HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 02, 2020

NIT chaanza kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa kozi za usafiri wa anga

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa (wa kwanza kushoto) akikata utepe kuashuria uzinduzi wa mafunzo kwa wakufunzi ya kozi nne za sekta ya anga jwa viwango wa kiamtaifa, katika ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa anga Tanzania (TCAA) Johari Hamza.

 

NA JANETH JOVIN

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimefanikiwa kupata ithibati ya kuendesha kozi nne za sekta ya anga za viwango vya kimataifa baada ya kukidhi vigezo vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) lenye makao yake makuu nchini Canada.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati akizinduzi kozi hizo ambazo zitatolewa kwa wakufunzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Johari Hamza amekipongeza chuo hicho kwa kukidhi vigezo vya kupata ithibati ya kuendesha kozi hizo ambazo ni muhimu  katika kuboresha Sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.

Amesema NIT kimekuwa kikifanya jitihada kubwa hadi kukidhi vigezo vya kupata ithibati ya kuendesha kozi hizo nne muhimu zenye viwango vya kimataifa na kuongeza kuwa ni dhahiri Sekta ya Anga sasa inaenda kukua kwa viwango vya Kimataifa hapa nchini.

"Tumeshuhudia kwa muda mrefu upungufu mkubwa wa wataalamu katika Sekta ya Anga lakini kupitia kozi hizi tatizo hili linaenda kupata muarobaini," amesema Hamza.

Hamza amesema katika kuhakikisha kuwa mafunzo haya yanaendelea kutolewa kwa viwango stahiki, wao kama Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga watashirikiana na NIT bega kwa bega ili kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanakuwa endelevu na yanaleta tija kwa jamii na Taifa nzima kwa ujumla.

"Ni matumaini yangu kuwa wadau wa usafiri wa anga wataitumia fursa hii kupata mafunzo hapa chuoni ambayo ni gharama nafuu ukilinganisha nje ya nchi," amesema Hamza.

Hata hivyo amesema kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo ya IATA wanao utaratibu wa kuwajengea uwenzo wakufunzi wa kozi hizo ili kuziendesha kwa utaalamu na ueledi wa hali ya juu.

"Nimeshaambiwa kuwa mwezeshaji kutoka IATA yupo hapa nchini ili kuendesha mafunzo haya kwa wakufunzi na wao waweze kufundisha vijana wetu hapa," amesema

Aidha, amesema utekelezaji na uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji, kitasaidia kutekeleza malengo ya uanzishwaji wa Chuo hicho.

"Hata hivyo hadi sasa tayari Serikali imeshapokea ndege mpya nane kati ya 11 zilizonunuliwa, ujenzi na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchi nzima. Viwanja hivi ni pamoja na Ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere,"

"Kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hii kutaongeza idadi na miruko ya ndege na huduma nyingine nyingi. Hivyo, Mafunzo haya ni muhimu sana katika kuimarisha na kuboresha usafiri wa anga hapa nchini," amesema Hamza

Naye, Mkuu wa Chuo Cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema kozi hizo zipo za aina mbili, ambapo moja ni kwa wale ambao tayari wameshasoma masuala ya anga na wapo kazini ambao wanataka kujenga uwezo na kwa wale ambao ni wapya, ambao watasoma kulingana na historia yao ya masomo.


"Kozi hizi zitakuwa za muda mfupi, ambapo wale ambao wanafanyakazi wanaweza kusoma kwa siku tatu, nne au tano, lakini wale wapya watasoma kwa siku kumi au wiki mbili itagemea na historia yao ya masomo, amesema Profesa Mganilwa


Profesa Mganilwa amesema kozi hizo watu walikuwa wanatumia gharama kubwa kwenda kusoma nje ya nchi, unakuta gharama ya kwenda na kurudi ni Dora za Marekani 800 na unakuta anakaa kwa siku tano, ambapo kila siku atakuwa analipa dola 400.


"Tumeamua kuanzisha kozi hizi hapa nchini kwa lengo la kupunguza gharama, kwa sababu mtu anaweza akatoka ofisini, nyumbani akaja akasoma hapa kwa gharama za kawaida, "amesema Profesa Mganilwa


Amesema mchakato huo wa kupata ithibati unavigezo vitatu, kigezo cha kwanza ni kuangalia wakufunzi, cha pili ni walimu kujengewa uwezo, ambapo wataangaliwa kama watafaulu au la kwa sababu hizi kozi zote zinaendana na mitihani, ambapo anaamini wote 25 watafaulu.

Pia, amesema hatua ya tatu  ni kuanza kufundisha, ambapo kwa hatua hiyo  bado gharama hazijaweza kujulikana wakishamaliza Novemba wataweza kujua wanafunzi wanatoka wapi na ambapo ndiyo wataweza panga gharama.

Amesema mtaalumu wa kozi hizo nne, ametoka nchini Uingereza, ambapo akishamaliza mwingine atakuja kwa ajili ya kumalizia kozi zingine.

No comments:

Post a Comment

Pages