HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 25, 2020

Miujiza ya USMJ Mtawatawa

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale, James Milanzi, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Wanakijij wa Kijiji Mtawatawa wakiwa  kwenye mkutano na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho kuona namna USMJ inavyotekelezwa kijijini hapo.
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mtawatawa Benadetha Kitang'ita akitoa ufafanuzi wa namna USMJ ilifanya miujiza kijijini hapo.
Ofisa Misitu Wilaya ya Liwale mkoani LindiNassoro Mzui (wa tatu kulia), Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA Elida Fundi (wa nne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wasimamizi wa misitu wa Mbila baada ya kutembelea msitu huo ambao umekuwa na faida lukuki kwa wananchi.

 

NA SULEIMAN MSUYA, LIWALE


USIMAMIZI Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) unaoratibiwa na mashirika mbalimbali na serikali umefanya miujiza katika vijiji vingi vya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi kikiwemo kijiji cha Mtawatawa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mtawatawa, Benadetha Kitang'ita wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho ambacho kinashiriki kwenye miradi ya USMJ inayotekelezwa wilayani Kilwa.

Waandishi hao walifanya ziara ya siku tano katika mkoani ya Iringa na Lindi kuangalia hali ya USMJ kupitia Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST) na uratibubu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) ambayo yanafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).

Kitang'ita ambaye ni Ofisa Kilimo wa kijiji hicho amesema kwa kipindi cha miaka mitano kupitia USMJ wamefanikiwa kukusanya zaid ya shilingi milioni 379 ambapo asilimia 55 ya mapato hayo yametumika kwenye kijiji ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 200.

Amesema fedha hizo zinatokana na uvunaji na uuzaji wa mazao ya misitu kwa mfumo endelevu wa rasilimali misitu zilizopo Msitu wa Mbila.

Alisema kwa miaka mitano kijiji kimeweza kuchangia kwenye Halmashauri ya Liwale ambapo zaidi ya shilingi milioni 150 zimetolewa.

Akifafanua maajabu ambayo yametokea Mtawatawa ni pamoja na kuchimba kisima chenye urefu wa mita 75 kwa shilingi milioni 12 hivyo kuondoa adha ya maji.

"Pia USMJ umewezesha ujenzi wa nyumba ya kuishi mtendaji kwa shilingi milioni 28, choo cha ofisi ya kijiji kwa shilingi milioni 6, tumekarabati jengo la Zahanati ya kijiji kwa shilingi milioni 24 ambalo lilisimama kwa miaka saba.

Pia tumenunua trekta kwa shilingi milioni 71 hivyo tunalitumia kwa kuongeza tija ya uzalishaji pamoja na kufanya kazi ya kubeba mbao ambazo zinavunwa kwa njia haramu," amesema.

Kitang'ita amesema trekta hiyo inatumika kukodishwa kwa ajili ya kulimia wananchi ambapo uzalishaji umeongezeka mara dufu.

"Trekta imewezesha uzalishaji kuongezeka kwa kulima hekari 235 kwenye bonde la kijiji na  ukijumlisha na wananchi mmoja mmoja zaidi hekari 500 na uzalishaji umeongezeka.

Kaimu mtendaji amesema maajabu mengine ya USMJ Mtawatawa ni ujenzi wa darasa moja ambalo limegharimu shilingi milioni 18.

"Kijiji kimetumia fedha zitokanazo na USMJ kuajiri mwalimu ambaye analipwa shilingi 200,000 kwa mwezi kwa miaka mitano lengo ni kukabiliana na uhaba wa walimu kwani tuna walimu wanne tu," amesema.

Aidha amesema kijiji kimenunua pikipiki tatu kwa kutumia fedha za USMJ jambo ambalo linaongeza uhifadhi na ulinzi wa misitu.

Amesema wametoa mchango kwenye Kituo cha Afya Kibutuka shilingi milioni 3 na kuchangia shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Kiangara.

"USMJ imesaidia kuongeza ufaulu na ufanisi kwa wanafunzi ambapo tumechangia fedha za kuweka wanafunzi katika kambi ambapo tumekuwa tukitoa shilingi 500,000 hivyo kuwapunguzia maumivu wazazi," amesema.

Kitang'ita amesema pia kijiji kimeweza kulipia kodi ya nyumba kwa ajili ya wauguzi wawili ambao hawana nyumba za kuishi.

Amebainisha kuwa maajabu ya USMJ Mtawatawa ni kijiji kuweza kulipa posho wajumbe wa kijiji na wahifadhi wa kamati ya maliasili.

"Sisi tukikutana kwenye mkutano mkuu wa kijiji tunahakikisha tunapika chakula na kuwapatia maji wajumbe wote hali ambayo inachangia ushiriki wa wananchi wengi," amesema.

Ofisa Kilimo huyo amesema katika vijiji 72 vya wilaya ya Liwale Mtawatawa imefanikiwa kupitia USMJ hivyo kuahidi kuendeleza kwani faida wanaiona.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtawatawa Omary Shamte, amesema sekta ya misitu imeweza kuwakomboa na pongezi kubwa ziende kwa Shirika la Limasi na Mradi wa Kuongeza Mnyororo wa Thamani kwenye Mazao ya Misitu (FORVAC).

"FORVAC na Limasi wametufungua macho hivyo ujio wa CoFoREST kupitia MJUMITA na TFCG ni jambo jema kwani watagusa matamanio yetu," amesema.

Kindamba Machwiiko Mzee wa Kijiji cha Mtawatawa, amesema uhifadhi unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa una faida kubwa kwa wananchi.

Ofisa Misitu Wilaya ya Liwale, Nassoro Mzui amesema wilaya hiyo ina vijiji 27 ambavyo vinajihusisha na USMJ katika msitu wa Angai.

Amesema idara yake imekuwa ikifanya vizuri kupitia USMJ kwani jamii imekuwa ikinufaika hivyo kushiriki kuilinda.

Mzui amesema ipo changamoto kubwa ambayo inachangiwa na ukumbwa wa misitu hivyo ulinzi kudororo.

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale, James Milanzi amesema ujio wa CoFoREST na miradi mingine ni muhimu kwani unachochea kukuza uchumi, maendeleo na uhifadhi.

Milanzi amesema miradi hiyo inapunguzia jukumu halmashauri bajeti ya utekelezaji miradi kama maji, afya, elimu na nyingine hivyo mpango wao ni kusambaza wazo hilo la wadau kwa kutumia fedha za halmashauri.

Ofisa Sera na Uraghibishi wa MJUMITA, Elida Fundi amesema ziara hiyo ya siku tano iliyonzia Kijiji cha Mahenge, wilayani Kilolo mkoani Iringa hadi Darajani na Mtawatawa wilayani Liwale ina lengo la kujifunza na kutoa taarifa za USMJ ilivyo na faida kwa jamii.

Fundi amesema dhana hiyo ya USMJ imepokelewa kwa mtazamo chanya kwani maendeleo na uhifadhi umeonekana kuwa mzuri.

"Ziara hii imeonesha tunachokipigania kina matokeo chanya kwa wanavijiji kusema wenyewe faida ni nyingi kuliko hasara," amesema.

Fundi ameitaka Serikali kuhamasisha na kutoa elimu ili dhana ya USMJ inasambaa nchini kote ili kukusuru vijiji ambavyo vina misitu ila haina mipango ya kuihifadhi kwa njia endelevu.


No comments:

Post a Comment

Pages