Mbunge wa jimbo la Lulindi Issa Mchungahela akichangia kwenye semina ya siku moja kwa wabunge wajumbe wa Kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Mashirika ya TFCG, MJUMITA na MCDI iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa bungeni Dodoma.
Mbunge wa jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Dk. Charles Kimei akichangia kwenye semina ya siku moja kwa wabunge wajumbe wa Kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Mashirika ya TFCG, MJUMITA na MCDI iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa bungeni Dodoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack akijibu baadhi ya maswali ya wabunge ambao ni wajumbe
wa Kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara
na Mazingira walioshiriki semina iliyoandaliwa na Mashirika ya TFCG,
MJUMITA na MCDI iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa bungeni
Dodoma.
Na Suleiman Msuya
KATIKA
kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa endelevu Shirika la Kuhifadhi
Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii Usimamizi wa Misitu
Tanzania (MJUMITA) na Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI) wametoa
maombi saba kwa Bunge.
Maombi
hayo yamewasilishwa bungeni na Meneja Mradi wa Kuleta Mageuzi katika
Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), Charles Leonard kwa niaba ya taasisi hizo
wakati wakitoa mafunzo kwa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na
Mazingira na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Leonard
amesema pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana kupitia Usimamizi
Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) wanaomba mambo saba hayo yafanyike
kwa maslahi ya nchi.
Amesema
Tanzania ina hekta za misitu milioni 48.1 ambapo hekta milioni 22.1 ipo
kwenye vijiji na hekta milioni 2 ndio inasimamiwa na vijiji jambo
ambalo ni hatari kwa miaka 50 ijayo kwani misitu inaweza kutoweka
nchini.
Meneja huyo
alitaja ombi la kwanza kuwa kuangalia sera, sheria na kanuni na taratibu
zinazokinzana kwenye sekta ya ardhi, misitu, kilimo, nishati na maji
baadhi ya vipengele vinakwamisha usimamizi wa rasilimali misitu.
Amesema wanaamini wabunge wanaweza kusaidia kwenye kuangalia namna ya kurekebisha vipengele hivyo.
"Ombi la pili tunaomba wabunge mtoe kipaumbele kwenye kuendeleza na kuhamasisha uwekezaji katika usimamizi wa misitu ya jamii.
Pia
kuhamasisha uvunaji, usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za
misitu ya asili katika ardhi za vijiji, hali itakayochangia ongezeko la
thamani la mazao ya misitu na kupeleka kwa vijiji vingine vyenye
misitu," amesema.
Meneja
huyo amesema kupitia msukumo wa wabunge kwenye eneo hili wataweza
kupunguza upotevu wa misitu ambapo kwa mwaka zaidi ya hekta 469,000
zinapotea.
Amesema USMJ
inapunguzia kazi Serikali kwa kuwa fedha zinazopatikana zinatekeleza
miradi ya maendeleo ya alimu, afya, maji na mingine mingi.
Leonard
amesema ombi lingine ni kuwataka wabunge waunge mkono shughuli za USMJ
kwa kuhamasisha vijiji vyenye misitu ya asili kuhifadhi, kutunza na
kuendeleza kwa njia endelevu.
Meneja
huyo alitaja ombi lingine kuwa ni wabunge waendelee kuishauri Serikali
kuhakikisha sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 inayowapa mamlaka
vijiji kumiliki, kuhifadhi na kusimamia misitu inatekelezwa bila
vikwazo.
"Kuishauri
Serikali kuhusu haki na wajibu kupitia sheria zilizopo ili wananchi
waweze kunufaika vizuri na rasilimali misitu zilizopo kwenye vijiji.
Vilevile
tunaomba muendelee kuishauri Serikali kuhusu kanuni za misitu
zilizotoka mwaka 2019 kwenye tangazo la Serikali namba 417 ambazo
zinaonesha kurudisha nyuma USMJ," amesema.
Meneja
alitaja ombi lingine wanalopeleka kwa wabunge ni kuwa tayari kutembelea
maeneo ambayo miradi imetekelezwa ili kujionea kinachoendelea ili
waweze kuthibitisha kwa vitendo yanayoelezwa.
Leonard
amesema TFCG, MJUMITA na MCDI wameamua kupigania rasilimali misitu
nchini ili kuhakikisha inanufaisha jamii hivyo wanaamini watunga sheria,
sera na kanuni wakiwa kitu kimoja misitu inatakuwa salama na endelevu.
Akizungumza
baada ya ombi hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii
Aloyce Kwezi amesema wamechukua maombi yote yaliyowasili na taasisi hizo
na kuahidi kufanyia kazi.
Kwezi
amesema TFCG, MJUMITA na MCDI wanachokifanya ni cha kuigwa na wadau
wengine ili kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa salama na endelevu.
"Ninapenda
kuahidi kuwa sisi kama kamati tumechukua maombi yenu kwani yamejikita
kulinda rasilimali misitu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi,"
amesema.
Amesema
changamoto zilizopo watazifanyia kazi na kuomba TFCG, MJUMITA na MCDI
kuendelea kushirikiana nao ili kuendeleza rasilimali misitu.
Kwa
upande wake Mbunge wa Lulindi Issa Mchungahela amesema wananchi wapo
tayari kuhifadhi mazingira ila changamoto ya kipato ni tatizo.
Aidha, amesema pamoja na manufaa ambayo yametajwa ni mengi ila inaonekena elimu bado haijafika kwa kiwango cha kuridhisha.
Mjumbe
huyo wa Kamati ya Viwada, Biashara na ?Mazingira amesema jamii
ikinapaswa kutambua faida za uhifadhi ya misitu ili kuweza kuachia
urithi kwa vizazi vijavyo.
Mbunge
wa Vunjo, Dk.Charles Kimei amesema jamii inaweza kulinda rasilimali
misitu iwapo itanufaika nayo kiuchumi, maendeleo na jamii.
"Nadhani
kuna juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha dhana ya ushirikishi
inatimia kwani wanavijiji wengi waliopo pembezoni mwa misitu au hifadhi
hawanufaiki nayo," amesema.
Mbunge
wa Kuteuliwa, Riziki Lulida amesema mafanikio yaliyopatikana kwenye
misitu ya vijiji kupitia mashirika hayo yanapaswa kusambaa kila kona ya
nchi ili kulinda misitu yote.
Amesema
rasilimali misitu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi iwapo
itatumika kwa kufuata sheria, sera na kanuni zilizopo.
No comments:
Post a Comment