika sekta hizi mbili za afya na
elimu, hata kwenye kilimo. Mwaka jana tuliajiri watumishi 6,000 na sasa
tuna kibari ambacho kitatoka hivi karibuni cha watumishi 16,000 kwa
upande wa sekondari na msingi.”
No comments:
Post a Comment