HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2020

SERIKALI YALETA SULUHU KATI YA WAFANYAKAZI NA MKANDARASI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (kulia), akizungumza na Mwenyekiti wa wafanyakazi wa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero, Alex Ndagaro, mara baada ya Mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15 Group, kukubali kulipa madai ya wafanyakazi mkoani Morogoro jana. (Picha na Wizara ya Ujenzi).
Baadhi ya Wafanyakazi wa Kampuni ya China Railway 15 Group wakisikilizwa na mmoja wa wataalamu waliokuja kusuluhisha mgogoro uliopo baina yao na kampuni hiyo ambapo tayari wafanyakazi 109 wamekwishalipa fedha zao na wengine 160 wakiendelea kuhakikiwa,
mkoani Morogoro.


Morogoro, Tanzania

Serikali imetatua mgogoro wa wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi ya ujenzi katika Daraja la Mto Kilombero kwenye kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15 Group uliodumu kwa zaidi ya miaka minne na kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mfanyakazi.

Mgogoro huo uliosimamiwa kikamilifu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Arch. Elius Mwakalinga, pamoja na wataalamu kutoka Sekta hiyo kwa muda wa siku tatu.
 
Mwakalinga, ameagiza uongozi wa kampuni hiyo kuwalipa wafanyakazi hao 109 kati ya 269 waliohakikiwa na kuelekeza wafanyakazi 160 waliobaki uhakiki wao ufanyike kwa haraka ili waweze kulipwa stahiki zao.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amezungumza na wafanyakazi hao katika ukumbi wa Halmashauri ya Ifakara, wilayani Kilombero mkoani Morogoro ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa Serikali iko kwa ajili ya wananchi wake daima.
 
"Niwashukuru nyie ni wazalendo maana bila nyinyi tusingepata daraja nguvu yenu katika daraja lile imeonekana na  madai yenu ya muda mrefu ambayo mmekuwa mkisubiri hatimaye yanamalizika", amesema Naibu Waziri huyo.

Ameongeza kuwa zoezi hili linaendelea kwa makundi mbalimbali yalioendelea kujitokeza lakini niwatoe hofu kila mtu atalipwa sawa sawa naanachostahili kwani Mkandarasi amekubali kulipa mpaka mtu wa mwisho.
 
Kwandikwa pia ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Kazi Mkoa, kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha wananchi hawa wanapata
haki zao.
 
Naye Bw. Ramadhani Selemani ambaye ni mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wanadai malipo yao na tayari amekwishalipwa fedha zake ameishukuru Serikali kwa kutatua hili tatizo kwa macho ya pande zote mbili na wanaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu aitunze Serikali hii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyakazi wa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero  Bw.  Alex Ndagaro, ameeleza kuwa mwaka 2013 waligundua kuwa waikuwa wanapunjwa mishahara yao kulinganisha na viwango vya Serikali vilivyowekwa kwa malipo ya siku.
 
"Tunashukuru Serikali kwa jitihada zao zote zakukubali kuwasimamia wananchi wake na kwa kumbana mkandarasi awalipe madai wafanyakazi wake hii ni Serikali tiifu na ya wanyonge hakika tunampongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na timu nzima ya Sekta ya Ujenzi", amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunjo, amesema mpaka sasa wafanyakazi 109 waliolipwa ni wale ambao masaa yao ya kazi yalikuwa chini ya siku 500 na wale walio zidi zaidi ya siku hizo na makundi mengine yaliyojitokeza wataendelea kusikilizwa na mkandarasi yupo hapa na
wataalamu wa sekta ya ujenzi kuhakikisha zoezi hili linasimamiwa na kuratibiwa vyema.

"Mkandarasi tumekubaliana kusikiliza wote na kufatilia takwimu na vielelezo vyote vya makundi mengine yaliyojitokeza ili kufanikisha zoezi hili", amesisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo

No comments:

Post a Comment

Pages