HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 19, 2020

KAMPUNI YA ASAS AYATOA MAFUNZO NA KUGAWA VIFAA KINGA DHIDI YA KORONA KWA BODABODA NA BAJAJI

 Afisa wa Usalama Mahali pa Kazi kutoka kampuni ya ASAS, Cosmas Charles, akitoa elimu kwa madereva bajaji juu ya kunawa mikono kujinga na maambukizi ya virus vya corona kwenye kituo cha bajaji cha M.R Hotel kilichoko manispaa ya Iringa.
  Afisa wa Usalama Mahali pa Kazi kutoka kampuni ya ASAS, Cosmas Charles, akitoa elimu kwa madereva bajaji juu ya kunawa mikono kujinga na maambukizi ya virus vya corona kwenye kituo cha bajaji cha M.R Hotel kilichoko manispaa ya Iringa.


Na Denis Mlowe, Iringa

KAMPUNI ya Asas imegawa msaada wa vifaa kinga na mafunzo dhidi ya kujinga na Virusi Vya Corona kwenye vituo vya Bodaboda na Bajaji manispaa ya Iringa.

Msaada huo wa ndoo maalum za kunawihia mikono na sabuni ‘Sanitezer’ zimetolewa kwa madereva bodaboda na bajaji wa vituo vya M.r Hotel, Soko Kuu la Iringa Ipogoro, Mahiwa na kituo cha Flerimo na maeneo mengine yote yanakopaki bodaboda.

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa zoezi la kutoa msaada wa vifaa vya kusafisha mikono vipatavyo 300 kwa madereva bajaji, Afisa wa Usalama Mahali pa Kazi kutoka kampuni ya ASAS, Cosmas Charles amesema kampuni hiyo imeamua kuunga mkono juhudi za serikali kupambana na ugonjwa wa corona ambao umekuwa tishio duniani.

Alisema kuwa kampuni ya Asas mkoa wa Iringa wameitikia maagizo ya serikali kuhusu kuzingatia masuala ya usafi katika maeneo ya kazi kama sehemu ya kupambana na tishio la maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona baada ya kuanzisha utaratibu wa kuwa na vifaa vya kunawia mikono kwenye kila kituo ambapo abiria hulazimika kuosha mikono kabla ya kuhudumiwa.

Alisema kuwa wametoa msaada huo kwa vituo hivyo kutokana na mazingira ambayo wanakumbana nayo madereva bajaji na bodaboda kwani watu wengi wamekuwa wakitumia vyombo hivyo hali ambayo kama kampuni tumetoa vifaa kinga na kutoa mafunzo sahihi kwa ajili ya madereva ambao wamepokea kwa furaha vifaa hivyo na mafunzo hayo.

Aidha aliongeza kuwa jamii inatakiwa kuwa na utamaduni wa kujiweka safi katika mazingira wanayoishi na hali ya hii ya kunawa mikono kwa sabuni inatakiwa kuwa utamaduni ambao unafanyika kila siku kuliko kusubiri changamoto kama hizi za gonjwa la corona.

Cosmas alisema kuwa utamaduni wa kuwa na mazingira safi kwa jamii ni muhimu kwani licha ya magonjwa kama haya yanayosumbua sasa kama corona kuna magonjwa ya mlipuko ambayo ni rafiki na mazingira machafu mfano wa Kipindupindu na kuwataka madereva hao kuwa mabalozi wazuri katika kutoa elimu ya usafi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa madereva Bajaji Iringa (UMBI) Norbert Sunka amesema msaada wa vifaa hivyo umekuja wakati muafaka na kuahidi kuvitumia vyema kwa madereva hao na watakuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa abiria kwani kabla ya kupanda atanawa mikono kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.

“Kwa kweli kampuni ya Asas imekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi mkoani Iringa na kikubwa zaidi sisi kama madereva bajaji na bodaboda wamekuwa mstari wa mbele kutusaidia na kama unavyoona leo wamekuja na msaada mkubwa kabisa wa kutupatia vifaa kinga na mafunzo dhidi ya janga la Corona, niseme tu MUNGU awabariki na waendelee kusaidia maeneo mengine” alisema

Mbaruku Kinyunyu mkazi wa Mfanyabiashara wa soko kuu alisema kuwa msaada wa vifaa kinga dhidi ya virus vya korona umekuja wakati mwafaka sana wakati nchi na dunia kwa ujumla wanaendelea kupambana dhidi ya kuenea kwake.

Hivyo kama mwananchi wa mkoa wa Iringa niwapongeze kampuni ya Asas kwa kupitia mkurugenzi wake, Ahmed Salim Abri kwa kutoa msaada huo kwa madereva bajaji na bodaboda kwani wamekuwa ni sekta isiyo rasmi ambayo inatumika na watu wengi nchini.

Katika hali ambayo hakutarajiwa baadhi ya mama lishe kwenye soko kuu la Iringa na vituo mbalimbali waliomba kampuni ya Asas kuwapatia vifaa kinga na Mafunzo kwani wamekuwa wakisikia tu kutoka kwa watu na kuona wengine wakipatiwa na wao wakiachwa nyuma.

Walisema kwamba vifaa kinga hivyo vitawasaidia wao na wateja wao kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa uwoga kutokana na kukosa vifaa maalum kama ambavyo kampuni ya Asas imewapatia madereva bajaji na bodaboda

No comments:

Post a Comment

Pages