HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 15, 2021

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR HAWATAKA WAZANIZAR KUWA NA MSHIKAMANO

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akitoa salamu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilika ka Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Amani.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alisema mshikamano wa pamoja kati ya Viongozi, Waumini wa Dini pamoja na Wananchi mahali popote walipo ndio njia ya msingi itakayorahisisha kulijenga Taifa imara.

Akitoa salamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa pembezoni mwa Uwanja wa Michezo wa Aman Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwakumbusha Waumini hao kwamba kila Mwananchi ana nafasi yake katika kujenga Nchi si lazima ame Mtumishi wa Umma.

Mheshimiwa Hemed alisema hatua hiyo ya mshikamano wa pamoja ambayo Serikali Kuu tayari imeshaonyesha muelekeo wa mfano katika ngazi ya Uongozi itawezekana na kufanikiwa ipasavyo endapo jamii nzima itaendelea kuhamasishana katika usimamizi wa masuala ya Amani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba yapo Mataifa Duniani baadhi ya Waumini wake wenye Imani ya Uislamu wameshindwa kutekeleza Ibada ya sala ya Ijumaa kutokana na machafuko yaliyosababishwa na Itikadi za Kisiasa au Kidini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alihimiza umuhimu wa Waumini na Wananchi kuendelea kuzingatia Uadilifu katika matendo yao kama ulivyosisitizwa katika Hotuba ya Ijumaa ili kuleta utulivu wa moyo ndani ya vifua vya Watu katika maeneo yao.

Alieleza kwamba changamoto za Kijamii kwa asilimia kubwa zinaweza kuondoka au kupungua kabisa kama ulafi wa baadhi ya Watu hasa katika masuala ya Fedha utadhibitiwa jambo ambalo hivi sasa Serikali Kuu imekuwa ikiendelea kuchukuwa hatua za kukabiliana nalo.

Aliwahimiza Wananchi pamoja na Waumini wa Dini kuvumilia kipindi hichi ambacho Uongozi wa Serikali umekuwa ukichukuwa hatua hizo zinazoonyesha mwanga kwa baadhi ya Washirika wa Maendeleo ndani na Nje ya Nchi kwa kutaka kuungwa mkono jitihada hizo za Serikali.

Mapema akitoa Hotuba ya sala ya Ijumaa Mwanachuoni Maarufu Ustaadh Rajab Mohamed Shaali aliwakumbusha Waumini wa Dini ya Kiislamu kuhakikisha kwamba suala la uadilifu linapewa nafasi yake ili Jamii Mitaani iendelee kuishi kwa upendo.

Ustaadhi Rajab alisema Utamaduni wa baadhi ya Watu kupenda kujilimbikizia Mali za dhulma sio malengo ya uwepo  wao Duniani katika kufanya ibada bali unazidisha chuki na uhasama miongoni mwa Jamii  katika ngazi ya ufukara, umasikini na utajiri.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikutana na Uongozi wa Jumuiya Wazee Wastaafu Zanzibar ili kubadilishana mawazo  mazungumzo yaliyofanyika Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Mh. Hemed alisema Serikali itaendelea kuwaheshimu Wazee wote Nchini kwa kuwapatia huduma stahiki ikitimiza wajibu wake ili waendelee kupata utulivu wa maisha yao  huku ikizingatia kuwa mchango wao ndio uliosababisha Taifa hili kufikia hatua kubwa ya maendeleo.

Mheshimiwa Hemed alisema Serikali inaelewa changamoto na matatizo mengi yanayowakumba Wazee katika maisha yao ya kawaida na ndio maana hulazimika kufanya utafiti wa kutosha unaosaidia kupata muelekeo wa kuwajengea mazingira rafiki.

Alisema katika hatua ya kuyakidhi mahitaji yao ya lazima Wazee , Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote imekuwa na mfumo wa kuangalia mazingira ya hali ya uchumi inavyozunguuka na pale inaporuhusu haioni tatizo nguvu hizo kuzielekeza kwa Wazee hao waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa wakati wa utumishi wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akitoa ushauri kwa Viongozi hao wa Jumuiya Wastaafu alisema ipo haja ya kuendelea kutoa Elimu kwa Watumishi wanaokaribia kustaafu ili pale watakapofikia muda waendelee na maisha yao bila ya wasi wasi wowote.

Mheshimiwa Hemed alisema Watumishi wengi wanapopata barua ya kumaliza muda wao wa Utumishi huchanganyikiwa huku wakijisahau kwamba wapo Vijana wengi waliomaliza masomo yao ambao wanahitaji kuziba nafasi zao  kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma Serikalini.

Mapema Katibu wa Jumiya ya Wastaafu Zanzibar Bibi Salama Kombo Ahmed alisema Wazee wengi Nchini wamefuharia uwepo wa Sheria iliyowashirikisha moja kwa moja wazee wenyewe ingawa bado haijawa na Kanuni zake.

Bibi Salama alisema Jumuiya ya Wastaafu Zanzibar iliyoasisiwa mnamo Mwaka 2001 pamoja na mambo mengine inaendesha mradi wa kuwaelimisha Wazee kupitia Mabaraza yao ya shehia Unguja na Pemba ili kutambua kwamba Miaka 60 ya ustaafu sio mwisho wa Maisha yao.

Katibu wa Jumuiya hiyo ya Wastaafu Zanzibar kwa niaba ya wanajumuiya wameishukuru Serikali Kuu kwa uamuzi wake wa kuendelea kuwapatia Pencheni kila mwezi sambamba na ile ya Shilingi 20,000 kwa Wazee wa Zaidi ya Miaka Sabini.

 Hata hivyo Bibi Salama alisema zipo baadhi ya changamoto zinazoendelea kuwasumbua Wazee akizitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa Kitambulisho ili kuwapa uangalizi wa huduma za Afya na Hospitali pamoja na Uwakilishi wa Wazee katika Mabaraza ya Kutunga Sheria.

No comments:

Post a Comment

Pages