HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 02, 2020

CWT IKUNGI YAWARUDISHA TENA VIONGOZI WAKE

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Ikungi mkoani Singida jana. kushoto ni Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Aran Jumbe na kulia ni Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Ikungi, Ladislaus Nkuu.
 Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Aran Jumbe akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Winfrida Kunto.
 Mwenyekiti Mpya wa CWT Wilaya ya Ikungi, Ladislaus Nkuu akizungumza.
 Wajumbe wa Mkutano  Mkuu wakishiriki uchaguzi huo.
 Wajumbe wa Mkutano  Mkuu wakishiriki uchaguzi huo.
 Afisa Tabibu, Shija Mhoja akimpima mmoja wa wajumbe kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa uchaguzi wa CWT wilayani hapo.
 Mwenyekiti Mpya wa Kitengo cha Wanawake (KE) Wilaya ya Ikungi, Sara Mnanda, akizungumza baada ya kuchaguliwa.
 Katibu wa CWT Wilaya ya Ikungi, Izdori Darabe (kulia) akigawa barakoa ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona kabla ya kuanza  kwa mkutano huo.
 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Aran Jumbe wakiagana kwa kugusana miguu ikiwa ni njia ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona.
 Katibu wa CWT wilaya ya Ikungi, Izdori Darabe (kushoto) akimpongeza Mwenyekiti Mpya wa CWT wa wilaya hiyo, Ladislaus Nkuu mara baada ya kushinda tena nafasi ya uenyekiti.
 Wajumbe wa Mkutano  Mkuu wakishiriki uchaguzi huo.
Baadhi ya Wajumbe wakimpongeza mwenyekiti mpya.

Na Godwin Myovela, Singida

WAJUMBE wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Ikungi mkoani hapa hatimaye kupitia Mkutano Mkuu wa chama hicho wamefanikiwa kuwarudisha madarakani viongozi wake wa safu ya juu kwa kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia sasa.
Katika mkutano huo uliokuwa na ajenda moja pekee ya uchaguzi, takribani robo tatu ya wajumbe walioshiriki waliridhia pasipo shaka yoyote kumrudisha tena Ladislaus Nkuu kuendelea na nafasi ya Mwenyekiti ngazi ya wilaya.
Nafasi ya Mweka hazina ilikwenda kwa Mwalimu Hashimu Ntandu, huku Mwalimu Sara Mnanda akipewa jukumu la kuongoza kitengo cha Wanawake kwa nafasi ya Mwenyekiti.
Akizungumza kwenye viwanja vya Sekondari  ya Ikungi, mara baada ya kuchaguliwa Nkuu aliwashukuru wajumbe kwa kumuamini kwa mara nyingine huku akiahidi kwa niaba ya viongozi wenzake kuendelea kutetea haki na maslahi ya walimu.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyowajali walimu hususani kwa hatua yake ya kupandisha madaraja ya walimu zaidi ya 900 katika vipindi viwili tofauti yaani (2016/2018-2019) ndani ya Wilaya ya Ikungi.
Awali, akifungua mkutano huo ambao ulizingatia ipasavyo tahadhari zote za namna ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa Corona, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo alipongeza ushirikiano mkubwa uliopo baina ya Serikali na Walimu.
Alisema katika kipindi hiki cha Awamu ya Kwanza cha Utawala wa Rais John Magufuli, Sekta ya Elimu na Walimu chini ya CWT imekuwa mstari wa mbele katika kujitokeza na kujitoa kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo, kama sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali.
"Halmashauri yetu imeendelea kukua kwenye ufaulu kupitia hamasa na kujitoa kwa dhati kwa chama cha walimu na walimu huku miundombinu ya shule ikiendelea kuboreka kupitia hamasa zenu," alisema Mpogolo.
Hata hivyo aliongeza kwamba ni kupitia juhudi hizo hizo za walimu ndizo zilizopelekea kufanikisha ipasavyo kwa shughuli za Mwenge wa Uhuru ndani ya wilaya hiyo.
Mpogolo alisisitiza ni Walimu hao hao, ndio waliokuwa mstari wa mbele kushiriki kipitia CWT kuhakiki madeni ya Walimu sambamba na kuhakikisha haki na maslahi vinatetewa.
" Ninyi Walimu ni miongoni mwa watu mliojitokeza kwa wingi kumuamini na kumchagua Rais Magufuli, na mpaka sasa hajatuangusha sisi sote. Niwasihi endeleeni kueleza mafanikio yote yaliyofanywa na Rais wetu mpendwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao," alisema.
Mpogolo alisema sote ni mashahidi kwamba kwenye Sekta ya Elimu na Walimu, mpaka sasa Serikali imefanikisha uwepo wa vyuo vikuu zaidi ya 48, huku zaidi ya asilimia 95 ya shule zote za msingi zikiwa na madawati.
Alisema kwenye sekta hiyo ya elimu na walimu jumla ya sh.bilioni 23 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya elimu bure huku bilioni 483 zikitolewa kama mikopo ya Elimu ya Juu, ambapo kupitia mkopo huo zaidi ya walimu elfu 23 wamenufaika.
"Walimu twendeni tukahamasishe watu wajiandikishe sambamba na kusaidia kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura," alisema Mpogolo.

No comments:

Post a Comment

Pages