October 10, 2020

Mabweni mawili yateketea kwa moto

Mabweni hayo ni Bweni la shule ya African Muslim iliyopo maeneo ya Kaloleni mkoani Kilimanjaro na bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Waadventista wa Sabato Tanzania iliyopo Usa river wilayani Arumeru Mkoani Arusha

Mkaguzi wa Jesi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kilimanjaro, Jerimiah Mkomangi amethibitisha leo Oktoba 9,2020  kutokea kwa moto katika bweni hilo la shule ya African Muslim na kwamba ni mara ya tatu kwa shule hiyo kuungua kwa vipindi tofuati

Amesema kwenye tukio hilo hakuna majeruhi wala kifo kwa sababu wanafunzi waliondolewa mapema na kupelekwa sehemu salama ingawa vitu vyao ikiwemo magodoro, vitanda, nguo, madaftari na vitu vingine vimeteketea kwa moto.

Katika bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Waadventista wa Sabato limeteketea kwa moto jana mchana  na kuunguza vifaa mbalimbali vya wanafunzi.

Imeelezwa kuwa moto huo umetokea wakati wanafunzi wa shule hiyo wakiwa madarasani na uchunguzi wa kupata chanzo cha moto huo bado unaendelea.

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Arumeru Mkaguzi Alhaji Kimaro ameeleza vifaa mbalimbali vya wanafunzi katika vyumba 14 vimeteketea kabisa na moto kati ya vyumba 30 vilivyopo katika bweni hilo.

Naye Mkuu wa shule hiyo Mborega Petro amewaomba wasamaria wema kuwasaidia kwa hali na mali wanafunzi ambao wamepoteza vifaa vyao vya matumizi ya kila siku ya shuleni hapo.

No comments:

Post a Comment

Pages