Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyetangulia mbele
katikati) akipata maelezo kuhusu ukarabati wa vichwa vya treni kutoka kwa
Kelvin Kimario (wa kwanza kulia mbele), Meneja Msaidizi wa Karakana ya Reli,
Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana hiyo.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) akipata
maelezo kutoka kwa Mhandisi Albert Magandi, Mkurugenzi wa Uhandisi Mitambo
kuhusu utendaji kazi wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye
Karakana hiyo
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akipata
maelezo kuhusu utengenezaji wa vichwa vipya vya treni kutoka kwa Mhandisi
Wenceslaus Kamugisha, Meneja wa Mradi wa Kampuni ya SMH RAIL ya Malaysia wakati
wa ziara yake kwenye Karakana ya Reli, Morogoro
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa
viongozi wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana
hiyo
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia) akipata
maelezo kuhusu ukarabati wa vichwa vya treni kutoka kwa Mhandisi Edgar Bakuza,
Meneja wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana hiyo
Mafundi wa Karakana ya
Reli, Morogoro wakiendelea kukarabati vipuri vya vichwa vya treni wakati wa
ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye
(hayupo pichani) kwenye Karakana hiyo.
Na
Mwandishi Wetu, Morogoro
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amelielekeza Shirika la
Reli Tanzania (TRC) kununua vipuri kwa ajili ya kufanya matengenezo na
ukarabati wa vichwa vya treni kwa wakati
Nditiye ameyasema hayo
wakati wa ziara yake jana kwenye Karakana ya Reli Morogoro ambapo alikagua
matengenezo na ukarabati wa vichwa vya treni yanayoendelea kufanyika kwenye
karakana hiyo mkoani Morogoro
Pia, ameshuhudia utengenezaji
wa vichwa vipya saba vya treni unaofanywa na Kampuni ya SMH Rail ya kutoka
nchini Malaysia kwa kushirikiana na mafundi na wataalamu watanzania wa karakana
hiyo
Wakati akiwa ziarani
hapo alifanya kikao na viongozi na mafundi wa Karakana hiyo na kubaini kuwa TRC
inachukua muda mrefu kufanya manunuzi ya vipuri au oil kwa ajili ya kukamilisha
ukarabati au matengenezo ya vichwa vya treni ambapo manunuzi yanachukua muda
mrefu
“wataalamu wa manunuzi
wa TRC muache tabia ya kuchukua muda mrefu kufanya manunuzi ya vipuri au oil
kwa ajili ya kufanya matengenezzo au ukarabati wa vichwa vya treni, kama kuna
changamoto kwenye manunuzi au malipo, menejimenti ya TRC fanyieni kazi jambo
hili,” alisisitiza Nditiye
Aliongeza kuwa
hatuhitaji tutafute vipuri izidi miezi mitatu na fundi anaomba oil ili afanye
matengenezo ya kichwa cha treni inachukua miezi miwili kwa kuwa sisi Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tumeona umuhimu wa reli, tutalinda reli yetu na
tutaendelea kurekebisha njia ili reli iendelee kuchagiza uchumi na kuongeza
pato la taifa letu kwa kuwa bila reli kichwa cha treni hakisogei na bila reli
uchumi haupandi
Tunashukuru kwenye
karakana hii tuna mafundi na wataalamu wa kutosha ambao wako tayari kufanya
kazi kwa bidii na kujitolea ili kuhakikisha kuwa treni zetu zinatembea na reli
yetu inafanya kazi na wako tayari kufundisha vijana ili waweze kuwaridhisha
utaalamu huo
Naye Meneja wa
Matengenezo ya Vichwa vya Treni, Karakana ya Reli ya Morogoro, Mhandisi Edgar
Bakuza amekiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa vipuri kwa wakati kwa
ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati wa vichwa vya treni kwenye Karakana
hiyo
“Ni kweli changamoto
za vipuri ni kubwa, tunajitahidi kupambana nayo ndiyo maana tupo hapa kwa ajili
ya kuzikabili changamoto ambazo zinatukabili na natumai kutokana na
mashirikiano mazuri ambayo tunayo kati yetu sisi na viongozi wetu wa juu changamoto
hizo zinafanyiwa kazi na natumai mwisho wa siku sisi hapa Morogoro huwa
tunapimwa kutokana na uimara wa kazi tunazozifanya hasa katika hivi vichwa vya
treni, uimara wake pamoja na uwingi wao katika hii fleet yetu ya locomotives
katika hii reli ya kati, kwa hiyo tuko mbioni kuikabili na kuiondoa kabisa,”
amefafanua Mhandisi Bakuza
Mhandisi Bakuza
amesema kuwa wanaendelea na matengenezo ya vichwa saba vya kupangia mabehewa na
mradi unaendelea vizuri na upo katika hatua nzuri ya kuweza kuukamilisha na
sasa kazi ya kuendelea kuunga vyuma na mabati mbali mbali inaendelea ili kuweza
kupokea vifaa mbali mbali ambavyo vimeagizwa nje ya nchi na tayari vifaa vingi
vimefika kwenye Karakana hiyo, vifaa vingine vimeagizwa, vimesafirishwa na
tayari vipo bandarini Dar es Salaam kwa ajili ya kugombolewa na kufikishwa Morogoro
Ameongeza kuwa mradi
huu utakapokamilika utawezesha kuondoa vichwa vikubwa vya treni kutoka katika
kazi ya kupangia mabehewa ili vitumike katika kazi ya kuvuta mzigo mkubwa
kwenda mikoa ya bara
Vichwa
vinavyotengenezwa vitakuwa na kazi ya kuvuta mzigo kutoka Bandari ya Dar es
Salaam ili kuufikisha Bandari ya TRC iliyopo eneo la Kwala mkoani Pwani ili
mabehewa hayo yavutwe na kichwa kikubwa cha treni kuelekea bara
Naye Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu wa TRC, Halima Lumuli alikiri uwepo wa changamoto
hiyo ya upatikanaji wa vipuri ila watajitahidi kuhakikisha vinapatikana kwa
kuwa vichwa vya treni ndio kila kitu katika utendaji wa TRC na Shirika
litajitahidi kuboresha eneo hilo pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi na
kuwapatia mafundi mafunzo ya kuongeza uwezo na weledi ili utendaji kazi wao
uweze kuongeza mapato ya Shirika
No comments:
Post a Comment