July 14, 2020

TUME YA UCHAGUZI KUTOKUONGEZA MAJIMBO UCHAGUZI MKUU 2020

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imesema haikusudii na wala hakuna mpango wa kuongeza au kupunguza majimbo ya Uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt Wilson Mahera Charles wakati akijibu swali kutoka kwa Mtangazaji wa Clouds wakati akishiriki kipindi cha Clouds 360 kilichokuwa kinarushwa moja kwa moja na kituo hicho kutoka katika ofisi mpya za Tume zilizopo eneo la Njedengwa nje kidogo ya jiji la Dodoma.

Dkt. Mahera amesema hatua ya hivi karibuni ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ya kufuta baadhi ya Majimbo ya Uchaguzi ililenga kuweka uwiano wa majimbo ya Uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar kutokana na ushirikiano wa Tume hizo mbili wakati wa Uchaguzi hivyo kufanya majimbo ya Uchaguzi Zanzibar kubakia 50 badala ya 54 ya awali.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ameongeza kusema kuwa Tume inafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake Tume inazingatia muda kadiri unavyoelekeza kisheria ikiwa ni pamoja na Ratiba ya Uchaguzi.

Akijibu swali kuhusu Tume kuchelewa kutangaza tarehe ya Uteuzi wa Wagombea Dkt Mahera amesema Tume itatangaza Ratiba yote ya Uchaguzi mara tu baada ya kutolewa kwa Tangazo la Serikali kuhusu kuvuja Bunge ambapo kwa mujibu wa Sheria si chini ya siku 5 na si zaidi ya siku 25 baada ya tangazo hilo.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi ametoa rai kwa wananchi na hususan vijana na Wanawake waliojiandikisha kuwa Wapiga Kura kujitokeza kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali pamoja na kushiriki katika kupiga kura Siku ya Uchaguzi itakapowadia kwani takwimu zinaonesha vijana wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

No comments:

Post a Comment

Pages