TEKNOLOJIA
ya uchakataji wa mazao wa misitu hasa magogo imetajwa kuongeza thamani
ya mazao hayo kwa asilimia 60 huku mapato yakiongezeka hadi kufikia
asilimia 100.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpingo na Maendeleo
(MCDI), Makala Jasper (pichani) wakati akizungumza mbele ya wadau wa sekta ya
misitu, mazingira na uihifadhi waliokutana jijini Dodoma.
Amesema
MCDI imekuwa ikishirikiana na taasisi zingine kama Shirika la Kuhifadhi
Misitu Tanzania (TFCG), Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya
Misitu (FORVAC) kuhamasisha uongezaji wa thamani mazao ya misitu.
Makala
amesema kwa muda mwingi uvunaji mazao ya misitu hususani magogo umekuwa
ukipoteza mbao nyingi ila ujio wa teknolojia mpya imesaidia kuchochea
ongezeko la mapato.
Amesema
MCDI kwa kushirikiana na wadau wengine wameweza kuwesha vijiji venye
misitu ya asili kupata mashine za kisasa ambazo zinaongeza thamani mazao
hayo kwa asilimia 60.
Mkurugenzi
huyo amesema ujio wa teknolojia umesaidia vijiji kuuza mbao na sio
magogo kama zamani ambapo walivuna kwa kutumia Sawmill.
"Kwa
sasa vijiji ambavyo vilikuwa vinauza magogo vimebadilika na vinauza
mbao zilichakatwa kwa teknolojia hivyo thamani ya mazao ya misitu hasa
mbao imeongezeka kwa asilimia 60.
Ila
kubwa zaidi ni mapato yameongezeka kati ya asilimia 60 hadi 100 jambo
ambalo linachochea usimamizi na ulinzi wa rasilimali misitu," amesema.
Makala amesema pia kupitia ujio wa teknolojia umewezesha ajira zisizo za moja kwa moja 200 na ajira za moja kwa moja 5.
"Lengo
la kuingiza teknolojia ni kuongeza thamani ya mazao ya misitu, mapato,
ajira na uhifadhi na yote yananyika kwa ufanisi," amesisitiza.
Kwa
upande wake Dk.Asha Salum kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema
ujio wa teknolojia umeongeza thamani na kuchochea maendeleo kwa
wanavijiji.
Dk.Salum
ambaye pia ni Balozi wa Kampeni ya Mama Misitu iliyoratibiwa na Mtandao
wa Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania (MJUMITA) amesema nguvu kubwa
ilekezwe kwenye teknolojia ili misitu iendelee kuwa salama na endelevu.
"Ushahidi
umeonesha uchakataji wa kutumia teknolojia unaongeza thamani kwa
asilimia 60, uhifadhi na mapato hivyo ni vema hamasa ikajikita huko ili
misitu iwe endelevu," amesema.
Mhadhiri
huyo mwandamizi amesema dhana ya kuongeza thamani mazao ya misitu
isambazwe kila eneo ambalo lina misitu ya asili ya vijiji.
Dk.Salum
amesema uendelevu wa misitu utarahisisha wanawake kutekeleza majukumu
yake kwa amani kwani atakuwa na uhakika wa kupata maji, nishati na
huduma nyingine muhimu.
Ameitaka
Serikali kuipa kipaumbele miradi ambayo inahusiana na Usimamizi
Shirikishi wa Mazao ya Misitu kwa kuwa imekuwa na matokeo chanya.
Mwenyekiti
wa Bodi ya MCDI na Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), John
Salehe amesema mafanikio ya mipango na mikakati ya kuifanya misitu kuwa
endelevu itafikiwa kwa wadau wote kuwa kitu kimoja.
"Usalama
na uendelevu wa rasilimali misitu ni lazima wadau wote yaani watunga
sheria, Sera, wasimamizi na waibua miradi kuwa kitu kimoja kwa kuangalia
Tanzania ijayo kinyume na hapo ni maumivu kwa wote," amesema.
No comments:
Post a Comment