Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, amewataka Mawakili wa Serikali Nchini kuendelea kujielimisha kila siku kutokana na kukua kwa taaluma ya Sheria Ulimwenguni kulingana na umuhimu wa kazi yao wanayoifanya ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Profesa Kilangi ametoa wito huo leo Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa Mawakili wa Serikali yenye lengo la kuwaongezea uwezo katika stadi za uendeshaji madai ya usuluhishi kwa kuwapa ujuzi ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu na yatasaidia kuwanoa Mawakili hao ili kuendana na mabadiliko ya taaluma ya Sheria ambayo yamekuwa yanatokea kila siku ulimwenguni.
Sambamba na hilo amesema Mafunzo hayo yataongeza uwezo na weledi katika suala zima la usuluhishi la madai mbalimbali huku akiitaka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kushirikiana na Taasisi mbalimbali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ofisi hiyo ikiwemo uhaba wa mawakili wa Serikali.
Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali,Gabriel Malata amesema ofisi hiyo ilipewa jukumu lakuendesha madai ya kesi ndani nan je ya nchi na kupitia mafunzo hayo yanaenda kuwaweka katika mtazamo mmoja wa uendeshaji wa mashauri kwaniaba ya Serikali na Taasisi zake huku akibainisha mafanikio na changamoto mbalimbali.
No comments:
Post a Comment