HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2020

Wanawake Tume ya Madini wakumbuka yatima

Mwakilishi wa wanawake kutoka Tume ya Madini, Ofisa Rasilimaliwatu Mwandamizi, Fatuma Chondo (kushoto), akikabidhi vifaa mbalimbali kwa watoto yatima wa Kijiji cha Matumaini kilichopo jijini Dodoma tarehe 06 Machi, 2020.



NA MWANDISHI WETU, DODOMA

WAFANYAKAZI Wanawake wa Tume ya Madini Tanzania, wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa Watoto Yatima wa Kijiji cha Matumaini kilichopo Mtakatifu Gasper jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kutoa msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 3,  Mwakilishi wa Tume hiyo Fatuma Chondo alisema wameamua kutumia siku ya wanawake kuwambuka yatima hao.

Siku ya Wanamake Duniani inaadhimishwa leo duniani kote ambapo kitaifa inafanyika wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Mwakilishi huyo alisema wametoa msaada wa mchele, sukari, unga, sabuni, dawa ya mswaki na miswaki na mafuta ambavyo vitasaidia kwa siku chache.

Chondo alisema wao ni wazazi hivyo wameamua kutoa katika kipato chao kusaidia kundi hilo ambalo linamahitaji mengi.

"Katika kuadhimisha siku ya wanawake tumeamua kutoa kidogo tulichonacho kuwasaidia watoto yatima wa Kituo cha Matumaini, naamini wengine watajitokeza kusaidia," alisema.

Chondo alisema lengo la ziara hiyo sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ni kuonyesha upendo kwa watoto yatima ambao wanahitaji malezi kutoka katika jamii inayowazunguka.

Alisema baada ya kufanya ziara katika kituo husika wamepata picha halisi ya namna watoto wanaoishi katika kituo hicho wanavyohitaji upendo na misaada kutoka katika jamii na kuongeza kuwa wataendelea kuwatembelea mara kwa mara.

"Hii sio mara ya mwisho kutembelea watoto yatima katika kituo cha watoto yatima wa Kijiji cha Matumaini, tutakuwa na ratiba ya kutembelea watoto hawa mara kwa mara," alisema Chondo.

Katika hatua nyingine,  Chondo aliitaka jamii ya watumishi wengine kutoka taasisi nyingine za Serikali na binafsi kuwa na utaratibu wa kutembelea watoto yatima katika Kijiji cha Matumaini.

Msimamizi  wa kituo  hicho  Sister Christina, ametoa shukrani kwa wanawake kutoka Tume ya Madini waliotembelea kituo hicho na kuongeza kuwa wameleta neema kubwa ya upendo kwa watoto hao.

"Mungu awabariki sana wanawake kutoka Tume ya Madini pamoja na watumishi wote wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya kwa kutoa muda wao kututembelea, naamini ninyi ni sehemu ya watumishi wote wa tume, maombi yangu Mungu azidi kuwabariki sana na kuwafanya baraka kwa nchi ya Tanzania, alisema Sister Christina

Akielezea historia ya kuanzishwa kwa kituo hicho Sister Christina alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa mwaka 2008 na Sister Rose lengo likiwa ni kuwasaidia watoto walioathirika na virusi vya UKIMWI na kutelekezwa na jamii ambapo walianza kwa kupokea watoto watatu na kuongeza kuwa mpaka sasa wapo watoto 113.

No comments:

Post a Comment

Pages