Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jamii na Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Rahima Njaidi akiwasilisha mada mbele ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Tanzania.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Aloyce Kwezi (kulia), akichangia
kwenye warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mashirika ya TFCG, MJUMITA
na MCDI, mwingine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na
Mazingira David Kihenzile.
IMEBAINISHWA kuwa mahitaji ya ardhi kwa ajili ya mashamba ya kilimo yanachangia upotevu wa misitu kwa asilimia 80.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili
Tanzania (TFCG), Charles Meshack wakati akizungumza na wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano ambao ni wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara
na Mazingira na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Dodoma.
Amesema
kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na TFCG na taasisi
nyingine zimeonesha upotevu mkubwa wa misitu nchini unasababishwa na
kilimo hasa cha zao la mahindi.
Amesema
asilimia kubwa ya upotevu huo unatokea katika maeneo ambayo misitu yake
haina mfumo wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
Meshack
amesema utafiti unaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48
za misitu ambapo asilimia 47 ya misitu hiyo ipo katika ngazi ya kijiji
ambapo hekta milioni 2 pekee ndio ipo kwenye USMJ.
"Misitu
nchini inapotea sana hapa nchini hasa katika vijiji ambao havina USMJ
kwani kati ya hekta milioni 22 ya misitu hiyo ni hekta milioni 2 pekee
ipo kwenye USMJ hivyo hekta milioni 20 zipo huru hali ambayo inachangia
kilimo kuchochea upotevu kwa asilimia 80," amesema.
Meshack
amesema iwapo hakutakuwa na jitihada za kuilinda, kuitunza na
kuindeleza baada ya miaka 40 ijayo misitu itakuwa imekwisha.
Mkurugenzi huyo amesema mfumo wa USMJ umeweza kuchochea uhifadhi, ulinzi na utunzaji huku maendeleo yakipatikana.
"Faida
ya USMJ ni kubwa sana kuliko kujikita kwenye kilimo hivyo ni jukumu la
wadau wote kushirikiana kunusuru misitu inateketea.
Ushahidi
upo kuwa USMJ umeweza kuongeza thamani mazoa ya misitu nchini, lakini
pia miradi ya elimu, afya, maji, uhifadhi ikifanikishwa kwa uendelevu,"
amesema.
Meshack amesema
iwapo Serikali inahitaji kupunguza hekta 469,000 zinazopotea kwa mwaka
ni vema iwekeze kwenye USMJ kwa kuwa imeonesha mafanikio mazuri.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI),
Jasper Makala amesema kupitia USMJ wameweza kuilinda misitu na kukuza
kipato kwa wananchi wanaozungukwa na misitu.
Amesema
MCDI, imekuwa ikijijita kutoa elimu namna ya kukabiliana na moto,
kuunganisha na masoko ya mazoa ya misitu na uhifadhi wa mazingira na
misitu.
"Kupitia uwepo wetu tumewezesha mapato kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 baada ya kuachana na kuuza magogo.
Pia tumewezesha kuongeza ajira kwa wanavijiji wengi jambo ambalo limechochea uhifadhi zaidi," amesema.
Makala
amesema MCDI kwa kushirikiana wadau mbalimbali kama Program ya Kuongeza
Mnyororo wa Thamani (FORVAC) na WWF wameweza kutoa mashine nne za
Norwood ambazo zinaongeza tahamani ya mazoa ya misitu kwa asilimia 60.
"Pia tumenunua mashine ya kukausha mbao hali ambayo imezidi kuongeza kuongeza thamani kwa mazao ya misitu hasa mbao," amesema.
Makala amesema kwa ujumla wanachofanya kwenye vijiji kwa sasa ni kuongeza wingi wa mazao na mapato.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania
(MJUMITA), Rahima Njaidi amesema USMJ umegawanyika katika maeneo wawili
muhimu ambayo ni vijiji na halmashauri kusimamia misitu na USMJ.
Njaidi amesema MJUMITA na wadau wengine walikuja na USMJ ili kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa salama.
"Tumekuwa
tukisimamia uhifadhi, utunzaji na uendelevu wa misitu kwa kuafuata
Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, Sera ya misitu ya mwaka 1998 pamoja na
kanuni zake kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha watu wote na nchi,"
amesema.
Mkurugenzi huyo amesema USMJ ni nyenzo muhimu kwenye ulinzi wa misitu nchini.
Aidha, amesema wametambua umuhimu wa wananchi katika ulinzi wa misitu iwapo dhana ya USMJ itapewa nafasi kwa ngumu kubwa.
Naye Mbunge wa Lulindi Issa Mchungahela amesema USMJ inapaswa kusambaa nchini kote kwa kuwa inagusa maisha ya wananchi.
Mchungahela amesema miradi hiyo ni moja ya maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge
wa Kinondoni Askofu Josephat Gwajima amesema misitu ni muhimu kwa
maisha ya binadamu hivyo inapaswa kutunzwa kwa nguvu zote.
No comments:
Post a Comment