NA TIGANYA VINCENT-Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, ameigiza Halmashauri ya Wilaya ya
Igunga kuhakikisha inakusanya kiasi cha
shilingi milioni 365.2 ambazo inadai wadau mbalimbali katika vipindi tofauti.
Fedha hizo zinatokana na mikopo ya asilimia 10 ya vikundi na ule
ilioutoa kwa Vijana Saccos ambayo hairajeshwa na fedha nyingine ambazo
zilikusanywa na wakala wa kukusanya mapato ya ndani ambayo hayakuwasilishwa
katika Halmashauri na kusababisha hoja za kiukaguzi.
Mwanri alitoa agizo jana wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Igunga la kupitia hoja ya mbalimbali zilizotolewa na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2018/19.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kati ya hizo shilingi milioni 174.9 ni mikopo
ya vikundi vya wanawake, walemavu na vijana ambayo walikopeshwa lakini hadi
bado wanadaiwa.
Alisema fedha nyingine ni kiasi cha milioni 95 ambazo zilitolewa kwa
Vijana Saccos katika mwaka wa fedha wa 2014/15 ambapo kati ya hizo aliyekuwa
Mkuu wa Wilaya wakati huo alitajwa kukopa shilingi milioni 24 na zote bado
hazijareshwa.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa fedha nyingine za Halmashauri ambazo
zilizotokana na makusanyo ya mapato ya ndani ambazo bado ziko mikononi mwa Wakala
ni shilingi milioni 90.2.
Alisema pamoja na Mahakama kutoa hukumu ya kuwataka kulipa fedha hizo ni
kiasi kidogo kimelipwa na Mawakala hao.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji
kuanza kukata mishahara ya walimu Wakuu wote waliokusanya kiasi cha shilingi
milioni 6.1 kinyume na kiwango kilichoidhinishwa na Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema TAMISEMI iliagiza kila mwanafunzi achangie shilingi 1,500/- kwa
ajili ya UMISETA lakini wao walichangisha shilingi 2,000/-
Mwanri alisema wahusika wote ndani ya Mwezi mmoja lazima wahusika wote
watafutwe na warejeshe fedha zote za Halmashauri ya Wilaya Igunga kwa ajili ya
shughuli nyingine za maendeleo.
Naye Mkaguzi kutoka Ofisi ya CAG Juma Erasto alisema katika ukaguzi wa
mwaka wa fedha wa 2018/19 , Igunga imepata Hati inayoridhisha.
No comments:
Post a Comment