…Lukuvi atoa miezi minne
Waziri Ardhi, Nyumba na Meandeleo ya Makazi, Willim Lukuvi. |
Na Suleiman Msuya
SERIKALI imetoa miezi minne kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kufanya uhakiki mpya wa majengo ya Msajili wa Hazina yaliyokuwa yametaifishwa na kupewa wananchi kwa mikataba ila yameuzwa kinyume na taratibu.
Aidha, Serikali imesema watu wote ambao wamepangishiwa nyumba kwa gharama ambazo hazitambuliki NHC (kilemba) wapeleke taarifa ofisini kwake ili warejeshewe fedha zao.
Miezi hiyo imetolewa na Waziri Ardhi, Nyumba na Meandeleo ya Makazi, Willim Lukuvi, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya NHC baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua miradi na nyumba za shirika hilo jijini hapa.
Waziri Lukuvi alisema baada ya ziara hiyo ambayo ilishirikisha wajumbe wa Bodi ya NHC wamebaini kuwepo nyumba za shirika hilo kuuziwa watu ambapo hawakuingia mkataba na Msajili wa Hazina jambo ambalo sio sawa.
Alisema katika ziara hiyo wamebaini Nyumba Namba 43 iliyopo Lusimo Kinondoni kuuzwa kwa raia mmoja wa Ghana huku kumbukumbu zikionesha nyumba hiyo ilikuwa inamilikiwa na raia wa asili ya Asia.
Lukuvi alisema utaratibu uliotumika baada ya nyumba hizo kutaifishwa, Serikali ilizirejesha kwa mikataba ambayo ilitaka waishi hadi watakapo kufa na nyumba kurejeshwa Serikali.
Alisema kuna wajanja wachache wameingia katikati na kuuza nyumba za Msajili wa Hazina kinyume na taratibu. “Nataka mfanye uhakiki mpya kulingana na Tangazo la Serikali (GN), iliyokuwepo awali nyumba zote zirejee kwa Msajili wa Hazina,” alisema.
"Natoa miezi minne kuanzia sasa NHC mshirikiane na ofisi ya Msajili wa Hazina mpitie nyumba zote mziangalie na watu waliorudishiwa kwa huruma na mikataba yao kwani wapo wajanja ambao wameingia katikati na kulaghai,” alisema.
Alisema iwapo uhakiki utabaini kuwa wahusika wanaomiliki sio wale ambao waliingia mkataba na ofisi ya Msajili wa Hazina zirejeshwe haraka na hatua nyingine zifuate.
Waziri Lukuvi alisema uhakiki huo wa nyumba za Sertikali utafanikiwa kuondoa wamiliki hewa ambao wanamiliki nyumba kinyume na taratibu kwa kubadilisha hati za nyumba hizo.
"Wanamiliki hewa wa nyumba za shirika wajiandae kuondoka hatuwezi kuruhusu utaratibu wa watu kuuziana nyumba zetu.Kimsingi wamekalia bomu," alisitiza Lukuvi.
Alisema wote ambao wamehusika wajue wanafuatiliwa ili ukweli ujulikane na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.
Waziri Lukuvi alisema wapo ambao wanadai kuwa walipata nyumba hizo kwa kuandika kuwa nyumba hizo walizipata kwa huruma ya Rais sio kweli kwa kuwa Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba iliweka bayana kuwa ni kinyume na sheria.
Kuhusu NHC kukosa kanzi data ya wapangaji wake Waziri Lukuvi aliitaka shirika hilo kuhakikisha mchakato wa kupata kanzi data hiyo unakamilika hadi mwezi Machi mwakani.
Alisema taarifa alizonazo ni kuwa wapangaji wengi wanalipishwa gharama kubwa na vishoka huku shirika likiwa halinufaiki na chochote.
Lukuvi alisema serikali haiwezi kuruhusu watu kupanga bei za kupangisha watu huku shirika likiendelea kukosa fedha.
“Nataka mpitie uhakiki mpya wa majengo yenu na ya Msajili wa Hazina mnayoyapangisha na mikataba ya wapangaji, najua kuna baadhi ya wapangaji wameanzisha vishirika ndani ya shirika watu wana nyumba mbili tatu nao wanapangisha.
Lakini wapo ambao wakihama nyumba wanauza nyumba kwa bei kubwa hadi shilingi milioni 10, 20 na kuendelea kinyume na utaratibu. Nataka kila mpangaji taarifa zake ziwepo katika mfumo wa kidigitali na muingie kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),” alisema.
