Baraka Vicent akitengeneza mikanda ya viatu.
Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Mzumbe kimetekeleza kwa vitendo kauli mbiu yake ya ‘Jifunze kwa Maendeleo ya Watu’ baada ya kuwatembelea wajasiriamali wa Soko la Machinga Complex jijini Dar es Salaam na kuwafundisha namna bora ya kuboresha biashara zao.
Zoezi hilo limefanyika leo sokoni hapo ambapo wanafuzni wanaosomea Uzamili wa Utawala wa Biashara na Uongozi wa Mashirika ama ‘MBA’ Baada ya kufundishwa na Prof Ngowi wametumia walichojifunza kufundisha wajasiriamali wa Machinga Complex kuhusu ubunifu katika biashara.
Wakizungumza na Habari Mseto Wanafunzi hao wamesema miongoni mwa changamoto walizozibaini kwa wajasiriamali ni pamoja na ukosefu wa vifaa, uhaba wa wateja lakini pia eneo la biashara sio rafiki kwa wateja.
“Asilimia kubwa ya wafanyabiara wanapitia changamoto ya ukosefu wa vifaa, kupungua kwa wateja, eneo la kufanyia biashara pia sio rafiki kwa sababu wako wengi ni kama wamebanana lakini pia hata uzalishaji wanafanyia hapohapo wateja wanapita hapohapo, yaani kila kitu ni hapohapo.
“Pia changamoto nyingine ambayo wengi wanakutana nayo ni suala la mtaji, wana mitaji midogo kwaiyo wanashindwa kukuza biashara zao. Kutokana na hayo tumeweza kuwashauri, kwa upande wa kupungua kwa wateja wanapaswa kufanya biashara ya mtandao ili kupanua soko lao na kuwafikia wateja wengi zaidi kuendana na dunia ya sasa ya Teknolojia.”alisema Mboni Rashid, Mwanafunzi Mzumbe.
“Lakini pia tumewashauri kuongeza ubunifu ili kutofautisha bidhaa zao kuweza kumshawishi mteja kwani kuwa na bidhaa za aina moja kunampunguzia mlaji radha ya chakula. Pamoja na hayo zoezi hili kwangu limekuwana mafanikio makubwa kiasi ambacho tumefikia lengo.”alisema Mboni.
Naye Baraka Matage amesea ziara hiyo imewafundisha mengi kutoka kwa wajasiriamali hao wa viatu ikiwa ni pamoja na jinsi wanavyofanya biashara yao.
“Pamoja na mengi ambayo tumejifunza lakini kuna changamoto kadhaa wa kadhaa ambazo wanakumbana nazo ikiwa ni pamoja na bei ya bidhaa hapa wanapaswa kutoiangalia Machinga Complex pekee bali wanapaswa kuyatazama masoko mengine nje ya hapa hasa katika maeneo ambayo watalii wanapatikana na watu wenye kipato cha juu.
“Kuhusu upungufu wa vifaa tumewashauri waweze kuuungana kwa kidogo walichonacho ili kuweza kunyanyuana lakini pia suala la mitaji wanapaswa kuwa na vikundu ambavyo vitawawezesha kupata mikopo katika mabenki. Pamoja na hayo nitoe wito kwa Sido iweze kuwatazama na kuwashika mkono ili waweze kupiga hatua zaidi.”aliongeza Baraka.
Kwa upande wa wajasiramali hao wamesema elimu waliyoipata imewafikia kwa wakati sahihi jambo ambalo litawaongezea kasi ya utendaji katika biashara zao, sambamba na hilo wametoa shukrani zao kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kuwakumbuka na kuwaasa kuwapelekea mafunzo ya mara kwa mara ili kuweza kupambana na chanagmoto mbalimbali kattika biashara zao.
“Kwanza nimefurahi sana kutembelewa na wageni kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, kazi kama yetu hii kutembelewa na wageni ni Baraka mojawapo ya kazi pia unapata mawazo mapya kutoka kwao.
“Mimi nimepata ushauri tofauti wa kuboresha kazi yangu kwa mfano kuwa na biashara ya mtandao amabyo itanisaidia kupata wateja kutoka nje ya Mkoa hata nje ya Nchi ikiwezekana ili biashara yangu iweze kutoka kwa wakati.
“Changamoto kubwa tuliyonayo hapa ni ukosefu wa vifaa, kukosa mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha kazi yetu kuendana na mabadiliko ya soko na uhitaji wa bidhaa sokoni.” Aliongeza Juma Masai, Mjasiriamali.
“Tumepata faida kubwa sana kwa elimu na mafunzo tuliyoyapata kutoka kwa ndugu zetu wa Mzumbe, nimegundua tunafanya makosa, ukiangalia tunatengenezea viatu hapa na kuviuza hapa jambo ambalo litakuwa linapunguza thamani ya bidhaa tunayoizalisha kwani mteja akija anaona kiatu jinsi kinatengenezwa naamini tunapaswa kutenganisha kiwanda na soko ili kuiongeea thamani biashara yetu.”alisema Willson Ayubu, Mjasiriamali.
Walichofanya wanafunzi ni sehemu ya zoezi la darasani lenye alama (marks) 10. Ikiwa ni njia bunifu ya kufundisha, kujifunza na kuwafikia wadau.
No comments:
Post a Comment