HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 11, 2020

*Unafahamu unywaji wa maji mengi unasababisha maradhi ya moyo?*

Lakini, mtaalamu bingwa kutoka *Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi,* ana kidokezo kuhusiana na matumizi ya nadharia hiyo kiholela kwamba yanaweza kumrudisha mhusika katika maradhi zaidi.

Profesa Janabi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo anasema maji hayo ya ziada yanakuwa na manufaa kwa mnywaji iwapo tu kuna kiwango sahihi cha kuushughulisha mwili wake hata maji hayo yakatumika kwa manufaa kiafya.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, katika hali ya kawaida, mwili wa binadamu huwa na kiwango cha wastani wa lita tano za maji zinazokuwa kwenye mzunguko mwilini na panapotokea maji ya ziada pasipo kutumika, ni hali inayouchosha moyo na kuishia katika kuzalisha maradhi.

Mtaalamu huyo anafafanua kwamba mwili wa binadamu unapokosa shughuli ngumu zinazosababisha jasho kutoka, kiwango cha juu cha unywaji maji kinapaswa kisizidi kati ya lita moja na nusu hadi mbili kwa siku.

“Maji yanayohitajika kwenye mwili wa binadamu kwa siku ni lita moja na nusu, kama hamna joto wala hufanyi kazi ngumu, unasababisha hatari kwenye moyo wako.

“Mzunguko wa damu tayari una lita tano na wewe unakunywa lita tano, kwa hiyo unaulazimisha moyo kusukuma mara mbili zaidi na mwisho wa siku unajikuta una shida ya moyo,” anatahadharisha.

Profesa Janabi anaeleza kwamba, wakati moyo wa mtu unafanya ya kusukuma maji ya ziada kuliko uwezo wake, athari inayofuata baada ya hapo ni baadhi ya chembe hai muhimu zinaanza kufa moja baada ya nyingine zikipishana na maradhi kuanza kuchukua nafasi yake.

Bingwa huyo wa maradhi ya moyo, alitoa katika hadhira ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, Septemba 29 mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.

Mtalaamu huyo anaelekeza kidole cha tahadhari hasa kwa watendaji wa maofisini na mazingira yanayofanana nayo kwamba mbali na hatari ya kuuchosha moyo, pia ziada ya maji hayo imebeba hatari kuyeyusha madini muhimu kwa mwili wa binadamu.

*ULAJI NAO TATIZO*

Profesa Janabi anataja sababu nyingine kubwa ambayo watu hawafahamu kama ni chanzo cha kuugua maradhi ya moyo kuwa ni ulaji usio wa mpangilio.

Anasema ulaji wa vyakula vya mafuta umekuwa ukitajwa na wengi kuwa tatizo kubwa katika kusababisha maradhi ya moyo, lakini siyo chanzo wala tatizo kubwa bali *Ulaji wa vyakula vya wanga ndiyo mzizi wa tatizo.*

Anasema vyakula vya wanga kama *Ugali na We* vinavyoliwa mara nyingi na Watanzania huhatarisha usalama wa moyo na hivyo *Anashauri* watu *kupunguza* ulaji wa aina hiyo ya vyakula.

*“Ukiweza kujibana, basi unaweza kupunguza kula ugali na wali angalau ule mara mbili kwa wiki kwa vyakula hivi,”* anashauri Profesa Janabi.

Anasema ratiba ya vyakula hivyo pia ni lazima izingatiwe na walaji kwa usalama wa moyo.

*“Mtu anakula saa tatu, nne hadi saa sita usiku sahani kubwa ya wali au ugali, akimaliza hapo anaingia kitandani analala, hapo badala ya chakula kufanya kazi kinaenda kukaa kwenye stoo,”* anatahadharisha Profesa Janabi.

Anasema mlundikano huo ndiyo husababisha zaidi madhara kwa mwili wa binadamu kama vile kutengeneza vitambi, shinikizo la damu na matatizo ya moyo.

Profesa Janabi anashauri kuwa muda sahihi wa kula chakula ni kuanzia saa 12 jioni hadi saa 1:00 usiku, ikiwa ni saa chache kabla ya kwenda kulala.

*HALI ILIVYO KITAIFA*

Profesa  Janabi anasema magonjwa ya moyo huchangia karibu asilimia 31 ya vifo vyote duniani na kwamba takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinabainisha kuwa kila mwaka, takribani watu milioni 18 hufariki dunia kutokana na maradhi hayo.

