NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) mkoani Dodoma imetoa mafunzo kwa watoa huduma wa afya kwa lengo la kupunguza matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba huku ikikumbushwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba.
Akizungumza katika mafunzo maalum juu ya matumizi ya dawa, Kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma Aziza Rajabu Mumba amesema lengo kubwa la kutoa mafunzo kama hayo ni kuhakikisha kupuguza madhara makubwa juu ya athari za dawa kwa watumiaji.
Amesema wamewapa elimu wataalamu hao ambao wako kwenye vituo vya Afya ili waweze kudhibiti madhara ya dawa na Vifaa Tiba yasitokee kwa watumiaji.
Aidha Kaimu katibu tawala huyo wa mkoa ametoa wito kwa mamlaka ya dawa na vifaa tiba[TMDA]kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.
Katika hatua nyingine amesema kwa sasa hali sio mbaya hasa kwenye eneo la madhara ambapo , mambo yamekuwa mazuri, kutokana na elimu kuendelea kutolewa kila wakati kwa jamii kuhusiana na utumiaji wa dawa na vifaa tiba katika afya ya mwanadamu.
Kwa upande wake kaimu meneja wa mamlaka ya dawa na vifaa tiba[TMDA] kanda ya kati Sonia Henry amesema mafunzo hayo dhima yake kubwa ni kuwakumbusha watoa huduma katika majukumu yao ili kuwa makini katika kutoa huduma inayostahili na kulinda afya ya jamii .
" Tumewapa mafunzo watumishi 30 wa sekta hii ya Afya kutoka Halmashauri zote za Dodoma lengo likiwa ni kuwajengea uwezo Ili waweze kutoa taarifa zitakazosaidia kupunguza madhara kwa wananchi pindi watumuapo dawa na Vifaa Tiba," amesema
Mamlaka ya dawa na vifaa tiba ni Taasisi ya serikali iliyopo chini ya wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto yenye jukumu la kudhibiti ubora,usalama na ufanisi wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi ili klinda Afya ya jamii.
No comments:
Post a Comment