November 23, 2020

NMB YASAIDIA SEKTA YA AFYA NA ELIMU MKOANI LINDI

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Renatus Mchau, akipokea msaada wa madawati 100 toka Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini, Janeth Shango, msaada huo ni kwa ajili ya Shule ya Msingi Kipindimbi wilayani humo baada ya kuwa na ongezeko la wanafunzi kutokana na kufungwa kwa shule ya msingi Njinjo iliyokumbwa na mafuriko mwanzoni mwa mwaka huu. Katikati ni Nelly Masisi, Meneja NMB Kilwa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na wazazi na wanafunzi wa shule hiyo mwishoni kwa wiki.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Renatus Mchau, akizungumza wakati wa hafla ya kupokea msaada wa madawati 100 toka Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini, Janeth Shango.

 

 

Na Mwandishi Wetu

 

BENKI ya NMB imetoa misaada kwa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi katika sekta ya afya na elimu yenye jumla ya shilingi milioni 12.5 .

 

Misaada hiyo ni urejeshaji wa faida ya benki hiyo kwa umma. Kwa mwaka huu  benki hiyo imetenga zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya kusaidia jamii.

 

Akikabidhi  misaada hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa Renatus Mchauru, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini, Janeth Shango, alisema  benki imewiwa kutoa misaada hiyo baada ya kuombwa na jamii.

 

Alisema wakati anapata matibabu katika kituo cha afya Masoko, alibaini hitilafu zilizokuwepo  katika kituo hicho na alipozungumza na utawala walimweleza tatizo na kuwashauri waandike barua ya kujieleza, kitu ambacho walifanya.

 

Alisema benki ya NMB imekarabati jengo la Baba, Mama na Mtoto  kwa kuweka paa jipya, kupaka rangi na kuweka michoro ambayo inaleta taswira njema kwa wadau wanaofuata tiba.

 

Alisema benki hiyo inaona fahari kusaidia eneo hilo ili liwe rafiki kwa wahitaji.Alisema kazi ya kukarabati jengo hilo la hospitali katika kituo cha afya Masoko uligharimu Sh milioni 2.5.

 

Naye Mganga Mfawidhi  wa kituo hicho, John Nkuba alishukuru Benki ya NMB kwa msaada wake na kusema kwamba mazingira ya matibabu sasa baada ya ukarabati huo yako bora zaidi.

 

Alisema kituo hicho kinachohudumia watu 50 kwa siku bado kinahitaji pia mashuka, vitanda na  nishati mbadala.

 

Mkurugenzi wa wilaya ya kilwa Renatus Mchauru pamoja na kushukuru kwa misaada hiyo, aliwataka watumishi kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bora zaidi kulingana na uzuri wa majengo yaliyopo sasa.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati katika shule ya msingi ya Msingi Kipindimbi, Shango alisema wametoa madawati 100 kwa ajili ya wanafunzi wapya wa shule hiyo.

 

Shule hiyo iliyokuwa na madawati 100  ilizidiwa baada ya wanafunzi kuongezeka kufuatia maafa ya mafuriko  yaliyokumba shule na makazi katika kata ya Njinjo mwanzoni mwa mwaka huu. Shule hizo ni pamoja na Njinjo na Ndende.

 

Maafa hayo yaliyokumba watu zaidi ya 6,804 katika kata ya Njinjo yalisababisha  shule ya Kipindimbi  wanafunzi wake kuongezeka kutoka watoto 400 hadi 909 na kusababisha upungufu wa madawati zaidi ya 100.

 

Katika hafla zote mbili Shango alishauri wazazi kuanza mapema kuwafunza watoto wao kuweka akiba kwa kuwafungulia akaunti watoto wao ili waweze kuja kujisaidia  siku za baadae.

 

“Wazazi wafungulieni akaunti unaweza kuanza na Sh 10,000 na kuendelea kuchangia  kila mwezi Sh 1,000 au zaidi ili zimsaidie anapokuwa mkubwa” alisema Shango.

 

 Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Bahati alisema pamoja na kusaidiwa madawati hayo , shule hiyo bado inakabiliwa na tatizo la matundu ya choo kwa wanafunzi na walimu na  pia nyumba za walimu.

 

Wanafunzi wa shule hiyo Khalid Salim na Neema Ali waliishukuru benki ya NMB kwa kuwasaidia madawati hayo na kuwataka wawasaidie pia matundu ya choo.

No comments:

Post a Comment

Pages