Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Makatibu Wakuu wa Hazina wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Hazina na Magavana
wa Benki Kuu za Jumuiya hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Na Farida Ramadhani, Dar es Salaam
Nchi
za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimeshauriwa kuunganisha nguvu zao kupambana na changamoto ya utakatishaji
fedha haramu na ufadhili wa makundi ya kigaidi zinazotishia usalama na kuharibu
uchumi wa nchi hizo .
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mwenyekiti wa Maafisa Wandamizi wa HAZINA wa SADC, Bw. Doto James wakati akifungua
Kikao cha Maafisa Waandamizi (Makatibu Wakuu) wa HAZINA na
Benki Kuu wa nchi wanachama wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
katika kikao hicho, Bw. James ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho
kitakachofanyika kwa siku mbili, alisema kuwa changamoto hiyo imesababisha baadhi ya nchi wanachama kuingia katika
orodha ya nchi zilizo kwenye athari ya kuingia kwenye vikwazo vya kimataifa kwa
kushindwa kutimiza vigezo na masharti ya Kikosi cha Masuala ya Fedha (Financial
Action Task Force), hali iyonaweza kuathiri malengo ya jumuiya ya kuvutia
uwekezaji.
Alisema licha
ya kuwepo kwa changamoto hiyo na nyingine kadhaa za kijamii,
kimazingira na kiuchumi Jumuiya hiyo imeendelea kutekeleza azma
yake ya kufikia malengo ya maendeleo iliyojipangia kupitia Mkakati Elekezi wa
Maendeleo wa SADC hali inayoashiria kuwa Jumuiya hiyo ni imara kutokana na
kuwepo kwa sera nzuri na mifumo mizuri wa kitaasisi ndani ya Jumuiya hiyo.
“Pamoja na
mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana kwa miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi
wanachama zimeendelea kukabiliana na changamoto nyingine katika sekta za uchumi
ikiwemo ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti na hii
changamoto mpya ya ugonjwa wa COVID-19
unaosababishwa na virusi vya corona”, alisema.
Bw.
James alisema katika kikao hicho Makatibu Wakuu hao
watajadili na kutoa mapendekezo ya ajenda mbalimbali za masuala ya fedha na
uwekezaji kwenye nchi za SADC ikiwemo athari
za Kiuchumi na Kijamii zinazotokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19
yatakayowasilishwa kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na
Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu wa SADC utakaofanyika tarehe 15 Julai, 2020
Alisema kuwa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji, pamoja na mambo
mengine, wanajukumu la kusimamia itifaki ya Fedha na Uwekezaji katika Jumuiya
ya SADC kwa lengo la kuhakikisha Sera na Maamuzi ya Baraza la Mawaziri wa SADC
kwenye masuala yanaohusu Fedha na Uwekezaji vinatekelezwa.
“Ili kukabiliana na athari hizo, ni vema nchi wanachama kutumia mifumo ya
kitaasisi katika kutafuta njia mbadala zenye ubunifu ili kuharakisha hatua za
kuimarisha uchumi ndani ya jumuiya yetu, ni matumaini yangu kuwa kikao hiki ni
njia muafaka katika kujadili changamoto za kiuchumi na kutoa mapendekezo ya
kitaalam yatakayowasilishwa katika Mikutano ya Kamati ya Mawaziri wa Fedha na
Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kama ilivyoanishwa katika agenda za mikutano
hiyo”, alisema Bw. James.
Alizitaja ajenda nyingine
watakazo jadili na kutoa mapendekezo kuwa ni kupitia taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano
uliopita wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha
na Uwekezaji uliofanyika Windhoek, Namibia mwezi Julai 2019, kupokea na
kujadili taarifa ya hatua iliyofikiwa ya namna uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo
wa Kikanda wa SADC (SADC Regional Development Fund) na kupokea taarifa ya
utekelezaji wa Mfuko wa Maandalizi ya Miradi ya Maendeleo wa SADC (Project
Preparation Development Facility).
Viongozi hao pia watajadili na
kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa Mfuko Maalum wa Kugharamia
Miradi ya Muundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme (Regional Transmission
Infrastructure Financing Facility - RTIFF)
inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, kupitia taarifa ya maendeleo ya Sekta ya
Fedha ya Magavana wa Benki Kuu nakupitia taarifa ya utekelezaji wa masuala ya
udhibiti wa fedha haramu.
Mkutano wa
Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na
Magavana wa Benki Kuu wa SADC unaondaliwa katika kikao hicho ulipangwa ufanyike
kuanzia tarehe 13 hadi 17 Julai, 2020 lakini kutokana na mlipuko wa COVID-19,
mkutano huu utafanyika kwa njia ya mtandao kama
ilivyoelekezwa katika Mkutano wa dharura
wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2020, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment