Bwana Miti, Yusuph Kiangio, akieleza waandishi wa habari waliotembelea
kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kupitia uratibu wa
FORVAC, kujifunza namna mazao ya misitu yanavyoweza kuongezwa thamani na
kuwa na tija kwa jamii.
Msimamizi na Mtaalam wa Misitu wa Program ya Mnyororo
wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Alex Njahani akiwaeleza
waandishi wa habari waliotembele kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru
mkoani Ruvuma, kwanini wameamua kununua mashine ya kuchakata mbao kwenye
vijiji vyenye Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
Mashine ya kisasa kuchakata mbao inayotumika kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
NA SULEIMAN MSUYA, TUNDURU
KATIKA
kuhakikisha mazao ya misitu yanaongezeka thamani Program ya Mnyororo wa
Thamani wa Mazao wa Misitu (FORVAC) imenunua mashine za kisasa za
kuchakata mazao ya misitu zinazogharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Mashine
hizo zitapelekwa kwenye vijiji vilivyopo kwenye wilaya zinazotekeleza
miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) inayofadhiliwa
na FORVAC.
FORVAC
inatekeleza program hiyo kupitia Idara ya Misitu na Nyuki chini ya
ufadhili wa Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland.
Program
hiyo imejikita katika kuendana na sera na sheria ya misitu ambayo
inataka jamii inanufaika kiuchumi, kijamii na maendeleo kupitia misitu
inayowazunguka.
Matamanio
ya FORVAC kuongeza thamani ya mazao ya misitu pia yanaungwa mkono na
taasisi zingine kama Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
(TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika
la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa
Mazingira na Wanyapori Duniani (WWF), Serikali na wengine.
Akizungumzia
uamuzi wa kununua mashine hizo za kisasa za kuchakata mbao, Msimamizi
na Mtaalam wa Misitu wa FORVAC, Alex Njahani amesema kumekuwepo na
upotevu wa mazao ya misitu hasa mbao hivyo ni imani yao wataweza kuokoa.
Amesema
kwa mwaka huu wamenunua mashine mbili zinazogharimu zaidi ya shilingi
milioni 200 ambazo zitapelekwa katika mkoa wa Lindi na Ruvuma.
"Sisi
tuna kongani tatu ambazo zinahusisha mikoa ya Tanga, Ruvuma na Lindi
hivyo kwa sasa tumenunua mashine mbili ambazo zitakazotumika Ruangwa,
Liwale, Nachingwea mkoani Lindi.
Pia
mashine nyingine itatumika katika wilaya ya Namtumbo na Songea mkoani
Ruvuma na tumenunua mashine ya kukausha mbao matarajio yetu ni kuongeza
thamani ya mazao ya misitu ya jamii ili vijiji vinufaike," amesema.
Njahani ametaja wilaya zingine ambazo zipo katika program hiyo ni Nyasa, Mbinga, Tunduru, Kilindi, Handeni, Mpwapwa na Kiteto.
Kwa upande wake Mtaribu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amesema matarajio yao ni kuona mnyororo wa thamani unoongezeka.
Msoffe amesema mashine hiyo itachochea kupunguza upotevu wa hekta 469,000 kwa mwaka kutokana na kuvuna bila kufuata utaratibu.
"FORVAC
inatekeleza lengo la Serikali kuongeza viwanda kwani hakuna shaka kuwa
mashine hiyo inatoa ajira kuanzia vijijini," amesema.
Amesema
iwapo teknolojia hiyo ya kutumia mashine za kisasa itasambaa nchini
kote mazao ya misitu yataongezeka thamani na upotevu wa mbao kupungua
kwa asilimia nyingi.
Mratibu
wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema mashine hiyo ya
kisasa itasaidia kuondoa misumeno ya mnyororo maarufu (Chensoo).
Mutunda amesema mashine inayotembea itawezesha kupatikana kwa mbao nzuri ambazo hazitahitaji umaliziaji mkubwa kama zamani.
"Mbao
ya mashine ya kisasa inayotembea ni bora kuliko hizi zilizochanwa kwa
Chensoo tunaamini zikisambaa nchini kote bidhaa za mbao zitaongezeka
thamani," amesema.
Naye
Bwana Miti katika Kijiji cha Sautimoja wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,
Yusuph Kiangio, amesema mashine ya kisasa ya kuchakata mbao inazalisha
mbao nyingi kwa muda mchache na bora.
"Mbao
tunazozalisha kwa mashine ya kisasa zinauzika kirahisi, lakini pia
inaokoa upotevu wa mbao kwa asilimia 63 na matarajio yao ni kupata
asilimia 80 ya mbao kwa gogo moja.
Ila pia asilimia 20 itakayobakia ambayo ni mabanzi, mbao fupifupi na unga ambao tunafikiria kuufanya mkaa," amesema.
Kiangio
amesema katika wilaya Kilwa na Tunduru ambazo MCDI inafanya kazi
wameweza kuongeza mapato kutoka shilingi milioni 26 kwa kuuza magogo
lakini kupitia mashine hizo wamekusanya zaidi shilingi milioni 125.
"Hapa
Sautimoja tumeingiza shilingi milioni 85 kutoka shilingi milioni 40
huku bei ya mashine ikigharimu shilingi milioni 75,"amesema.
Aidha
amesema mashine hii inaweza kuzalisha mbao 250 kwa siku kutoka mbao 25
kwa siku hivyo anashauri mashine hizo zitumike kwa kuwa zina gharama
ndogo kuinendesha na rasilimali watu wachache.
Mtendaji
wa kijiji cha Sautimoja Philemon Dastan amesema mashine hiyo pamoja na
kuongeza thamani ya mazao ya misitu pia imesaidia kupatikana kwa ajira
kijijini hapo.
Dastan
amesema USMJ imechochea uhifadhi kuongezeka kwenye msitu wa Chihuruka
kwa kuwa kila mwanakijiji ananufaika kupitia msitu huo kwa huduma za
jamii, uchumi na uhifadhi.
No comments:
Post a Comment