HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2020

Paradigm Initiative Afrika yawakutanisha wadau kujadili sheria ya matumizi ya mtandao


Mratibu wa masuala ya kimtandao kutoka Shirika la Paradigm Initiative, Peter Mmbando (aliyesimama) akijadiliana jambo na baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa wakishiriki majadiliano yaliyohusu sheria ya matumizi ya mtandao pamoja na kujadili haki za mtumiaji kuendana na uhitaji wa matumizi ya sasa na baadaye, yaliyofanyika Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa majadiliano yaliyohusu sheria ya matumizi ya mtandao pamoja na kujadili haki za mtumiaji kuendana na uhitaji wa matumizi ya sasa na baadae.


Na Janeth Jovin

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Paradigm Initiative Afrika limewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria na waandishi wa habari kwa lengo la kujadili sheria ya matumizi ya mtandao na haki za mtumiaji kuendana na uhitaji  wa sasa na baadae.

Majadiliano hayo ambayo yamefanyika kwa siku mbili kwa njia ya mtandao  yalihusisha pia wadau kutoka nchi ya Nigeria ambapo kwa pamoja walitoa maoni yao na kuomba kupata uzoefu kutoka Tanzania ambayo tayari imepiga hatua ikiwemo kudhibiti kikamilifu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Pamoja na mambo mengine wadau wamepata nafasi ya kuangalia na kujadili muswada wa Nigeria unaohusu masuala ya matumizi ya mtandao pamoja na kuangalia ni maeneo gani ya kusaidia kuboresha ufanisi, misingi bora ya utumiaji ya mitandao ya kijamii kwa Tanzania na Afrika ya sasa kwa siku za baadae.

Akizungumza kuhusu majadiliano hayo Mdau na mtumiaji wa mtandao, Mratibu wa majadiliano hayo, Peter Mmbando amesema watumiaji wa mtandao ya kijamii wanapaswa kuitumia kwa usahihi hasa kwa kufuata sheria.

Hata hivyo Mmbando amesema  kwamba ni wakati mwakafa wa kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na nchi nyingine ikiwamo Nigeria ili kuona nini cha kujifunza kuendana na wakati kwa mahitaji ya sasa na baadae.

"Nawaomba watumiaji wa mtandao tuendelee kufuata sheria zilizopo ili kuendana na mahitaji ya sasa na baadae lakini kama kutakuwa na maboresho tufikishe maoni yetu kwenye vyombo husika kwa ajili ya kujadili na kujenga hoja," amesema Mmbando

Ameongeza washiriki wametoa maoni yao kulingana na muktadha wa nchi yetu na nchi nyingine za Afrika kama bara moja ambalo linatamani kuwa na maudhui yanayoendana na Waafrika katika kutumia intanenti.

No comments:

Post a Comment

Pages