Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
Wanawake waliopo uongozini katika nafasi mbalimbali nchini, wametakiwa kuwawezesha wanawake wengine ili kujitokeza katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika kufikia ajenda ya 50/50 ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoainishwa katika malengo ya millennia ikiwa ni lengo namba 5.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na mbunge wa viti maalum Agness Hokololo ambaye ni katibu wa wabunge wanawake katika Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania wakati wa majadiliano baina ya Wabunge wanawake na Chama cha wanahabari wanawake nchini Tamwa katika kuangalia changamoto zinazokabiri ushiriki wa wanawake katika siasa na nafasi za maamuzi.
Pia amevitaka vyama kutimiza wajibu wake kwa kundi la wanawake na tume ya uchaguzi iweke katika kanuni za uchaguzi eneo la wanawake kuchukuliwa kwa umuhimu katika teuzi za vyama.
Mbunge wa viti maalum Kundi la Vijana Mwasi Kamani amesema pamoja na jitihada zote ni lazima kuangaliwa utayari wa wanawake kushiriki kwenye chaguzi na uwezo katika nafasi husika huku mbunge wa mafinga Cosato Chumi ambaye ni kinara kwenye mjadala akishauri maandalizi kwa kundi la wanawake kuwania nafasi yaanze ngazi za chini ili kufikia 50/50.
Naye mbunge wa jimbo la Ngasi kaskazini Aida Kenani Ametaka kuwepo na uwazi kwenye michakato ya uchaguzi katika vyama ili ushiriki wa wanawake ujulikane tofauti na hali ilivyo sasa.
Mkutano huo umeandaliwa na Tamwa kwa kushirikiana kwa kushirikiana na kituo cha Usuluhishi (CRC) kilichopo Tamwa pamoja na Young & alive initiative (YAI) lengo kuu ikiwa ni kuwashirikisha wabunge wanawake ili kuziondoa changamoto zilizopo katika jamii ambazo zinakwamisha nafasi ya mwanamke kushiriki katika masuala ya siasa na nafasi za juu za maamuzi katika taifa.
No comments:
Post a Comment