HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 08, 2020

Bil.2.3/- zaboresha elimu maalum msingi, sekondari

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa shule za Msingi na Sekondari jijini Dar es Salaam.
 Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi kifaa saidizi mwanafunzi Godfrey Moris kutoka shule ya sekondari Pugu wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam.
 Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi laptop mwanafunzi Happines Chelangwa kutoka shule ya sekondari Jangwani wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi Agustino Ilomo kutoka Shule ya Sekondari Tabata Kimanga akifurahi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu alipokabidhiwa  laptop wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa wenye mahitaji maalum walioshiriki tukio la uzinduzi wa usambazaji wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu liliofanyika jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya awamu ya tano imetumia Sh.Bilioni 2.3 kununua vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule za msingi 708 na sekondari 45. Fedha hizo zimetumika mwaka 2019/2020.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa vifaa hivyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu  amesema vifaa hivyo vinalenga kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo katika shule za Msingi na Sekondari hapa nchini.

Dkt. Semakafu amesema pamoja na kugawa vifaa hivyo wizara iliendesha mafunzo kwa walimu wa  lugha ya alama wanaofundisha  shule za sekondari ili waweze kutekeleza jukumu la ufundishaji ikiwa ni  pamoja na  kutengeneza Kamusi ya lugha za alama ya kufundishia shule za msingi na sekondari.

"Tunashukuru maono ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa baada ya kuingia madarakani imefungua fursa za  elimu kwa kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinasababisha watoto kufaidika na fursa hizo.  Katika kuhakikisha tunatekeleza hilo Wizara ya Elimu  iliandaa mkakati wa kujibu ombwe hilo ambao ni kuwapatia vifaa wezeshi na vya kielimu watoto wenye mahitaji maalum," amesisitiza Dkt. Semakafu

Dkt. Semakafu amemtaka Mkurugenzi wa Elimu maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia Dkt. Magreth Matonya kuwa na eneo la kipaumbele la kushughulikia  kila mwaka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, na kwamba kwa mwaka wa fedha unaoanza 2020/21 kipaumbele kielekezwe kwa wanafunzi wenye usonji ili kuwezesha upatikanaji wa elimu bila changamoto.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya ametaja baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa kuwa ni mashine kubwa ya kuchapa maandishi ya wasioona, mashine 27 za kurudufisha maandishi ya nukta nundu, mashine 60 za kupima kiwango cha usikivu na vifaa 60 vya kufundishia matamshi kwa wanafunzi wenye changamoto ya matamshi.

Vingine ni miwani 5,167 za kuzuia mionzi ya jua, vioo 2,067 vya kukuzia maandishi kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu, vifani 5,720,  abakasi 9,909, pazo 2,260 za kufundishia stadi za kujimudu na hisabati kwa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji pamoja na vitimwendo kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo.

Naye Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam Maulid Maulid amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu Semakafu  kuwa vifaa hivyo vitafika shuleni kwa wakati na vitatumika ipasavyo badala ya kufungiwa stoo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi Selemani Joseph kutoka shule ya Sekondari Pugu ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa hivyo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kusoma bila changamoto yoyote.

No comments:

Post a Comment

Pages