HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 26, 2020

Covid 19 na Athari zake katika Upatikanaji wa Chakula na ilivyopandisha bei za limao, ndimu nchini Tanzania


Na Janet Jovin

Novemba 2020

 

JANUARI 30, 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza rasmi ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) kuwa ni dharura ya jamii kimataifa na Machi 11, mwaka huu likatangaza kuwa ni janga la dunia.


Ugonjwa huu ulipotangazwa, mataifa mengi yaliingiwa na hofu ambayo iliwafanya watu duniani kupoteza maisha huku wengine wakikata tamaa hata ya kuishi.


Kwa hapa nchini takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha kuwa hadi kufikia Aprili 24, 2020 jumla ya wagonjwa 284 walithibitika kuwa na maambukizi ya Covid 19, kati yao waliopona ni 48 na waliofariki walikuwa 10.


Aidha takwimu za WHO zinaonesha kuwa hadi kufikia Oktoba 9, 2020 jumla ya nchi 235 duniani zimeripoti kuwa na virusi vya corona ambapo watu milioni 36.2 wameugua huku milioni 1.05 wamefariki duniani.


Hata hivyo, ugonjwa huu uligundulika Tanzania mwezi wa Machi 16, 2020. Hii ni siku ambayo Mtanzania wa kwanza mwenye umri wa miaka 46 alitangazwa kuwa na virusi vya korona. Mtanzania huyo ndiye aliyekuwa amesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark na aliporejea Tanzania na kupimwa aligundulika kuwa na virusi hivyo.


Pamoja na ugonjwa huu wa korona kusababisha vifo na kuleta athari mbalimbali katika jamii, inaelezwa kuwa ulisababisha pia kasi ya uzalishaji wa chakula katika maeneo mengi duniani kupungua kutokana na watu kuwa na uoga wa kutoka ndani kwenda kufanya shughuli zao.


Kwa Tanzania, kipindi cha mwanzo cha ugonjwa huu wa Covid 19 ulisababisha athari mbalimbali hasa katika upatikanaji wa mazao ya matunda ambayo ni ndimu na limao. Vilevile ugonjwa huu licha ya kusababisha athari hizo pia uliwafundisha watu namna ya kuhifadhi chakula.


Omary Rashidi ni mfanyabiashara katika soko la Ilala. Omary anasema licha ya kuwepo kwa mazao mbalimbali upatikanaji wa matunda kama ndimu na limao ulikuwa mgumu katika kipindi cha corona.

Anasema ndimu na limao vilikuwa vikipatikana kwa shida na vilipanda bei kutokana na watu wengi wakivitumia kama tiba asili dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.


“Viungo hivi vilipanda bei katika masoko yote jijini Dar es Salaam kutokana na bidhaa hizo kuwa na mahitaji makubwa hata katika masoko ya Nairobi na Mombasa nchini Kenya,” Omary alieleza. 


Mfanyabiashara huyo anasema mwanzoni mwa Julai mwaka huu kipindi ambacho corona ilichachamaa, kiroba kimoja cha malimao shambani kiliuzwa Sh. 90,000 kutoka Sh. 40,000 na ndimu ziliuzwa sh.95,000 hadi 100,000 kutoka 60,000.


“Bei hiyo ilikuwa ni kutoka shambani, hapo bado mtu hajasafirisha kuleta hapa sokoni Dar es Salaam. Hali hiyo ilisababisha katika masoko ya Mabibo, Temeke na Ilala wafanyabiashara kuuza limao moja Sh. 500 hadi 700,” anasema.


Hata hivyo anasema magari mengi ya Tanzania ya mizigo yalikuwa yakienda Kenya na ya Kenya kuja hapa nchini kwa ajili ya kufuata malimao na ndimu kutokana na mahitaji makubwa ya watu ambao walitumia kama tiba dhidi ya virusi vya corona.


“Kiukweli waliokuwa wakiuza malimao na ndimu walipata fedha sana kipindi cha corona licha ya mazao hayo kupatikana kwa tabu, hata hivyo kama fedha hizo hawakuzifanyia kitu cha maendeleo basi nitawashangaa sana,” anasema.


Halfan Hamisi ni mfanyabiashara katika soko la ndizi lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam. Hamisi anasema katika soko hilo hilo upatikanaji wa mazao ya chakula haukuwa wa shida lakini kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakinunua bidhaa za vyakula kwa wingi.


Anasema watu hao walikuwa wakinunua vyakula hivyo kwa lengo la kwenda kuhifadhi ndani kwa kuhofia kuwa litatolewa agizo la watu kutotoka nje.


“Wafanyabiashara wa chakula hapa kwetu walifanya sana biashara kwani watu wengi walikuwa wakinunua vitu na kuhifadhi ndani kwa kuhofia wanaweza kukumbwa na njaa pindi watakapoambiwa wasitoke nje,” anasema na kuongeza.


“Kipindi cha corona nilijifunza pia namna ya kuweza kubana matumizi, kuhifadhi chakula na nilitambua kuwa kama sitaweza kuwa na chakula cha akiba nitakwama hasa katika kuendesha familia yangu, kila wakati nilimsisitizia mke wangu juu ya umuhimu wa kutumia vitu vizuri tena nikamwambia hakuna kitu kitakachotupwa,” anasema.


