July 22, 2020

THRDC yaishauri WOWAP kuungana na mashirika yanayojihusisha na maswala ya ukatili, utetezi wa watoto

NA JANETH JOVIN

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, (THRDC) imeishauri Taasisi ya Women Wake Up Wowap iliyopo Dodoma kuungana na mashirika yanayojihusisha na maswala ya ukatili wa kijinsia na utetezi wa watoto ili kuwa na sauti ya pamoja itakayofanikisha agenda za muhimu hasa za kutetea wanawake kufanikiwa.

Hayo yamebainishwa leo na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa wakati alipoitembelea taasisi hiyo inayojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto mkoani Dodoma.

Olengurumwa amesema  Wowap inapaswa  kuungana na mashirika yanajihusisha na maswala ya ukatili wa kijinsia na utetezi wa watoto ili kuwa na sauti ya pamoja itakayowezesha kufikisha agenda zao muhimu kupitia majukwaa ya kitaifa na kimataifa yanayohusu haki za binadamu hasa za mwanamke na watoto.

Pia Olengurumwa ameshauri kuwa na mfumo mmoja wa ukusanyaji taarifa kwa njia ya simu "mobile tracking" ili kuweza kuwa na taarifa za pamoja kikanda juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia hiyo itasaidia kuwa na takwimu za pamoja za taarifa hizo.

Katika taarifa iliyotolewa na THRDC ilieleza kuwa Taasisi hiyo ya Wowap ina kitengo cha msaada wa kisheria ambacho kimekuwa kikifanya kazi za kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi mkoani Dodoma

Ilieleza taasisi hiyo imeendelea kuelimisha jamii juu ya namna ya kuondokana na mila potofu na kandamizi kama  ukatili wa kijinsia, ukeketaji kwa wanawake mimba za utotoni, pamoja na uozeshaji wa watoto wakike walio na umri Mdogo, vitendo hivi viovu bado vipo juu sana katika kanda hii ya kati kutokana na mila na desturi za baadhi ya jamii mkoani Dodoma.

Aidha ilieleza taasisi hiyo imekuwa ikikumbana na changamoto ya kifedha kwani imekuwa ikiwahudumia wahitaji wengi katika kanda ya kati lakini upatikanaji fedha umekuwa kikwazo kuweza kuwafikia wahitaji wote, hasa kwenye maswala ya mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia kama inavyoonyesha katika takwimu za Tanzania Dodoma ni miongoni mwao hiyo yote ni kutokana na hali duni ya maisha.

Wakati huo huo, Olengurumwa ametembelea Taasisi ya Peace Legal Aid and Justice Centre (PLAJC), ambayo inajishughulisha 

na masuala ya haki za binadamu hasa utoaji msaada wa kisheria.

Katika taarifa ya THRDC iliyotolewa leo ilieleza kuwa, PLAJC imekuwa ikihamasisha ushiriki  wanawake na vijana kwenye maswala ya Amani na haki za binadamu katika wilaya mbali mbali za mkoa wa Dodoma.

Ilieleza PLAJC kupitia kitengo cha msaada wa kisheria imeweza kupokea mashauri mbalimbali ya Ndoa, Mirathi, na Ardhi kwa mkoa wa Dodoma.

“Pia taasisi hii imesaidia wahitaji wa msaada wa kisheria wanaotoka mikoa mingine kwa ajili ya kushughulikia mashauri yao mkoani, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri, kuandaa nyaraka za kisheria na uwakilishi mahakamani,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa PLAJC imeweza kuunda klabu 49 za Amani na haki za binadamu mashuleni katika ngazi zote za Elimu kwa kushirikiana na Tume ya haki za binadamu.

“Dhumuni la kuunda club hizo za amani na haki za Binadamu mashuleni ni kuwawezesha watoto kutambua misingi na wajibu wa haki zao katika kujenga, kudumisha, kulinda, na kutunza amani, club izo zimeundwa katika Shule mbali mbali mkoani Dodoma mjini, wilaya za kondoa na chamwino,” ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages