July 14, 2020

BOCCO MCHEZAJI BORA VPL

MSHAMBULIAJI wa Simba ya Dar es Salaam, John Bocco amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Juni wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2019/2020, huku Kessy Mziray wa Alliance FC akiibuka kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
 
Bocco alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Atupele Green wa Biashara United na Martin Kiggi wa Alliance FC alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa mwishoni mwa wiki na Kamati ya Tuzo za VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
 
Kwa mwezi Juni, Bocco alikuwa na kiwango bora akiisaidia Simba kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili ikiendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa LigiKuu ya Vodacom, akipachika nyavuni mabao matatu katika michezo minne aliyocheza. Simba iliifunga Mwadui mabao 3-0, ikaizamisha Mbeya City mabao 2-0 ikatoka sare na Ruvu Shooting mabao 1-1 na ikatoka 0-0 na Prisons.
 
Atupele Green aliingia hatua hiyo baada ya kuisaidia Biashara United katika michezo mitatu ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu ‘hat trick’ katika mchezo dhidi ya KMC uliomalizika kwa Biashara United kushinda mabao 4-0, wakati Kiggi aliingia hatua hiyo baada ya kutoa mchango mkubwa kwa Alliance, ikishinda michezo miwili na kutoka sare mmoja, huku Kiggi akifunga mabao mawili.
 
Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Mziray kuwa Kocha Bora wa mwezi Juni akiwashinda Sven Vandenbroeck wa Simba na Luc Eymael wa Yanga alioingia nao fainali.
 
Mziray aliiongoza timu yake katika michezo mitatu ikishinda miwili na kutoka sare mmoja, ikipanda kutoka nafasi ya 18 hadi ya 14. Alliance iliifunga Mbeya City bao 1-0, ikaifunga Coastal Union bao 1-0 na ilitoka sare na Polisi Tanzania bao 1-1, wakati Vandenbroeck aliiongoza Simba kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili ikiendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa  ligi, huku Eymael akiiongoza Yanga kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili ikiendelea kuwa nafasi ya tatu.
 
Wakati huo huo, kikao hicho cha Kamati ya Tuzo kilichagua Kocha Bora wa Mwezi Machi na Mchezaji Bora wa Mwezi Machi mwaka huu, ambao hawakuwa wamepatikana licha ya ligi kuchezwa raundi nne hadi iliposimamishwa katikati ya mwezi huo kutokana na tishio la ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).
 
Kwa mwezi huo Machi Mchezaji Bora alichaguliwa Meddie Kagere wa Simba aliyeiongoza timu yake kushinda michezo mitatu na kupoteza moja ikibaki kileleni mwa msimamo wa ligi,  huku Kagere akifunga mabao matano, ambapo Simba iliifunga Azam FC mabao 3-2, ikaifunga Singida United mabao 8-0 na ikaifunga KMC mabao 2-0 na ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga.
 
Kagere aliingia fainali na Paulo Nonga wa Lipuli aliyefunga mabao matatu na Never Tigere wa Azam aliyetoa mchango mkubwa kwa timu yake ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu.
 
Kwa upande wa kocha aliyechaguliwa ni Hererimana Haruna wa KMC aliyeingia fainali na Vandenbroeck wa Simba na Khalid Adam wa Mwadui.
 
Hererimana aliiongoza timu yake katika michezo mitano ikishinda minne na kupoteza mmoja, ikipaa kutoka nafasi ya 19 hadi ya 15, ambapo KMC iliifunga JKT Tanzania bao 1-0, ikaifunga Mbao FC mabao 2-0, ikaifunga Yanga bao 1-0 na iliifunga Alliance mabao 2-1, huku ikipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba.
 
Vandenbroeck aliingoza Simba katika michezo minne ikishinda mitatu na kupoteza mmoja na kubaki nafasi ya kwanza, huku Khalid Adam akiisaidia Mwadui kushinda michezo mitatu na kupoteza mmoja ikipanda kutoka nafasi ya 16 hadi ya 12.

No comments:

Post a Comment

Pages