September 18, 2021

DC NGUVILA AKUTANA NA WAWAKILISHI WA WAZEE WILAYA YA MULEBA


Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila, amewaahidi wazee wa wilaya ya Muleba kuwa nao bega kwa bega katika kutatua changamoto zinazowakabili wakati alipokutana na wawakilishi wa  Umoja wa wazee wa wilaya ya Muleba unaoratibiwa na Shirika la Kwa Wazee Nshamba katika ukumbi wa Waisuka.


Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Toba Nguvila ameeleza kuwa uzee ni hazina hivyo katika utendaji kazi wake atashirikiana nao na kuwapa kipaumbele katika kutatua changamoto zinazowakabili.


Wakitoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee hao wameomba kuwa na uwakilishi mbungeni kwani ni kundi ambalo limesahaulika kuwa na msemaji katika mhimili huo. Naye Mhe. Nguvila amewaahidi wazee kuwa suala la uhitaji wa kuwa na wawakilishi Bungeni ni suala la msingi kwani kwa kuwa na wawakilishi wao Bungeni itawasaidia kutatua kero zao.


"Nitalipeleka suala hili kwenye mamlaka husika  kwa sababu mimi ni mwakilishi wa Mhe. Rais hivyo ombi la kuwa na uwakilishi ni la kimchakato, nitalipitisha kwa Mkuu wa Mkoa hivyo muwe na subira linapoendelea kutekelezwa na mamlaka," amesema Mhe Toba Nguvila


Pia Mhe. Nguvila amejibu suala la wazee kucheleweshwa vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuwa atalifuatilia makao makuu na kuwaomba wazee ambao bado hawajajiandikisha wafike ofisi za NIDA zilizopo Halmashauri wajiandikishe kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.


Aidha, wazee hao waliomba kuwa na kituo cha kumbukumbu ambacho kitaendelea kutunza/kuhifadhi historia ya asili ya wilaya ya Muleba. Jambo ambalo Mhe. Nguvila ameliridhia na kuahidi kulifanyia kazi jambo hili la ujenzi wa kituo cha kuhifadhia vitu vya kiutamaduni kwa kutafuta eneo la kujenga na kutafuta wafadhili ili kiweze kutumika kuhifadhia bidhaa za kiutamaduni na kutunza historia ya wilaya ya Muleba kwani hata watoto na vizazi vijavyo wataweza kunufaika na kituo hicho.


Kwa upande wa suala la Wazee kupatiwa chanjo ya Uviko 19 ameeleza kuwa tayari maelekezo yametolewa  kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya na kila zahanati ni lazima itoe chanjo ya Uviko 19 ili kuwasaidia wazee kupata chanjo hiyo na utekelezaji unaendelea. Hivyo amewambia wazee kwenda kwenye zahanati pamoja na vituo vya afya ili waweze kuchanjwa chanjo ya uviko 19.


"Nendeni mkachanje ili muishi salama kwa faida ya maisha yenu. Niwaombe sana, nendeni mkachanje kwa ajili ya usalama wa maisha yenu na afya zenu," amesisitiza Mhe. Nguvila


Ameendelea kueleza kuwa kuwa lengo la Mhe. Rais ni pamoja na wazee kuwa na kadi maalumu za Bima ya Afya kwa ajili ya kuwasaidia kutibiwa bure kutokana na umri waliotumikia Taifa. Kuwa wamelitumikia kwa muda mrefu, hivyo wanahitaji kupumzika na kupata kadi za bima ya afya zitakazowawezesha kupata matibabu bure. Huku akikemea suala la unyanyasaji kwa wazee hususani wakina mama wajane na kusisitiza kupewa haki zao kama inavyostahili.


Kwa pamoja wawakilishi wa wazee waliohudhuria mkutano huo wamemshukuru sana Mkuu wa Wilaya kwa kuja kuwasikiliza na kuwaahidi kutatua changamoto zao na zingine kuzifikisha katika mamlaka za juu kwa utekelezaji.

No comments:

Post a Comment

Pages