Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbasi akifungua Semina ya Waandishi wa Habari za Miches Jijini Dar es Salaam leo Septemba 04, 2021.
Na Grace Semfuko, MAELEZO, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali itaanza kujenga na kukarabati viwanja vitatu vya mazoezi vya Jijini Dar es Salaam, Dodoma na Geita, ambapo Shilingi Bilioni 9.5 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kwa mwaka huu wa fedha.
Amesema zoezi hilo litaendelea kila mwaka kwa kujenga na kukarabati viwanja vya aina hiyo vitatu kwenye maeneo mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kuibua, kukuza vipaji vya michezo na kuimarisha afya.
Ameyasema hayo Septemba 04, mwaka huu wakati akifungua semina ya Waandishi wa Habari za Michezo Jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa na Bodi ya Ligi, iliyolenga kuwapiga msasa waandishi hao katika kuandika habari zenye tija kwenye tasnia ya michezo nchini.
"Kuhusu miundombinu ya michezo, mnafahamu ahadi ya serikali ya kujenga uwanja wa mpira Dodoma, utakuwa mkubwa pengine kuliko hata huu wa Mkapa, na utakuwa mkubwa Afrika Mashariki na huenda kusini mwa Bara la Afrika, viwanja vitaendelea kujengwa hata kama sio kama huu wa Mkapa, sasa hivi tunakwenda kujenga kila mwaka viwanja vitatu vya aina ya Jakaya Kikwete Park kidongo chekundu Dar es Salaam, hivi tunavyoongea tayari tuna Bilioni 9.5 ambazo tutaanza kuboresha viwanja vya Indoor vya Dar, Dodoma na Geita, hiyo bajeti tunayo na kila mwaka tutachagua kupeleka kwenye maeneo mengine, Serikali inakuja na miradi hiyo ya viwanja vitatu kila mwaka, pia tutawekeza kwenye vituo na shule maalum ili kuendeleza na kuvikuza vipaji vingi vya michezo” amesema Dkt Abbasi.
Aidha amezungumzia namna ambavyo Serikali imejipanga kutatua baadhi ya changamoto za sekta ya michezo zinazojitokeza kwenye vipindi vya michezo vya Redio, Televisheni na kwenye magazeti ikiwepo ya ufadhili na uboreshwaji wa miundombinu ya sekta hiyo.
“Serikali inasikiliza vipindi vyenu vya michezo, kila ukifungua radio, TV au ukisoma kurasa za magazeti kuna malalamiko tunayasikia, lamiko la kwanza ni kwamba hatujawekeza ufadhili kugharamikia michezo, tulilichukua na kulifanyia kazi, leo tunavyozungumza tumeshapata fedha katika michezo ya kubahatisha, tumeshapambania na kuanzia sasa asilimia tano fedha hizi zitaenda mfuko wa maendeleo ya michezo na kuanzia mwezi huu wa tisa zitaanza kuingizwa kwenye akaunti ya maendeleo ya michezo na pia tunakamilisha taratibu za kurejesha bahati nasibu ya Taifa ambayo kwa mujibu wa sheria ilipaswa kuchangia asilimia 50, tunataka kuirudisha upya ili fedha ziende kwenye mfuko huo” amesema Dkt Abbasi.
Katika Semina hiyo Dkt Abbasi pia amewataka Waandishi wa Habari za Michezo nchini, kuwa wabunifu na kuzingatia weledi katika kuandika habari ili kuvutia wasikilizaji na wasomaji wa habari zao.
Dkt Abbasi pia amewataka waandishi hao kubuni misamiati mipya ya lugha ambayo pamoja na kuvutia wasikilizaji na wasomaji wa habari zao, pia itasaidia kupanua zaidi lugha la Kiswahili ambayo imekuwa kivutio kwa mataifa mengine.
No comments:
Post a Comment