“Ni tatizo linaloonekana kuongezeka, takwimu zinaonyesha katika kila wanawake wanne na wanaume watano, mmoja ananakabiliwa na tatizo la shinikizo la damu,” anabainisha.

Anaongeza  kuwa magonjwa ya moyo ni kati ya magonjwa yasiyoambukiza, ambayo kinga ni rahisi kuliko tiba, ndiyo maana WHO pamoja na Jumuiya ya Magonjwa ya Moyo Duniani baada ya kuona yanaongezeka, wakaamua kuanzisha Siku ya Moyo Duniani.

"Watu pia wanapaswa kuzingatia unywaji wa pombe kwa kiasi, kuacha uvutaji wa sigara, kula vyakula vinavyofaa, wazingatie kunywa dawa wanazoandikiwa (waliokutwa na matatizo haya) na wafanye mazoezi, wapunguze uzito uliopitiliza. Haya ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wa mtu bila gharama,” anasema.

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa JKCI tangu mwaka 2015 ilipoanzishwa hadi sasa, tayari imeshaona takribani wagonjwa 350,000 huku 6,000 kati yao wakifanyiwa upasuaji.

“JKCI tupo mstari wa mbele kutoa elimu ili watu waepuke magonjwa haya,” anasema Profesa Janabi.

BP IKO JIRANI

Mtaalamu huyo anabainisha kuwa asilimia 70 ya wagonjwa wanaotibiwa JKCI, wanakabiliwa na tatizo la Shinikizo la Damu (BP).

Anasema takwimu zao zinaonyesha ndiyo tatizo linaloongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa katika taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Samweli Rweyemamu, anasema wapo pia wengine wanaokabiliwa na tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye moyo ambayo husababisha kifua kuuma.

“Kuna wengine wanaohitaji upasuaji na idadi inaongezeka kila siku. Kwa mfano, wale ambao mishipa ya damu inaziba, tunawazibua kwa upasuaji mkubwa au ule wa tundu dogo,” anasema Dk. Rweyemamu.

Anabainisha kuwa hadi Desemba mwaka jana, waliwachunguza karibu wagonjwa 1,000, ambao awali walikuwa wakipewa rufani ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Daktari bingwa huyo anasema kuwa kwa siku, huwa wanaona wagonjwa kati ya 300 na 400, hali inayoonyesha kwamba watu wenye matatizo ya moyo wanaongezeka nchini.

Dk. Rweyemamu anatoa mfano I got kwamba Wilaya ya Temeke kwenye Viwanja vya Zakheem walipima watu 100 na kati yao, asilimia 18 walikuwa na BP IS na wengine moyo umetanuka. Pia, 21 walionekana wana matatizo ya moyo.

Anasema pia walifanya kazi kama hiyo katika viwanja vya Mwembe Yanga kwa watu 150 na kati yao, asilimia 22 walionekana kuwa na maradhi ya moyo. Anasema kati ya hiyo asilimia 22, asilimia 19 walikuwa na shinikizo la damu la juu.

Anaongeza kuwa idadi hiyo inawezekana kuwa ni ndogo lakini utafiti uliofanyika Dar es Salaam, unaonyesha karibu asilimia 30 wana shida ya shinikizo la damu.

“Sasa ukiwa na shinikizo la damu ni ‘risk factor’ (ishara hatari) ya kuziba kwa mishipa ya moyo hatimaye utafika kwetu tukuzibue kwa vifaa maalum,” anasema Dk. Rweyemamu.

Anasema mtu akiwa na shinikizo la damu, moyo hutanuka na kuwa na dalili za kushindwa kufanya kazi, hivyo asilimia kubwa ya matatizo ya moyo kwa watu wazima yanaanza na presha.

Mratibu wa Tiba wa Manispaa ya Kinondoni kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk. Omary Mwangaza,  anasema kipindi cha Julai na Agosti mwaka huu, katika vituo vya kutolea huduma za afya, waliibua wagonjwa wapya zaidi ya 600 wanaokabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza.

“Shinikizo la damu na kisukari ni magonjwa yaliyokuwa yakiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa, wagonjwa wote hawa tumewaingiza kwenye mfumo wetu wa matibabu,” anabainisha.

No comments:

Post a Comment

Pages