HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 25, 2020

TAMWA: Mkapa amechangia kuhimiza usawa wa jinsia, kuijenga nchi kisiasa

Na Janeth Jovin

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kimesema kuwa itamkumbuka Mwanadiplomasia Mkongwe na Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania. Benjamin Mkapa kwa namna ambavyo aliijenga nchi hii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

TAMWA imesema itamkumbuka mwanahabari huyu mahiri hasa mchango wake katika kujenga na kuhimiza usawa jinsia, kisheria, kisera na katika ngazi za maamuzi.
Mmoja wa waanzilishi wa TAMWA, Eda Sanga amesema anaukumbuka mchango wa Hayati Mkapa katika kusimamia ubora wa habari, usawa wa kijinsia hasa sheria ya makosa ya kujamiiana ya Sospa ya mwaka 1998.

“Huyu ndiye alikuwa waziri wetu wa habari, wakati tunaanzisha TAMWA. Mimi nikiwa na wenzangu tulienda ofisini kwake tukiwa na nakala ya jarida la ‘Sauti ya siti,’ tulimpa ili alione asije tu kuliona mtaani.

Tukaongea naye, ili akubaliane na yale tuliyotaka, kwa sababu wakati huo tulikuwa ni waandishi wa vyombo vya habari vya serikali.

“Huyu baba alisaidia sana kuwaona wanawake katika sura hiyo mpya, sura ya kufanya taifa liwe na usawa wa kijinsia, kwa kuwa sote tunaamini kuwa taifa likiwa na wanaume peke yake, ni sawa na mtu anayekwenda na mguu mmoja,” amesema Mama Sanga na kuongeza

“Mimi binafsi nimefanya naye kazi kwa ukaribu kabisa, nikiwa nafanya kazi RTD, yeye alikuwa anasoma taarifa habari na mimi nikisimamia vipindi vya external services,” amesema Sanga

Amesema wakati wa mkutano wa Beijing ulioangazia masuala ya usawa wa kijinsia Rais alikuwa Hayati Mkapa. Na hata walipomaliza mkutano na ripoti kuandikwa, yeye ndiye aliyepokea ripoti.

“Wakati anaipokea tulimuona ana mtazamo chanya akionyesha kuyakubali masuala tuliyoyazungumza kule likiwamo suala la elimu, afya, ambavyo vinahusu zaidi wanawake,” amesema

Amesema Mkapa alikuwa ni mtu mzuri kwa upande wa haki za wanawake na katika kuendeleza taaluma ya habari akisisitiza habari zizingatie ustaarabu, umoja na utamaduni wetu.

Mwanzilishi mwingine wa TAMWA, Ananilea Nkya amesema, unapozungumzia suala la kijinsia, tunazungumzia sauti za watu wenye ulemavu, wanawake na watoto.

“Wakati wa utawala wa Mkapa (mwaka 1995-2005) aliweka mazingira salama ya kisiasa ambayo makundi maalum yaliweza kupaza sauti zao kwa ambalo linawagusa,” amesema

Amesema kulikuwa na fursa kubwa ya watu kukutana na kujadili, ndiyo maana wanaharakati walianzisha FemAct (Mtandao wa Mashirika ya kijamii yanayotetea haki kwa mtazamo wa jinsia).

“Unapomzungumia Mkapa, cha kwanza aliruhusu sauti za watu wa makundi maalum. NGO zilikuwa ‘active’ na aliruhusu maandamano na kukosolewa kwani alijua hizo ni sauti za wananchi,”amesema
Amesema kwa upande wa habari, alikuwa muumini wa vyombo vya habari kupaza sauti za wananchi.

Mwanzilishi mwingine wa TAMWA, Rose Mwalimu amesema anamkumbuka Hayati Mkapa aliyezaliwa tarehe 12 Novemba 1938 kwa kupambana na kumaliza mauaji ya vikongwe.

“Rais Mkapa tunamkumbuka kwa mengi, alikuwa mstari wa mbele, hasa katika kutetea haki za jinsia, ameongeza idadi ya wanawake katika uongozi, na kumaliza mauaji ya vikongwe,”amesema

Amesema kati ya mambo aliyoyafanya ni kusimamia maadhimio ya mkutano wa Beijing baada ya mwaka 1995.

“Maadhimio hayo yametupa hamasa nyingi TAMWA katika kutetea masuala mbalimbali ya jinsia. Alisaidia kupitisha sheria ya makosa ya kujamiiana 1998, katika miaka ambayo kulikuwa na ubakaji na unyanyasaji ulioshika kasi kubwa pia alitambua na kujua kwa nini TAMWA na wadau wengine wanahimiza haki na usawa wa kijinsia,”amesema Mwalimu

Mama Mwalimu amesema, Sera ya jinsia, imetoa dira, mwongozo na kuweka misingi ya taifa linalosimamia misingi ya jinsia.

Mwasisi mwingine wa TAMWA, Maria Shaba amesema anamkumbuka kwa mengi, lakini hatasahau mkono wake katika kupitisha Sheria ya Makosa ya Kujamiaana mwaka 1998.“Mwaka 1998, lilipopelekwa azimio huko bungeni la kuundwa kwa sheria ya kujamiiana ambapo rais aliweka mkono, kukubali kupitisha sheria hiyo.

Mwanzilishi mwingine wa TAMWA na mwanaharakati wa masuala ya jinsia, Leyla Sheikh amesema:“Tumepoteza champion wa haki jinsia. Tutamkumbuka kwa mengi aliyofanya kuleta haki jinsia, kuondoa unyanyapaa, dhidi ya watu wanaoishi na VVU, kutokomea ukeketaji, mauaji ya vikongwe kwa tuhuma za uchawi, kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za uongozi,” amesema

No comments:

Post a Comment

Pages