HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 09, 2020

WAZIRI MKUU AFUTA MNADA WA NAFAKA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefuta mnada wa nafaka ulioendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Januari 7, 2020 na kuuagiza uongozi wa mamlaka hiyo kutangaza upya zabuni baada ya kutoridhishwa na taratibu zilifanyika awali.

Mnada huo ambao unahusisha mahindi tani 5,000 na ngano tani 460.12 unafanyika baada ya wahusika kushindwa kutimiza masharti ya kiforodha, hivyo Serikali imeamua kuuza ili kufidia gharama zake. Nafaka hizo ziliingia nchini Machi 2017.

Waziri Mkuu amesitisha mnada huo leo (Alhamisi, Januari  9, 2020) wakati akizungumza na Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA, Bw. Ben Asubisye, ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu ameagiza kutangazwa upya kwa mnada mwingine wa kuuza mahindi hayo sambamba na ngano na wahakikishe masuala yote kuhusu mnada huo yanakamilika ndani ya siku tatu kuanzia leo tarehe 09 Januari 2020.

“Mahindi yameuzwa kwa bei ya sh. 340 kwa kilo moja ambayo ni chini na bei ya soko kwa sababu bei ya mahindi sokoni kwa sasa ni sh. 800. Zabuni imetangazwa kwa muda mfupi watu wameshindwa kushiriki. Ilifunguliwa saa 8 mchana na imefungwa saa 5 usiku.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa TRA uhakikishe mnada unaofuata unakuwa wa wazi, huru pamoja na kutoa muda wa kutosha kwa wananchi wote kushiriki ili kuondoa malalamiko. 

“Kwa kuwa mnada unafanyika kwa njia ya mtandao, hakikisheni matumizi ya mtandao yanakuwa rafiki kwa wananchi wote watakaovutiwa kuwasilisha zabuni zao.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa TRA ishirikiane na mamlaka nyingine za Serikali kuhakikisha wanunuzi wa nafaka hizo hawaziingizi sokoni kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Nafaka hizo zimepimwa na kuthibitika kuwa zinafaa kwa matumizi ya wanyama.

No comments:

Post a Comment

Pages