HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 21, 2020

WAZIRI MKUU ATOA SIKU 15 HOSPITALI YA UHURU IKAMILIKE

*Asema lengo ni kuhakikisha inazinduliwa Desemba 9, 2020  

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kwa uongozi ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Suma JKT wahakikishe ujenzi wa hospitali ya Uhuru katika Halmashauri ya Chamwino unakamilika.

 

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu amesema lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inazinduliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ifikapo Desemba 9, mwaka huu ili kutimiza maono yake ya ujenzi wa hospitali hii.

 

“Nimeridhika na hatua hii ya ujenzi lakini haitoshi, hamieni hapa, huu ni wakati wa kazi, hakikikisheni kazi inafanyika usiku na mchana ili Desemba 5, 2020 kazi ikamilike na Desemba 9, 2020 izinduliwe”

 

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa anataka kuona vifaa vyote vya ujenzi wa hospitali hiyo vinatoka kwenye viwanda vya ndani ili kuharakisha ukamilishwaji wa hospitali hiyo hasa marumaru kwani tayari tuna viwanda vikubwa vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa ubora wa hali ya juu. 

 

“Mnabishana kuhusu uwekaji wa tiles, mnataka za nje? TBA mnang’ang’ania kununua tiles kutoka nje ya nchi, kwa nini? Sisi tumehamasisha ujenzi wa viwanda na viwanda vipo vinavyotengeneza tiles tena nzuri, tuna kiwanda Chalinze kikubwa sana na kingine kipo Mkuranga, hata jengo letu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeweka tiles za ndani, na bora mshitiri hujazinunua, na usinunue kutoka nje, tuna viwanda vipo nchini,” amesisitiza.

 

Akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMSEMI), Mhandisi Joseph Nyamhaga amesema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Magufuli alilolitoa kuwa kiasi cha sh. milioni 995.1 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru mwaka 2018 zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo. Pia, Januari 2019, wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya simu ya Airtel, aliagiza kiasi cha sh. bilioni 2.415 zitumike kwenye ujenzi huo.

 

Amesema hadi kufikia Novemba 19, mwaka huu, kiasi cha sh. 4,430,721,498.00 kilikuwa kimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. “Kiasi ambacho kimetumika ni sh. 4,062,310,051.76 na kiasi ambacho hakijatumika ni sh. 368,411,446.24,” amesema.

 

Akielezea mipango ya baadaye, Mhandisi Nyamhanga amesema kwa mwaka 2020/2021, Serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 ambazo kila moja imetengewa sh. bilioni moja. Aidha, alisema sh. bilioni 27.75 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati 555 ambapo zahanati tatu zitajengwa kwa kila Halmashauri na kila zahanati inagharimu sh. milioni 50.

 

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Laurence Lukema amesema wao kama wakandarasi wa ujenzi, watahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati.

 

No comments:

Post a Comment

Pages