December 04, 2020

FORVAC yanunua mashine za kisasa kuokoa upotevu mazao ya misitu

 


Bwana Miti, Yusuph Kiangio, akieleza waandishi wa habari waliotembelea kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kupitia uratibu wa FORVAC, kujifunza namna mazao ya misitu yanavyoweza kuongezwa thamani na kuwa na tija kwa jamii.
 
Msimamizi na Mtaalam  wa Misitu wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Alex Njahani akiwaeleza waandishi wa habari waliotembele kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, kwanini wameamua kununua mashine ya kuchakata mbao kwenye vijiji vyenye Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
 
Mashine ya kisasa kuchakata mbao inayotumika kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
 
 
NA SULEIMAN MSUYA, TUNDURU
 

KATIKA kuhakikisha mazao ya misitu yanaongezeka thamani Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao wa Misitu (FORVAC) imenunua mashine za kisasa za kuchakata mazao ya misitu zinazogharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

Mashine hizo zitapelekwa kwenye vijiji vilivyopo kwenye wilaya zinazotekeleza miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) inayofadhiliwa na FORVAC.

FORVAC inatekeleza program hiyo kupitia Idara ya Misitu na Nyuki chini ya ufadhili wa Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland.

Program hiyo imejikita katika kuendana na sera na sheria ya misitu ambayo inataka jamii inanufaika kiuchumi, kijamii na maendeleo kupitia misitu inayowazunguka.

Matamanio ya FORVAC kuongeza thamani ya mazao ya misitu pia yanaungwa mkono na taasisi zingine kama Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyapori Duniani (WWF), Serikali na wengine.

Akizungumzia uamuzi wa kununua mashine hizo za kisasa za kuchakata mbao, Msimamizi na Mtaalam wa Misitu wa FORVAC, Alex Njahani amesema kumekuwepo na upotevu wa mazao ya misitu hasa mbao hivyo ni imani yao wataweza kuokoa.

Amesema kwa mwaka huu wamenunua mashine mbili zinazogharimu zaidi ya shilingi milioni 200 ambazo zitapelekwa katika mkoa wa Lindi na Ruvuma.

"Sisi tuna kongani tatu ambazo zinahusisha mikoa ya Tanga, Ruvuma na Lindi hivyo kwa sasa tumenunua mashine mbili ambazo zitakazotumika Ruangwa, Liwale, Nachingwea mkoani Lindi.

Pia mashine nyingine itatumika katika wilaya ya Namtumbo na Songea  mkoani Ruvuma na tumenunua mashine ya kukausha mbao matarajio yetu ni kuongeza thamani ya mazao ya misitu ya jamii ili vijiji vinufaike," amesema.

Njahani ametaja wilaya zingine ambazo zipo katika program hiyo ni Nyasa, Mbinga, Tunduru, Kilindi, Handeni, Mpwapwa na Kiteto.

Kwa upande wake Mtaribu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amesema matarajio yao ni kuona mnyororo wa thamani unoongezeka.

Msoffe amesema mashine hiyo itachochea kupunguza upotevu wa hekta 469,000 kwa mwaka kutokana na kuvuna bila kufuata utaratibu.

"FORVAC inatekeleza lengo la Serikali kuongeza viwanda kwani hakuna shaka kuwa mashine hiyo inatoa ajira kuanzia vijijini," amesema.

Amesema iwapo teknolojia hiyo ya kutumia mashine za kisasa itasambaa nchini kote mazao ya misitu yataongezeka thamani na upotevu wa mbao kupungua kwa asilimia nyingi.

Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema mashine hiyo ya kisasa itasaidia kuondoa misumeno ya mnyororo maarufu (Chensoo).

Mutunda amesema mashine inayotembea itawezesha kupatikana kwa mbao nzuri ambazo hazitahitaji umaliziaji mkubwa kama zamani.

"Mbao ya mashine ya kisasa inayotembea ni bora kuliko hizi zilizochanwa kwa Chensoo tunaamini zikisambaa nchini kote bidhaa za mbao zitaongezeka thamani," amesema.

Naye Bwana Miti katika Kijiji cha Sautimoja wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, Yusuph Kiangio, amesema mashine ya kisasa ya kuchakata mbao inazalisha mbao nyingi kwa muda mchache na bora.

"Mbao tunazozalisha kwa mashine ya kisasa zinauzika kirahisi, lakini pia inaokoa upotevu wa mbao kwa asilimia 63 na matarajio yao ni kupata asilimia 80 ya mbao kwa gogo moja.

Ila pia asilimia 20 itakayobakia ambayo ni mabanzi, mbao fupifupi na unga ambao tunafikiria kuufanya mkaa," amesema.

Kiangio amesema katika wilaya Kilwa na Tunduru ambazo MCDI inafanya kazi wameweza kuongeza mapato kutoka shilingi milioni 26 kwa kuuza magogo lakini kupitia mashine hizo wamekusanya zaidi shilingi milioni 125.

"Hapa Sautimoja tumeingiza shilingi milioni 85 kutoka shilingi milioni 40 huku bei ya mashine ikigharimu shilingi milioni 75,"amesema.

Aidha amesema mashine hii inaweza kuzalisha mbao 250 kwa siku kutoka mbao 25 kwa siku hivyo anashauri mashine hizo zitumike kwa kuwa zina gharama ndogo kuinendesha na rasilimali watu wachache.

Mtendaji wa kijiji cha Sautimoja Philemon Dastan amesema mashine hiyo pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya misitu pia imesaidia kupatikana kwa ajira kijijini hapo.

Dastan amesema USMJ imechochea uhifadhi kuongezeka kwenye msitu wa Chihuruka kwa kuwa kila mwanakijiji ananufaika kupitia msitu huo kwa huduma za jamii, uchumi na uhifadhi.

No comments:

Post a Comment

Pages