Yasemavyo mashirika ya Chakula duniani

 
Katika ripoti ya pamoja kuhusu usalama wa chakula na lishe duniani iliyotolewa Julai 13, 2020 na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Kilimo na Chakula (IFAD) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), imeeleza namna ambayo mataifa mbalimbali watavyokumbwa na baa la njaa kutokana na uwepo wa corona.


Taarifa hiyo imeonesha kwamba, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kutokana na janga kubwa la corona inakadiriwa kwamba watu zaidi ya milioni 130 wanaweza kushambuliwa na baa la njaa.


Takwimu za mashirika hayo zimeonesha pia, waathirika wakubwa wa baa la njaa duniani ni watu kutoka barani Asia, Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean.


Waziri Hasunga afunguka

 
Akitoa taarifa kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na upatikanaji wake hapa nchini kwa msimu wa mwaka 2020/2021, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema nchi inakiwango cha utoshelevu wa mazao hayo.


Hasunga anasema tathmini iliyofanyika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inasema kwa kuzingatia kigezo cha upimaji wa kiwango cha utoshelevu, matokeo yanaonesha kuwa kwa mwaka 2020/2021, nchi inatarajiwa kuwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 124.


Vilevile, Waziri Hasunga alisema kiwango hicho kimeongezeka ikilinganishwa na msimu wa 2018/2019 katika kipindi kama hicho ambapo kiwango cha utoshelevu wa chakula kilikuwa asilimia 119.


Aidha anasema Serikali imeendelea kuhimiza na kuelekeza wakulima kuzalisha kwa tija ili kuongeza uzalishaji na kufanya uimarisha mifumo ya usambazaji na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati hususani mbolea, mbegu bora, viuatilifu na zana bora za kilimo.


Hata hivyo Wizara hiyo ya Kilimo kwa kushirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na NBS, mwezi Juni 2020 ilifanya tathimini ya Hali ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula kwa msimu wa 2019/2020 na Upatikanaji wa Chakula kwa mwaka 2020/2021.


Tathimini hiyo ilifanyika katika mikoa yote 26 na kuhusisha halmashauri 184 za Tanzania Bara kwa lengo kubaini uzalishaji na mahitaji.


Kwa mujibu wa tathimini hiyo, hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini iliendelea kuwa nzuri kipindi chote cha zaidi ya miaka mitano mfululizo licha ya ugonjwa wa Corona kuingia nchini Machi, 2020.

Ilionesha kuwa nchi inatarajiwa kuwa na ziada ya tani 3,394,434 za chakula, ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2,072,413 ni za mazao yasiyo nafaka.


Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa anasema wao wana jukumu kuu la kuhakikisha usalama wa chakula ndani ya nchi kwa kununua, kuhifadhi, kutoa chakula katika maeneo yenye upungufu na kwa waathirika wa majanga mbalimbali.


Anasema NFRA pia inazungusha na kuuza akiba ya chakula ili kutoa nafasi ya uhifadhi na kupata fedha za ununuzi akiba mpya ya chakula.


“NFRA inatekeleza majukumu yake kupitia Kanda nane ambazo ni Arusha, Kipawa (Dar es salaam), Dodoma, Shinyanga, Makambako, Songea, Songwe na Sumbawanga. Kwa sasa, NFRA inamiliki jumla ya maghala 34 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 251,000,” anasema.


Vilevile anasema Wakala imekuwa ikinunua nafaka mbalimbali kutoka kwa wakulima kila mwaka hivyo kuwapatia wakulima soko la uhakika la mazao ya nafaka. 


Aidha, anasema Wakala imeweza kuhakikisha usalama wa chakula kwa kuhifadhi akiba ya kutosha kila mwaka na kutoa na kuuza akiba ya chakula kwa ajili ya kukabiliana na majanga mbalimbali. 


“Wakala imeweza kuuza akiba ya chakula ndani ya nchi katika halmashauri za Wilaya mbalimbali zilizokabiliwa na upungufu wa chakula hivyo kupata fedha za kununulia akiba mpya ya chakula,” anasema.


Lupa anasema Wakala huo umeongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka na inatekeleza mradi wa kuongeza uwezo huo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000. 


“Mradi huu unajumuisha ujenzi wa vihenge 56 na maghala ya kisasa 9 ambavyo kwa pamoja vinaongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 250,000. Kwa sasa Mradi huu umefikia asilimia 75 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2020/2021,” anasema.


Lupa anasisitiza kuwa kutokana na utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi, Wakala umeweza kuhakikisha usalama wa chakula nchini na kuwezesha Serikali kusaidia nchi jirani zilizokabiliwa na upungufu wa chakula. 


Katika kipindi cha miaka mitano, Wakala imeweza kutoa msaada wa chakula kwa nchi za Malawi na Sudani ya Kusini zilipokumbwa na janga la mafuriko na upungufu wa chakula.


Aidha anasema mkakati wa Wakala ni kupanua wigo wa uhifadhi na masoko ili kuwezesha kuhifadhi chakula cha kutosha na kupata masoko zaidi ya nafaka ndani na nje ya nchi, hivyo kuchangia katika ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.

 

Hadithi hii iliungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti  Majanga

 This story was supported by Code for Africa’s WanaData Initiative, Twaweza and the Pulitzer Center on Crisis Reporting.

No comments:

Post a Comment

Pages