· Mikakati yabainishwa kuhakikisha TEHAMA inawafikia wananchi wengi zaidi
· TCRA yabainisha nia yake ya kushirikiana na serikali katika kukuza TEHAMA nchini
Na: Robin Ulikaye
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imebainisha dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanakuza uchumi wa kisasa unaoendana na falsafa ya uchumi wa kidijitali na uchumi wa buluu/bluu.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar Amoul Hamil wakati akikabidhi kituo cha Kompyuta kwa Umma (Tele-Center) kwa Skuli ya Sekondari Tumbatu kilichojengwa kwa udhamini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa shabaha ya kutoa huduma za TEHAMA kwa walimu,wanafunzi na jamii ya kisiwa kidogo cha Tumbatu kilichopo umbali mchache kutoka kisiwa cha Unguja.
“Matarajio yetu kama serikali ni kwamba sasa tunakwenda kutekeleza dhamira yetu ya dhati, ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza dira zetu za Maendeleo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na matumizi bora na matumizi mapana ya suala zima la TEHAMA” aliongeza Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar Amoul Hamil akiwa sambamba na Mkuu wa Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano Zanzibar Bi. Esuvatie Masinga wakifurahia jambo baada ya kukabidhi kituo cha TEHAMA katika Shule ya Sekondari Tumbatu, Zanzibar. Picha na: TCRA
Alibainisha kwamba wizara yake itakachofanya ni kuhakikisha inaweka mikakati ya kuhakikisha shule nyingi zaidi na jamii ambazo hazijafikiwa na TEHAMA zinapata huduma hiyo muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa kisasa.
“Niwahakikishie baadhi ya wadau naweza kuwasiliana nao ili kuhakikisha tunakuza TEHAMA kwa manufaa ya jamii zetu” aliongeza Katibu Mkuu.
Kituo hicho cha TEHAMA ambacho kimedhaminiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni kituo cha Sita miongoni mwa vituo vilivyopatiwa miundombinu wezeshi ya TEHAMA chini ya mpango wa TCRA wa fungu la TEHAMA (ICT-pack) ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za Mawasiliano hasa maeneo ambayo hayajafikiwa, kikitarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi Elfu Tatu.
Akizungumzia kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wakati wa kukabidhi vifaa vya kituo hicho vilivyowekwa kwenye darasa maalum la kompyuta lililounganishwa na mtandao wa Intaneti kwenye shule ya Sekondari ya Tumbatu, Mkuu wa TCRA Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie Masinga alibainisha kuwa lengo la TCRA ni kuhakikisha huduma za TEHAMA zinakuwa jumuishi na kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini.
“TCRA Ofisi ya Zanzibar katika kutekeleza mpango huu wa kutoa kwa jamii vifaa vya TEHAMA tumeamua kwa awamu hii kujikita kwenye visiwa ndani ya visiwa kwa upande wa hapa Unguja tuna vituo viwili tumevifungua; hiki ni kituo cha Sita na tuna mpango kwamba mwaka ujao wa fedha tutaomba fedha ili twende kisiwa cha Kojani na maeneo mengine ya Zanzibar lengo likiwa kufikisha huduma za Mawasiliano na TEHAMA kwa jamii kubwa zaidi” alifafanua na kuongeza Bi. Masinga.
Mkuu wa Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano Zanzibar Bi. Esuvatie Masinga akisaini Hati ya Makabidhiano ya Kituo cha TEHAMA katika kisiwa cha Tumbatu, Zanzibar kilichofadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwezesha upatikanaji wa huduma za TEHAMA katika elimu na jamii. Picha na: TCRA
Kituo hicho kikiwa ni kituo cha Sita miongoni mwa vingine vilivyofadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kitahudumia shule mbili zilizopo katika kisiwa cha Tumbatu ambacho ni moja miongoni mwa visiwa vikubwa vya Zanzibar sambamba na kuhudumia jamii yote,wanafunzi na walimu.
Wanufaika wa mradi huo wameelezea furaha yao kwa kujengewa kituo cha TEHAMA kwa kuwa kitarahisisha upatikanaji wa huduma za elimu na kuwawezesha wananchi wa Tumbatu kuwasiliana kwa urahisi na kuendana na ukuaji wa TEHAMA.
Akiwasilisha salamu za wakazi wa Tumbatu na Menejimenti ya Shule, Mkuu wa shule hiyo alieleza kuwa kituo hicho sit u kitasaidia ujifunzishaji miongoni mwa wanafunzi lakini pia kitawezesha upatikanaji wa huduma za TEHAMA miongoni mwa wanafunzi wa shule mbili za sekondari zilizopo kwenye kisiwa hicho.
“Nipende kuwashukuru kwa hisani yenu na kukuahidini kwamba kituo hiki hakitakuwa mali ya shule ya sekondari Tumbatu pekee bali hata wenzetu wengine wa skuli ya sekondari Jongowe na wananchi wengine wa kisiwa hiki watanufaika na uwepo wa kituo hiki cha TEHAMA” alisisitiza Mwalimu mkuu Jala Pandu Khamis.
Awali Katibu Mkuu aliwaalika wadau wengine wa Mawasiliano kuwezesha ukuaji wa TEHAMA hasa katika taasisi za elimu na maeneo ambayo hayajafikiwa na TEHAMA visiwani Zanzibar ili kuwezesha kutimia kwa azma ya serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali na uchumi wa bluu kwa kuwa falsafa hizo mbili kuelekea uchumi mkubwa zinashabihiana.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikiwezesha upatikanaji wa huduma za TEHAMA katika maeneo anuai kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa wezeshi vya TEHAMA kwa wananchi hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa kwa sehemu kubwa na huduma za Mawasiliano hasa ya kompyuta zikiwemo taasisi za mafunzo na elimu.
Mkuu wa Skuli ya Sekondari Tumbatu, Zanzibar akionyesha wananchi na wanafunzi wa Tumbatu Hati ya Makabidhiano wa Kituo cha TEHAMA kilichofadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA na kukabidhiwa kwa shule hiyo. Kituo hicho kilichounganishwa na Intaneti kitawezesha Mawasiliano kwa wananchi wote wa Kisiwa cha Tumbatu. Picha na: TCRA
No comments:
Post a Comment