Waziri Lukuvi alisema anataka kila mpangaji anayeingia kwenye nyumba za shirika ajulikane anafanya nini, mwajiri wake ni nani na anuani zake zote kwani wapo ambao wanapangisha nyumba huku wao wakiwa hapo katika nyumba hizo.
"Natangaza kuanzia leo (jana) iwapo kuna mpangaji ametozwa fedha nyingi kinyume na utaratibu wa shirika iwe Sh.Milioni 100, 80, 60 au 20 aje na ushahidi atarejeshewa fedha zake," alisema.
Waziri Lukuvi alitumia nafasi hiyo kuagiza shirika kuacha utaratibu wa kutoza kodi ya miezi sita au mwaka iwapo mteja hana na kwamba utaratibu unataka mpangaji kulipa kila mwezi.
Alisema utaratibu huo unapaswa kufuatwa na wamiliki wa nyumba wengine kwani ndivyo sheria zinataka huku akisisitiza kuwa katika kukabiliana na changamoto hivyo Serikali ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mamlaka ya kusimamia wapangaji.
Aidha Waziri Lukuvi aliagiza Bodi na Menejimenti ya NHC kupitia mikataba ya miradi 192 ambayo wanashirikiana na sekta binafsi ili kuangalia namna ya kuachana nao.
Waziri Lukuvi alisema mikataba hiyo ambayo shirika inapata asilimia 25 haina tija kwa shirika na taifa bali inawanufaisha wabia ambao wanapata asilimia 75.
"Naagiza Bodi na Menejimenti ya NHC ipitie upya mikataba ya miradi 192 ambayo mnashirikiana na wabia binafsi naona haina faida kwa shirika hili lifanyike mapema nipate taarifa," alisema.
Alisema changamoto ya ushirikiano wa NHC na wabia inasababisha shirika kukosa ushiriki wa karibu katika kusimamia miradi husika.
Lukuvi alisema uthubutu wa Bodi kusimamisha miradi 45 kati ya 192 unapaswa kuendelezwa ili shirika liweze kunufaika moja kwa moja.
Pia Waziri Lukuvi ameagiza miradi yote ambayo inatekelezwa na NHC ijengwe na Kampuni ya Ujenzi ya Shirika kwa kuwa imeonesha mafanikio mazuri.
Alisema mafanikio ya Kampuni hiyo ua Ujenzi yamefanikiwa kulipatia shirika miradi zaidi ya 32 hadi sasa hivyo kuitaka kampuni iongeze nguvu zaidi na ubora wa kazi.
"Pia natumia nafasi hii kuagiza shirika lianze ujenzi wa nyumba katika eneo la Chamwino Dodoma ambazo zitaweza kuishi kaya zaidi ya 100 kwani itawaongea sifa.
Alisema hataki kusikia shirika likiajiri mkandarasi kutoka nje ya shirika kwa kuwa wanao wataalam wa kutosha na wenye uwezo.
Waziri Lukuvi alisema atafanya ziara ya kukagua mradi huo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu hivyo hatahitaji propaganda katika suala hilo.
Halikadhalika Waziri Lukuvi ameitaka NHC kuhakikisha inalipa deni la kodi ya ardhi linalofikia Sh.Milioni 400 ifikapo mwishoni mwa Januari 2020 kwani ni aibu kwa shirika kudaiwa.
Alisema mchakato huo wa kulipa deni hilo la Sh. Milioni 400 liendane na kusisitiza watu wote ambao wamejenga katika viwanja vya shirika hilo kulipa kodi kwa wakati na kupatia hati za umiliki.
Aidha, Waziri Lukuvi aliitaka menejimenti ya NHC kufanyia marekebisho majengo waliyouza katika eneo la Mwongozo wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Alisema juzi alipotembelea nyumba hizo za Mwongozo amepokea malalamiko hivyo anataka maboresho yafanyike haraka.
“Kule Mwongozo hamjajenga vizuri kusema kweli juzi nimetembelea kule nimesikia lakini nimeona mwenyewe mifumo ya maji, umeme na mingine haipo vizuri naomba muende mrekebishe.
Aidha, Waziri huyo amepiga marufuku kwa shirika hilo kukopa fedha za ujenzi wa miradi kwenye mabenki ya kibiashara na kulitaka litumie fedha zake.
Lukuvi alisema Mradi wa Morocco, Kawe na mingine ikamilike kwa fedha za ndani na hataki kusikia watu wanaenda kukopa fedha kwenye mabenki ya kibiashara kwani fedha wanazo.
Alisema Bodi na menejimenti mpya ya NHC imeonesha ubunifu mkubwa hivyo ameitaka iendelee na kasi hiyo.
No comments:
Post a Comment