NA
GOODLUCK HONGO
WATAALAM
na Makamishna wa Masuala ya Nishati kutoka nchi 12 za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana jijini Dar es Salaam kujadiliana namna na
nchi hizo kupata nishati toshelevu hasa vijijini.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Zena Saidi, wakati akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Alisema
mkutano huo ni sehemu ya mwendelezo wa vikao vya SADC nchini, unahusisha
wataalam, wakurugenzi, makamishna kutoka nchi 12 ya jumuiya hiyo ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa uamuzi uliopitishwa na viongozi wa jumuiya hiyo.
Saidi
alisema wataalam hao watajadiliana kuhusu uanzishaji wa kituo cha umahiri cha
kuendeleza nishati na matumizi bora ya nishati, matumizi ya gesi asili kwa nchi
za SADC.
“Tanzania inatengeza Mradi wa Kuzalisha Umeme
wa Nyerere (NHPP), pindi utakapokamilika tunaweza kuuza umeme wa ziada katika
nchi za SADC. Tunataka bei ya umeme ipungue, matumizi ya mkaa yapungue na uhifadhi wa mazingira uboreshwe,” alisema
Saidi.
Alisema
upatikanaji wa umeme katika nchi za SADC hususani vijijini upo chini ya
asilimia tano, hivyo kuna haja ya kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo
hayo.
Kwa
upande wake Kamishna wa Nishati na Gesi wa Wizara ya Nishati Tanzania, Adam
Zuber alisema wataalam hao pia watajadiliana masuala ya nyuklia, kufanya
mapitio, kujadiliana utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile uanzishaji wa
kituo cha umahiri cha kuendeleza nishati jadidifu na matumizi bora ya nishati
kwa nchi za SADC.
“Kamati
ya Nishati ya SADC, wamekutana ikiwa ni utekelezaji wa maamuzi ya marais, ambapo
nchi wanachama 12 zimehudhuria, na kituo hicho kitaanzishwa baada ya kupata
uhalali wa wanachama 11 kati ya 16 wa jumuiya hiyo, kwa sasa ni nchi nane
ambazo zimeshasaini uannzishwaji wa kituo hicho,” alisema Zuber.
Mkurugenzi
wa Miundombinu wa SADC, Mapolao Makoena alisema mojawapo ya agenda
itakayojadiliwa kwa undani ni mabadiliko ya protokali ya nishati, kwamba
maamuzi yake yatapelekwa kwa mawaziri ambao nao watayawasilisha kwa marais wa
nchi.
No comments:
Post a Comment