June 14, 2021

Viongozi wa Dini waiomba Serikali kuharakisha usikilizaji kesi viongozi waislamu, wakemea matusi kwa viongozi wastaafu

 


Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zubeiry, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao kilichowakutanisha viongozi wa dini kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kujenga undugu kati ya waamini wa dini zote.



Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Viongozi wa Dini nchini wameiomba Serikali na Mamlaka husika kuharakisha mchakato wa ushughulikiaji na usikilizaji wa kesi za viongozi wa dini ya Kiislamu walioko magerezani kwa miaka mingi ili haki itendeke na kwamba watakaokutwa na hatia wachukuliwe hatua za kisheria.

Ombi hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zubeiry baada ya Kikao kilichowakutanisha viongozi hao kumaliza kikao kilichojadili masuala mbalimbali ikiwemo kujenga undugu kati ya waamini wa dini zote, mustakabali wa taifa na kuhamasisha kudumisha amani, umoja na mshikamano.

Amesema kuwa anaiomba mahakama na MKurugenzi wa Mashtaka na Serikali kwa ujumla kuharakisha usikilizaji wa kesi wa viongozi wa dini kwani wameshikiliwa kwa muda mrefu bila kujua hatma zao.

" Tunaiomba mahakama, DPP na Serikali itatue kesi zikilizwe kwa haraka watakaokutwa na makosa wachukuliwe hatua za kisheria," amesema Mufti Bin Zubeiry.

Amebainisha kuwa viongozi wa dini wanaoshikiliwa na vyombo vya sheria watendewe haki kwa kusikilizwa kesi zao kwani kuwaweka ndani muda mrefu ni kuwanyima haki zao za msingi.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri  Tanzania, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa  amesema ili kukakikisha linakuwa na kizazi chenye maadili mema yatakayochangia maendeleo ya taifa na kwamba kila mzazi anatakiwa kutimiza wajibu wake kwa kuwapa watoto wao malezi mema.

Askofu Dkt. Malasusa amesema kila dini inassisitiza na kuhimiza kila mwenye mtoto kutoa malezi bora yanayochangia ustawi wa jamii imara na taifa lenye maendeleo.

Amewasisitiza na kuwahimiza viongozi wa madhehebu yote kuendelea kuwahamasisha waamini wao kudumisha umoja, amani na mshikamano uliopo.

Mufti huyo amesema hadi sasa Baraza la Waislamu Tanzania halijapata taarifa sahihi za watu wanaotaka kwenda Hijja kutoka Wizara ya Hijja ya Saudia Arabia na Ubalozi wa nchi hiyo nchini hivyo zikilifikia watatoa taarifa.

Naye Askofu wa Kanisa la Menonite Tanzania, Dayosisi ya Masahariki na Pwani, Nelson Kisare amesema waamini wa dini wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuilinda nchi hata baada ya kifo cha Rais Dkt. John Magufuli hivyo ni kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni jambo jema na la kihistoria kwa taifa.

Aidha, amesema jamii inatakiwa kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto kwani ni dhambi na kusisitiza elimu kutolewa kwa wahusika ili watambue madhara ya kukiuka haki za kundi hilo.

Askofu Mkuu wa Elimu ya Pentekoste Peter Konki amekemea vitendo viovu ya kudhihaki Marais wastaafu na aliyeoko madarakani kwa lugha ya matusi kwani kufanya hivyo kuwakosea kulikosea taifa kwa ujumla.

Ameiomba Serikali kushughulikia  suala la mfumuko wa bei kwani linaathiri maisha ya watu wa hali ya chini kwani wengi hushindwa kumudu gharama za maisha.


No comments:

Post a Comment

Pages