Dodoma, Tanzania
Tarehe 6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa
Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mkutano huo
ulijadili janga la mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa
na virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri
wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara,
Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni
Angola, Botswana, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya
Ushelisheli, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.
Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo
kuhusu Usafirishaji wa Bidhaa Muhimu na Huduma Katika Nchi za SADC katika
kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona. Mwongozo huu utatumika katika
kipindi hiki unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na usafirishaji wa
bidhaa ambazo ni za muhimu tu na unazitaka Nchi Wanachama kuzingatia na
kutekeleza sera na miongozo mbalimbali iliyotolewa na inayoendelea kutolewa na
Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Forodha Duniani (WCO), Shirika la
Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na Shirika la Usafiri wa Maji Duniani (IMO).
Kwa
mujibu wa Muongozo huo Malori na magari yatakayoruhusiwa kusafirisha mizigo ni
yale yatakayobeba bidhaa za Vyakula; Vifaa tiba na Dawa, vifaa binafsi vya
kujikinga; Mafuta na makaa ya mawe; Pembejeo za kilimo; vifungashio, vipuri vya
magari na mashine.
Raia
wanaorejea katika nchi zao wanatakiwa kuzingatia sheria za nchi zilizowekwa za
kupimwa na ikiwa atagundulika mgonjwa mwenye Virusi vya Corona, atatakiwa
kutengwa kwa kuwekwa kizuizini kwa muda uliowekwa; Kupunguza idadi ya wasafiri
katika mabasi na vyombo vingine vya usafiri; Kutumia miongozo ya WHO ya usafi
katika vyombo vya usafiri, vituo vya mabasi na maeneo mengine ambayo mabasi
yatasimama; Madereva/waendeshaji kutoa taarifa mbalimbali kuhusu njia za
kupambana na COVID-19 kwa wasafiri katika lugha za wasafiri na; Kujaza fomu
zinazohoji maeneo waliopita wasafiri na kuhakikisha fomu hizo zinawasilishwa
kwa kituo cha maafisa afya.
Vyama vya wasafirishaji vinatakiwa Kushirikiana na maafisa
afya kuandaa na kutekeleza programu ya uhamasishaji kwa wasafirishaji magari na
waajiri wake;Kuwaelekeza madereva wa malori kujaza fomu maalum zinazoonyesha
maeneo ambayo watapita, maeneo watakayosimama wakati wa safari na kituo cha
mwisho cha safari ambazo zitawekwa katika ofisi za maafisa afya zilizopo
mipakani ili kuweza kuwasiliana na kufuatilia madereva kwa uchunguzi;
Wasafirishaji magari wanatakiwa
kushirikiana na Serikali kuangalia jinsi taarifa za gari zinavyoweza kutumika
wakati wa kuifuatilia; Kuhakikisha madereva wanaovuka mipaka wanabeba sabuni na
maji ya kunawa; Kuwaelekeza madereva kutobeba watu wasiohusika katika magari
yao; Kuelekeza madereva wa malori kuzingatia umbali wa mita moja kati yao
wakati wa safari; na; Kugawa vifaa maalum kwa wafanyakazi na waajiriwa ambao
wapo katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi.
Madereva wa malori watalazimika kuweka
bayana kituo cha mwisho cha safari yao na wanaaswa kusimama katika vituo maalum
vilivyopangwa na endapo dereva au wahudumu wa chombo husika wataonesha dalili
za kuugua COVID-19 lori hilo litalazimika kupitia hatua za usafishaji kabla ya
kuruhusiwa kuendelea na safari, watoa huduma wa chombo hicho watengwa katika
eneo maalum (Quarantine) au kupelekwa
kituo cha matibabu kwa gharama zao; Mmiliki wa lori atalazimika kuandaa dereva
na watoa huduma wengine ili kuwezesha bidhaa kufika mahali zilipokusudiwa.
Dereva na wasaidizi wake wakishusha
mzigo watapaswa kukaa watengwa katika eneo maalum ( Quarantine) kwa siku 14 na kutofanya safari nyingine ya nje katika
kipindi hicho na wataalamu wa afya waliopo mpakani mwa nchi husika watalazimika
kuwasiliana kwa kina na wataalamu wa afya wa nchi mwenyeji wa lori husika ili
kupata taarifa zitakazo saidia kuchukua hatua ya kuwatenga katika eneo maalum dereva
na wasaidizi wake wakati wa kushusha au kupakia mzigo.
Vyombo vya usafiri wa majini kutoka
nchi ambazo zipo hatarini zaidi katika maambukizi au zenye wasaidizi au abiria
waliopo kwenye hali hatarishi zaidi ya maambukizi watalazimika kutengwa katika
eneo maalum kwa siku 14 kwa gharama zao kabla ya kuruhusiwa kutoka eneo ambalo
chombo hicho kilitia nanga na chombo kilichobeba abiria na wasaidizi walioathirika
na COVID-19 hakitaruhusiwa kutia nanga.
Ndege zinazofanya safari katika
maeneo mbalimbali zitalazimika kufuata hatua zote za usafishaji kwa kupuliziwa
dawa na hatua zingine za kujikinga ambazo kila ndege iliyobeba abiria walioathirika
au washukiwa wa COVID 19 inapaswa kuzipitia.
SADC ilikubaliana kuwa hakutakuwa na
zuio dhidi ya wasafirishaji wa nje waliosajiliwa la kuingia nchi mwanachama
endapo wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sera za
usalama za nchi husika.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
No comments:
Post a Comment