Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Seif Kulita akizungumza jambo na Meneja wa Huduma za kusafirisha vifurushi EMS, Mbarouk Sasilo.
Na Janeth Jovin
WAFANYABIASHARA wadogo wadogo zaidi ya 65, wamesajiliwa na kutambulika kufanya biashara zao kwa njia ya mtandao kwa ushirikiano wa Shirika la Posta Tanzania (TPC)ambapo maduka mawili kati ya hayo ni ya watanzania waishio Marekani.
Akizungumzia utaratibu huo kwenye Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam(DITF),yanayoendelea Meneja Biashara Mtandaoni wa Shirika la Posta, Amina Salum amesema hiyo ni huduma mpya ambayo imeanzishwa kusaidia wajasiriamali wadogo nchini kufanya biashara za mtandaoni kwa utaratibu mzuri na wa uhakika.
"Tumeanzisha huduma hii kwa wajasiriamali wadogo wanaopenda kufanya biashara mtandaoni tunawasajili na hadi sasa tangu tuanze chini ya mwaka mmoja tumeshasajili wajasiriamali 65 na wawili kati yao wako Marekani wanaendesha biashara kwa mtandao na hii imesaidia kuwaongezea kipato lakini pia kukuza uchumi na sisi kupata faida kwa sababu ndio wasafirishaji wa hizo bidhaa kwenda kwa mteja pindi anunuapo,"amesema Salum.
Aliongeza biashara mtandaoni ina fursa nyingi na kwamba kwa Shirika hilo kuratibu wajasiriamali hao kumeleta uaminifu kwa wauzaji na wanunuaji kwa sababu wana uhakika wanachokiagiza mtandaoni kupitia wajasiriamali waliosajiliwa nao hufika bila kutapeliwa.
Amesema wajasiriamali wengi wanaoenda kufanya biashara kwa mtandao lakini wanakutana na vikwazo kama kutapeliwa au migizo waliyoagiza kuja ikiwa tofauti na ile waliyoiona hivyo kupitia TPC,muuzaji ni lazima aweke bidhaa kama ilivyo na kuelezea ukubwa wake bila kuongopa.
Akizungumzia maduka ya mtandaoni ya watanzania waishio Marekani ambayo wameshafunguliwa, Salum amesema moja linauza vinyago na jingine linauza bidhaa mbalimbali na wateja ni wengi kwa sababu ya uhakika wa bidhaa kutokana na ushirikiano huo ambao TPC wanaratibu.
"Tunashukuru wananchi wameanza kujua huduma hii na hivi karibuni tutaizindua rasmi hivi karibuni,tunawashauri wananchi watembelee tovuti yetu wajue jinsi ya kujisajili kwa maana ni bure,"amesema Salum.
Hata hivyo alishauri wajasiriamali kuhakikisha wanaongeza thamani bidhaa zao kwa sababu zinaonekana duniani kote hivyo ili kumshawishi mteja ni lazima ziwe kwenye vifungashio vyenye ubora na viwe vimehakikiwa na mamlaka mbalimbali nchini.
Akizungumzia huduma ya kusafirisha vifurushi Meneja wa huduma za EMS wa shirika hilo, Mbarouk Sasilo amesema Shirika hilo limeingia ubia na wizara na taasisi mbalimbali za serikali kwa ajili ya kusafirisha sampuli mbalimbali za vipimo.
Amesema katika ubia huo, wanashirikiana na Wizara ya Afya,Jamii,Jinsia,Wazee na watoto kusafirisha sampuli kutoka jijijini na kuzipeleka kwenye vituo vikubwa kwa wakati.
"Hata kipindi cha janga la corona tulisafirisha sampuli za wananchi waliodhaniwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona kutoka vituo vya kutolea sampuli kwenda maabara na tulifanya kwa uaminifu na ufanisi wa hali ya juu,"amesema Sasilo.
No comments:
Post a Comment