December 05, 2019

MOI YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA MADAKTARI BINGWA

Waziri   wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia), akiwa na Rais wa  Taasisi ya Masuala ya Uchumi na  Maendeleo ya Afrika nchini Japan (AFRECO), Tetsuro Yano.

Na Asha Mwakyonde

WAZIRI  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), ina upungufu wa
madaktari bingwa wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (Neurosurgeons), pamoja na wa usingizi.

 Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam leo wakati wa ziara yake na Rais wa Taasisi ya Masuala ya Uchumi na  Maendeleo ya Afrika nchini Japan (AFRECO), Tetsuro Yano, Waziri Ummy alisema  rais huyo alikuja nchini kwa ajili ya  kufuatilia uhusiano kati ya Japan na Tanzania katika sekta ya afya.

Alisema kuwa taasisi ya MOI ina madaktari bingwa wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu  saba  na kwamba wanaohitajika ni 13 na wausingizi waliopo ni watano huku wanaohitajika ni 15  na nchi nzima hawafiki 30.

" Nimeomba kupitia kwao kutufundishia madaktari hawa pia tumeomba kushirikiana nao katika ujenzi wa miundombinu ikiwamo vyumba vya upasuaji. Hapa MOI tunahitaji vyumba  13 lakini vilivyopo ni tisa tu," alisema.

Waziri Ummy alisema kuwa rais Yano walikuwa Dodoma na watasaidia Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), kuanzisha kituo cha matibabu  pamoja na kuanzisha kiwanda cha kutengeneza maji maji ya dawa.

" Nineona nije nao hapa MOI ili kuweza kuwasilisha maombi yetu ya kwao kwa ajili ya kuboresha matibabu ya kibingwa ya Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahami,",alisema  Waziri  Ummy.

Aliongeza kuwa alimleta katika taasisi hiyo rais huyo ili kuwaomba awajengee kituo cha huduma za utengemao kwani mtu anaweza kupata ajali na akafanyiwa upasuaji  na kwamba viungo vyake vikawa havijarudi katika hali yake ya kawaida.

"Wenzetu wa Japan wameendelea katika masuala ya teknolojia, miundombinu  na ujuzi. Nimeona tushirikiane nao katika masuala haya," alisema

Alisema  maombi hayo yamekubali  na kwamba Tanzania na Japan rasmi kushirikiana  hususani katika kujenga uwezo wa huduma za kibingwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ya MOI , Dk. Respicious Boniface, aliishukuru serikali ya awamu ya tano kuwekeza katika sekta ya afya.

No comments:

Post a Comment

Pages