Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (katikati), akifafanua jambo kwa Mbunge wa Kilombero Mhe. Abubakar Asenga walipokutana wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara ambayo ujenzi wake unaendelea (kulia), ni Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Morogoro Eng. Baraka Mwambage.
Muonekano wa nguzo za daraja jipya la Kilombero mkoani Morogoro ambalo ujenzi wake unaendelea.
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameelezea kutoridhishwa
kwake na kasi ya ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara yenye urefu wa Km 66.9
inayojengwa na Mkandarasi Reynolds Construction Company (RCC), toka Nigeria.
Kufuatia hali hiyo amemuamuru Meneja Mradi wa
Ujenzi huo, Bw. Edan Tesfir kuondoka katika eneo la kazi ili kupisha wataalam
wengine kufanyakazi.
Ujenzi huo wa barabara kwa kiwango cha lami pia
unahusisha madaraja makubwa matano ulianza mwaka 2017 na ulitarajiwa kukamili
mwezi Oktoba mwaka huu lakini hadi sasa umefikia asilimia 37.5 hali inayoonesha
hautakamilika kwa wakati.
"Tanroads Mkandarasi hana spidi ya kumaliza mradi huu hivyo hakikisheni
mnazingatia mkataba ili haki itendeke na watakaoshindwa kazi waondolewe,
wananchi wanataka barabara," amesema Prof. Mbarawa.
Amesema barabara hiyo ambayo ni sehemu ya
barabara kuu inayoanzia Dumila- Kilosa- Mikumi -Kidatu hadi Ifakara itakapokamilika itaunganisha mkoa
wa Morogoro na mikoa ya Njombe na Ruvuma na hivyo kuhuisha uchumi wa mikoa hiyo
na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amemtaka
mkandarasi anayejenga barabara ya Rudewa-Kilosa Km 24 kuongeza kasi.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa
Morogoro Eng. Baraka Mwambage amesema wamejipanga kuwasimamia kikamilifu
wakandarasi mkoani humo ili kuepusha adha kwa wasafiri wakati wa mvua.
Naye Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga
amepongeza hatua ya ufuatiliaji wa karibu unaofanywa na TANROADS na kusisitiza
kuwa wananchi wanaisubiri kwa hamu barabara hiyo ili kuhuisha shughuli za
kilimo, uvuvi na biashara.
Zaidi ya shilingi bilioni 100 zinatarajiwa
kutumika katika ujenzi huo ambazo ni ufadhili toka nchi za Umoja wa Ulaya,
USAID na UKAID.
No comments:
Post a Comment