HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 25, 2020

Membe: Mkapa ni kiongozi wa dunia, nitamkumbuka kwa ushauri wake katika masuala ya uchaguzi



Na Mwandishi Wetu, Lindi

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania katika serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe amesema kuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa, alikuwa Kiongozi wa dunia, mshauri masuala ya uchaguzi na kinara katika kulisaidia bara la Afrika kutatua migogoro bila kuchoka.

Membe aliyasema hayo jana mkoani Lindi, muda mchache baada ya kuahirisha Kikao cha Chama Cha ACT Wazalendo kilichokuwa kiketi mjini humo sambamba na kukutana na viongozi mbalimbali wa Chama ngazi za kata.

Amesema, Mkapa alikuwa kinara katika kusaidia bara la Afrika kuweza kutatua migogoro bila kichoka hatua ambayo imeacha pigo kubwa.

“Kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya familia na Wana-ACT Wazalendo kutoa salamu za pole zetu za dhati kwa msiba mzito ambao umetukuta. Mzee Mkapa ambaye ni Baba yetu na rais mstaafu alikuwa kiongozi siyo wa Tanzania tu bali alikuwa kiongozi wa dunia, amesuluhisha migogoro mingi, nimepokea salamu kutoka kwa Waziri wa Namibia akitoa salamu zake.

“Tutamkumbuka kwa kuwa kiongozi ambaye alitumia wakati wake mwingi kuisaidia jamii ya Tanzania, alikuwa miongoni mwa marais wazuri wa Tanzania, kifo chake kimetuletea majonzi watu wote,” amesema Membe.

Amesema yeye kama Mwana-diplomasia atamkumbuka, Mzee Mkapa kwa elimu yake, ushauri wake, maagizo yake na mafundisho yake juu ya diplomasia ya kweli, diplomasia ya kisiasa na diplomasia ya uchumi ambayo alikuwa anaisimamia.

“Nchi kama Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, Kenya, Sudani na Congo Mzee Mkapa ameshiriki katika utatuzi wa migogoro mbalimbali tangu aache nafasi yake ya urais mwaka 2005.

“Nina hakika baada ya kifo hiko dunia itamkumbuka kama kiongozi mashuhuri barani Afrika na duniani kwa ujumla kwa kuweza kutatua migogoro mbalimbali iliyokuwa ikiikabili Afrika bila kuchoka kwa muda wote alipotakiwa kufanya hivyo,” amesema Membe.

Aidha, Membe aliongeza kuwa ni pigo kuona kiongozi huyo akiondoka katika wakati ambao Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu Oktoba 28, Mwaka huu.

“Katika kipindi cha Uchaguzi kama hiki ni bahati mbaya kuona tunampoteza mtu ambaye alikuwa anahimili mambo mengi ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ushiriki wake na ushauri katika masula ya uchaguzi.

“Ni bahati mbaya kwamba kwa mwaka huu ambapo uchaguzi utakuwa mkubwa na mkali zaidi tumempoteza mshauri mkuu wa masuala ya uchaguzi ya kitaifa lakini Mwenyezi Mungu atatusaidia, na hakika ataendelea kubaki mioyoni mwetu,” amesema Membe.

Amesema Wanachama na Viongozi wa ACT Wazalendo wamelazimika kuahirisha shughuli zote za chama ili kumpa heshima kiongozi huyo ambapo watalazimika kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na kisha kielekea Masasi mkoani Mtwara kwa ajili ya kushiriki mazishi.

Rais mstaafu Mkapa alifariki dunia Julai 23, mwaka huu hospitalini jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ambapo anatarajiwa kuzikwa mkoani Mtwara wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment

Pages