July 22, 2020

Olengurumwa aendelea na ziara ya kutembelea wanachama wa THRDC


NA JANETH JOVIN

MRATIBU wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa ameendelea na ziara ya kutembelea wanachama wa mtandao huo kwa lengo la kubaini fursa na changamoto wanazopitia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Jana Julai 21, 2020 Mratibu huo alianza ziara yake kwa kutembelea Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), tawi la Dodoma.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na mtandao huo ilieleza kuwa, LHRC ni kituo ambacho kimekuwa kikijishughulisha na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa jamii, kuwezesha uma kutambua haki zao, kukuza kuimarisha na kulinda haki za Binadamu, kutoa elimu kwa jamii juu michakato ya katiba pamoja na kuhamasisha utawala bora nchini Tanzania.

Taarifa hiyo ilieleza Wakili wa LHRC, Godliver amesema mbali na kutoa msaada wa kisheria na elimu juu ya michakato ya katiba kituo hicho  kinatumia vipindi vya radio kupitia Dodoma FM ili kutoa elimu kwa jamii.

Wakili Godliver ameongeza kuwa kituo hicho kinashirikiana na mashirika mengine wanachama wa mtandao katika maswala mbali mbali yahusuyo utetezi wa  haki za binadamu ikiwa pamoja na uchambuzi wa miswada, pamoja na msaada ya kisheria.

Amesema pamoja na kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na kituo hicho  bado kinakabiliana na changamoto kadha wa kadha ikiwamo ya uchache wa Wateja na uwepo wa mashauri machache ya kuyashughulikia.

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa Olengurumwa ametembelea pia Taasisi ya Dungonet  inayojihusisha na uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Dodoma pamoja na shughuli za utetezi wa haki za watoto,vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wanawake wenye umri mkubwa( wazee).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Olengurumwa amelishauri taasisi hiyo kujenga misingi imara ikiwa ni pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya pesa za wafadhili kwa maendeleo endelevu ya shirika na pia kujaribu kuomba fedha kutoka kwa wafadhili pale wanapoona fursa.

Aidha ilieleza taasisi hiyo kupitia miradi yake imekuwa ikiwasaidia wanawake wenye umri mkubwa ambao wameachiwa majukumu mazito ya kulea wajukuu zao ambao ni yatima au watoto waliotelekezwa na wazazi wao.

"Wanawake wenye umri mkubwa ni kundi ambalo limetengwa na kusahaulika  na jamii lakini ni watu muhimu na waliotupiwa majukumu makubwa ya kulea wajukuu ambao wazazi wao wamefariki( yatima)." Amesema Daniel Msogya Katibu DUNGONET

Hata hivyo Olengurumwa ametembelea pia Taasisi ya CESOPE inayojihusisha na mazingira hasa katika kuangazia athari zatokanazo na uchimbaji wa madini ya Uranium na ikihamasisha jamii kuachana na mpango huo, elimu ya haki za binadamu pamoja na kufanya miradi ya kupambana na umaskini mkoani Dodoma.

Pia amekitembelea Chama cha Wanawake Mawakili Tanzania (TAWLA) 

Taasisi ya TAWLA inafanya kazi ya kutoa msaada wa kisheria, kuendesha mashauri katika mahakama, kutoa uwakilishi wa kisheria kwa wateja.

Taasisi hiyo inafanya kazi na wasaidizi wa kisheria (Paralegals) ambao kwa pamoja wanatoa msaada wa kisheria, Pia TAWLA imekuwa ikitoa huduma kwa njia ya simu (Mobile Clinic).

Njia hiyo ya Simu (Mobile Clinic)  imekuwa ikiwawezesha wananchi kupatiwa msaada na ushauri bila kuwa na haja ya kusafiri umbali mrefu kupatiwa huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages