HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2020

THRDC: NGO's ondoeni ofisi zenu katika majengo ya Umma

 
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa.


Na Janeth Jovin


MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)  ni shirika lisilo la kiserikali lenye lengo la kuhakikisha kuna uwepo wa mazingira salama, mazuri na endelevu kwa watetezi wa haki za binadamu nchini.

THRDC kwa sasa inawanachama binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali  takribani 200, Tanzania Bara na Zanzibar.

Mtandao huu kupitia taasisi zake umekuwa pia ukisaidia wananchi katika masuala mbalimbali ya kisheria pindi wanapopata changamoto na kukosa watetezi au wanasheria wa kuwasimamia mahakamani.

THRDC inatambua kuwa miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo jamii ni uelewa mdogo katika masuala ya sheria hali inayosababisha kuwepo kwa uchelewaji wa kuripoti kesi mahakamani.

Na ucheleshwaji wa kesi hizo usababisha kuharibika au huku taasisi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu kushindwa kabisa kuwatetea na kuwasimamia.

Kutokana na hali hiyo bado kunauhitaji mkubwa wa jamii kujua ni namna gani mtandao huu unavyofanya kazi kwa jamii na kuona wanashirikishwaje katika kusimamiwa kesi zao hususani pale ambapo zinakuwa hazijafika katika hali mbaya ya usimamiwaji.

Hivi Karibuni Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amefanya  ziara ya kutembelea baadhi ya  wanachama wa mtandao huo katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma na Singida.

Olengurumwa anasema lengo la ziara hiyo ni kuangalia ni kwa namna gani Ofisi za wanachama hao zinafanya kazi zao, kubaini fursa na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuweza kuzichukulia hatua.

“Hizi ziara tunazozifanya ni moja ya kazi za mtandao wetu hasa katika kuangalia ni kwa namna gani asasi ambazo ni wanachama wa THRDC zinazofanya kazi hasa katika kuwatetea wananchi wanaokumbana na changamoto mbalimbali za uvunjwaji wa haki zao,” anasema

Anasema katika muktadha wa usalama wa vituo vilivyochini ya mtandao huo vinapaswa  kuwa na ofisi ambazo hazipo katika majengo ya umma ili kupunguza changamoto za kiusalama zinazoweza kujitokeza.

Olengurumwa anasema ofisi hizo zikitoka katika majengo ya umma na kukaa sehemu nzuri ambayo itakuwa rahisi kwa wananchi kuzifikia ili kupata msaada wa kisheria na mawazo katika matatizo yao yanayowakabili ikiwamo kesi mbalimbali.

Akiwa  Mkoani Dodoma  katika ziara yake, Olengurumo anasema inatakiwa ifikie wakati wananchi waanze kupatiwa elimu juu ya utendaji kazi na umuhimu wa asasi na mashirika hayo katika jamii.

“Kuna baadhi ya wananchi bado hawajui Watetezi  wa haki za binadamu wanafanya kazi gani na wengine wanakuwa wanakuja kuripoti kesi zao zikiwa katika hali mbaya hivyo kushindwa kusimamia ipasavyo  mashauri yao.

“Ili tatizo hilo liondoke tunapaswa kutoa elimu kwa jamii namna ambavyo mashirika haya yanavyofanya kazi na mahali halisi yanapopatikana,” anasema

Anasema hivi karibuni mtandao huo umepokea kiasi cha Sh. Milioni 60 kwa ajili ya kutumika katika kuboresha shughuli mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu nchini.

Olengurumwa anasema fedha hizo zitatumika katika kujenga ushawishi na mahusiano kati ya Watetezi wa haki za binadamu na taasisi mbalimbali za Serikali.

Anasema mkataba wa fedha hizo ambao utakaodumu kwa Kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 2020 hadi Julai 2021, unalenga pia kutoa  msaada wa kisheria kwa Watetezi wa haki za binadamu nchini, huku wanufaika wakubwa wa mradi huo wakiwa ni watetezi wa haki za binadamu.

Anasema kupitia msaada huo utaweza kuwafikia watetezi hao ili kufanya kazi kwa umakini na uweledi katika kusimamia majalada mbalimbali.

Kwa Upande wake Wakili Godliver Shiyo kutoka LHRC, anasema wao ni miongoni mwa wanachama wa mtandao huo na kituo chao kimekuwa kikijishughulisha na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa jamii, kuwezesha umma kutambua haki zao, kukuza kuimarisha na kulinda Haki za Binadamu, kutoa elimu kwa jamii juu michakato ya katiba pamoja na kuhamasisha utawala bora nchini Tanzania.

Anasema mbali na kutoa msaada wa kisheria na elimu juu ya michakato ya katiba kituo hiki  kinatumia vipindi vya radio mbalimbali kutoa elimu kwa jamii.

"Tumekuwa tukishirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji na kituo hiki kinashirikiana na Mashirika mengine wanachama wa mtandao katika maswala mbali mbali yahusuyo utetezi wa  haki za binadamu ikiwa pamoja na uchambuzi wa miswada, pamoja na msaada ya kisheria,"anasema Wakili Shiyo

Anasema pamoja na kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na kituo hicho bado kinakabiliana na changamoto kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na uchache wa wateja, kwa Ofisi ya Dodoma kutokana na  ofisi kuwa mpya.

"Kituo hiki tumekizinduliwa mwishoni kwa mwaka 2019 hivyo tumekuwa na mashauri machache ya kuyashughulikia lakini pia Stumeendelea kujitangaza kupitia elimu tunazotoa kwa jamii na vipindi vya radio na changamoto nyingine ni jamii imekuwa na mapokeo hasi juu ya kazi zinazofanywa na watetezi wa haki za binadamu kwa kuwalinganisha na wanasiasa wa upinzani hii ni changamoto kubwa kwetu watetezi,"Anasema Wakili Shiyo

No comments:

Post a Comment

Pages